Habari za Punde

WAZIRI KIGWANGALLA ATUA NCHINI HISPANIA, AUNGURUMA


Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiwa ni miongoni mwa Wazungumzaji  kwenye kongamano la 10 la Uwekezaji na Biashara katika sekta ya Utalii Afrika (Investour) lililofanyika jana katika jiji la Madrid nchini Hispania ambapo katika Kongamano hilo Waziri Kigwangalla alitumia fursa hiyo  kuwaita Wawekezaji kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya Utalii na viwanda.
Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Washiriki wa kongamano la 10 la Uwekezaji na Biashara katika sekta ya Utalii Afrika (Investour) lililofanyika Jana katika jiji la Madrid nchini Hispania ambapo katika Kongamano hilo Waziri Kigwangalla alitumia fursa hiyo kuwaita Wawekezaji kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya Utalii na viwanda.

Na Mwandishi wetu-Hispania
Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Hamisi Kigwangalla amewaita Wawekezaji kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya Utalii wakati aliposhiriki kongamano la 10 la Uwekezaji na Biashara katika sekta ya Utalii Afrika.

Kongamano hilo limefanyika jana katika jiji la Madrid nchini Hispania likiwa limeandaliwa na Shirika la Utalii  la Umoja wa Mataifa (UNWTO)kwa kushirikiana na Taasisi za Casa Afrika pamoja na Taasisi yamaonesho ya Biashara ya Madrid (IFEMA) na kushirikisha nchi mbali mbali duniani.

Katika Kongamano hilo, Waziri Kigwangalla alipata fursa ya kuwa mmoja wa wazungumzaji ambapo amewahakikishia Wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza nchini Tanzania kwamba ni sehemu salama ukizingatia hali ya amani na utulivu iliyopo nchini lakini pia kuna vivutio vingi vya utalii na fursa za kuwekeza.

"Nawakaribisheni nyote, Njooni Tanzania muwekeze kufuatia uwepo wa mazingira na miundombinu bora kwa ajili uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na viwanda" Alisema

Waziri Kigwangalla pia  alitumia nafasi hiyo kwa kuutangaza ukanda mpya wa kusini mwa Tanzania ambao umejaliwa kuwa na vivutio vya Utalii vya kipekee vinavyopatikana katika  Hifadhi ya Taifa ya  Ruaha, Mikumi pamoja  Pori la Akiba Selous.

Katika hatua nyingine , Waziri Kigwangalla wakati akizungumza  katika kongamano hilo aliwaeleza washiriki hao  kuhusu  juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli kwa kutaja mifano michache kama vile kufufua kampuni ya ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya sita pamoja kujenga chanzo kikubwa cha kuzalisha  umeme katika mto Rufiji.

Alisema serikali ya Tanzania pia inaendelea na mradi wa kisasa wa ujenzi wa njia mpya ya kisasa ya reli (Standard Gauge) pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.

Alibainisha kuwa kutokana na juhudi hizo zilizochukuliwa  na Serikali hiyo, sekta ya utalii itaweza kusonga mbele ikiwa pamoja na kurahisisha usafiri kwa watalii pamoja na  wawekezaji kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.