Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Akihutubia Wakati wa Kuhairisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Baraza La Wawakilishi leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mawaziri pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Balozi Seif wakati akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Balozi Seif akibadilishana Mawazo na Waziri wa Ujenzi, Mawasilioano na Usafirishaji Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mamboya Kushoto na Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele Mh. Ali Suleiman Ali {Shihata } Nje ya Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Balozi Seif  Kushoto akisalimiana na kumpongeza Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa baada ya kuteuliwa na Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Balozi Seif Kushoto, Naibu Waziri Ujenzi Mh. Mohamed Ahmada kushoto ya Balozi Seif na Waziri wa Elimu Mh. Rziki Pembe Juma Kulia wakimpongeza Balozi Ramia baada kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kufuatia Uteuzi wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein alioufanya Mwishoni mwa Wiki iliyopita.
Picha na – OMPR – ZNZ.

N.Othman Khamis. OMPR.
Wakati Wananchi wakitolewa wito wa kuyatunza maeneo yenye vianzio vya vya Maji kwa hali na Mali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafikiria kuyahifadhi Kisheria maeneo yote yenye vianzio hivyo kama ilivyohifadhi Kisheria Misitu Mikuu ya Jozani na Ngezi ili kuilinda  Rasilmali hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii.
Akiahirisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema maeneo ya vianzio vya Maji hayataruhusiwa kufanywa shughuli zozote za Kibinaadamu, hivyo aliwanasihi wale waliojenga katika maeneo hayo wajitayarishe kuondoka kwa hiari yao.
Balozi Seif alisema Serikali imejipanga kupambana na changamoto mbali mbali zinazoikabili Sekta ya Maji ikiwemo upotevu wa Maji unaosababishwa na uchakavu wa Miundombinu, uvamizi wa vianzio vya Maji, mwitiko mdogo wa kuchangia huduma ya Maji pamoja na utumiaji ovyo wa Maji majumbani na Ofisini.
Alisema lengo la Serikali Kuu ni kuongeza Miundombinu  itakayowezesha kujenga nguvu za kuwapatia huduma ya Maji safi na Salama Wananchi wote Unguja na Pemba ambapo usambazaji wa huduma hiyo unakadiriwa ufikie asilimia 97%  kwa maeneo ya Mjini na asilimia 85% Vijijini ifikapo Mwaka 2020.
Aliwaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi washirikiane na Serikali katika kupambana na changamoto hizo ili kuihifadhi Rasilmali hiyo ya Maji inayoonekana kupungua kwa kasi Duniani kutokana na sababu tofauti ikiwemo kuchafuka kwa Mazingira.
Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani {WHO} ifikapo Mwaka 2025 nusu ya Watu wanaoishi Duniani wapatao zaidi ya Bilioni Nane watakuwa wanaishi kwenye maeneo yenye matatizo ya upatikanaji wa huduma ya Maji.
Akizungumzia Mipango ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inatayarisha Mkakati Shirikishi wa Kitaifa wa usimamizi wa Taka taka wenye lengo Kuu la kuhakikisha taka zote zinazozalishwa Nchini zinasimamiwa ipasavyo ili Miji yote iwe safi kwa faida ya Kiuchumi, Kimazingira pamoja na Kijamii.
Alisema suala la uchafuzi wa mazingira Nchini hasa utupaji taka na uchimbaji mchanga ovyo bado linaendelea kuleta changamoto kwa Taifa na Wananchi wenyewe katika maeneo mbali mbali Nchini.
Balozi Seif alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zina uwezo wa kusimamia wastani wa asilimia 50% ya Taka zote zinazozalishwa zikiwa na wastani wa Tani Laki 238,700 kwa Mwaka Unguja na Pemba.
Alisema ni jambo la kusikitika kuona taka zinazobakia hutupwa ovyo vichakani badala ya kupelekwa kwenye jaa jipya lililotengenezwa Kitaalamu katika eneo la Kibele.
Alionywa kwamba kuna taarifa zinazoelezea uwepo wa baadhi ya Hoteli za Kitalii hutumia Makampuni ya kukusanya taka taka ambazo kwa tamaa zao za kutaka faida kubwa huishia kuzitupa taka taka hizo kwenye vichaka badala ya eneo maalum lililotengwa na Serikali liliopo Kibele.
Balozi Seif  alizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzanzia sasa kuhakikisha kwamba Hoteli zote zilizomo kwenye Mamlaka yao zinatumia Makampuni yanayofuata Sheria ya Utunzaji wa Mazingira badala ya kuzitupa ovyo katika Mitaa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo kwenye mitaro hasa kipindi hichi kinachokaribia kuingia msimu wa Mvua za Masika ambazo wakati mwengine husababisha mafuriko yanayoweza kuleta maafa hapo baadae.
Alisema juhudi za Serikali ilizozichukuwa na inayoendelea kuzichukuwa katika kukabiliana na maafa haziwezi kufanikiwa bila ya mashirikiano ya kina pamoja na Wananchi wake.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake imejipanga kupambana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua hizo kwa ujenzi wa daraja la Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe sambamba na ujenzi wa Mitaro inayoendelea ya maji ya Mvua katika maeneo mengi ya Mkoa Mjini Magharibi ambayo huonekana kuathirika zaidi wakati wa mvua kubwa zinaponyesha.
Akizungumzia jitihada zinazochukuliwa na Serikali za mapambano dhidi ya vitendo vya Udhalilishaji Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kadhia hiyo bado inaendelea kuwatesa Wanawake na Watoto siku hadi siku na hivi sasa vinaonekana kutokea kwa njia nyengine.
Balozi Seif alisema katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Disemba 2018, jumla ya matukio Mia 466 yanayohusu vitendo vya udhalilishaji vikiwemo kubaka 257, kulawiti 56, kuingilia kinyume cha maumbile 8, kutorosha 70, shambulio la aibu 75 yameripotiwa katika vyombo vya Dola.
Alisema kwa vile hali bado ni mbaya katika Jamii aliwashauri na kuwaaidhi Wazazi pamoja na Jamii yote kuwa karibu kwa kufuatilia mienendo ya Watoto wao ili kuweza kujua walipo na wanachofanya muda wote.
Hata hivyo Balozi Seif  aliwakumbusha Masheha na Wananchi Mitaani wanapogundua uwep wa Mtu asiyeeleweka  katika maeneo yao wanapaswa kutoa Taarifa haraka kwenye vyombo husika ili kufuatiliwa na hatimae kujiridhisha na hali halisi ya mazingira ya uwepo wa Mtu huyo.
Alitoa msisitizo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Viongozi wa Dini, Asasi za Kiraia, Makundi ya Malezi kuendelea kuwaelimisha Wananchi Mitaani katika kusimamia Malezi bora yanayoendana na Mila, Silka na Tamaduni zilizoachwa na Wazee waliopita.
Akigusia Sekta ya Utalii ikiwa ni miongoni mwa muhimili muhimu unaotegemewa na Taifa katika Uchumi wa Nchi Balozi Seif  alisema tukio lolote linaloweza kuhatarisha Sekta hiyo halitavumiliwa na Serikali kwani linaweza kuviza Ustawi wa Jamii kupitia Sekta hiyo.
Alitahadharisha kwamba Serikali inatoa onyo kali kwa wale wanaoendesha vitendo vya uhalifu kwenye Fukwe wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo mbaya inayolitia aibu Taifa kwa wageni wanaoamua kufika Nchini kimatembezi.
“ Hatutamuonea haya Mtu ye yote atakayeendesha vitendo vya uhalifu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”. Alionya Balozi Seif.
Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwataka Vijana wanaofanya biashara ndogo ndogo kuacha mtindo wa kuwabughudhi Watalii wanapotembea ufukweni kwa kuwalazimisha kununua bidhaa zao hata kama hawazihitaji.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  walijadili Miswada Miwili, kupokea Ripoti za Kamati za Baraza ikiwemo ile ya Kamati Teule ya kuchunguza Majengo ya Skuli 19 za Sekondari  katika Mkutano wa Kumi na Tatu za Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar.
Pia Wajumbe hao walipokea Taarifa ya Serikali inayohusu Hoja ya Mjumbe kuliomba Baraza la Wawakilishi kutoa Maazimio ya kushughulikia kwa haraka tatizo la kuharibika kwa vifaa Tiba vya Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba pamoja na kupokea Muelekeo wa Mpango wa Taifa.
Jumla ya Maswali ya msingi yapatao Mia Moja na Thalathini na Tano na Mia Moja na Kumi na Saba ya nyongeza yaliulizwa na Wajumbe wa Baraza la Waakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara Tofauti.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar {BLW} limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 08 Mei Mwaka 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.