Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, zilizofanyika Kitaifa Kisiwani Pemba Wilaya ya Wete Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Pemba.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa umadhubuti wa nchi pamoja na
utajiri wake unategemea kwa kiasi kikubwa jinsi gani nchi hiyo imejidhatiti
katika kuendeleza na kudumisha utawala wa sheria (Utawala Bora).
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar yaliyofanyika huko katika ukumbi
wa Baraza la Wawakilishi, Wete Pemba, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alisema kuwa maadhimisho ya siku ya Sheria yana umuhimu mkubwa katika
kutoa mwamko kwa wananchi katika kuzifahamu na kuzitii sheria za nchi zikiwa
ndio msingi mkubwa wa kukuza utulivu, amani na maendeleo.
Aliongeza kuwa suala la
kuzifahamu na kuzitii sheria hupelekea kuishi kwa nidhamu na misingi ya
kuheshimiana katika maisha ya kila siku kwani sheria lazima zitambuliwe ili
wananchi waweze kupambanua haki na wajibu.
Alisema kuwa ikiwa jamii
itaishi bila ya kuzifata sheria basi utakosekana ustaarabu katika utekelezaji
wa mambo kwani sheria ni suala nyeti linalogusa maisha katika nyanja mbali
mbali.
Dk. Shein alisema kuwa
kwa msingi huo Mamlaka tatu zilizopo katika mfumo wa mgawanyo wa madaraka yaani
mamlaka ya Utendaji ambayo ni Serikali, Mamlaka ya Kutunga Sheria yaani Baraza
la Wawakilishi pamoja na Mahkama ni lazima zihakikishe zinashikamana bila ya
kuathiri uhuru wa sehemu moja.
Katika hotuba yake hiyo,
Rais Dk. Shein pia aliwahimiza wananchi wote kuendelea kutii sheria za nchi
kama Katiba inavyoelekeza huku akiwahiziwa viongozi wa dini zote zinazofuatwa
na wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla kuendelea kuhubiri utii wa
sheria za nchi.
Alieleza kufurahishwa na
Kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “ Uimarishaji wa Taasisi za Umma ni Ustawi Bora
wa Upatikanaji wa Haki kwa Jamii” alisisitiza kuwa Kauli mbiu hiyo inakwenda
sambamba na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha taasisi za umma kwa maendeleo ya jamii.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Serikali katika vipindi mbali mbali na awamu zote saba tafauti imefanya
jitihada kubwa kuimarisha taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa ustawi wa
upatikanaji wa haki kwa jamii unakuwa siku hadi siku.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba
imefanya jitihada kubwa za kuimarisha taasisi za umma zinazosimamia haki
na sharia, Taasisi zinazoshughulikia huduma za jamii, elimu, afya, maji safi na
salama, kilimo, miundombinu ya usafiri, utalii, michezo na mengineyo.
Akinukuu Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 18 (2), Rais Dk. Shein ameendelea kuwasisitiza
viogozi wenzake wahakikishe wanatekeleza amatakwa ya Kikatiba ya kutoa taarifa
kwa wananchi kwa kujiwekea utaratibu maalum wa kutoa taarifa kwa wananchi
kupitia vyombo ya habari.
Rais Dk. Shein alieleza
jitihada za kuziimarisha taasisi zinazosimamia haki na sharia zinazozingatia
maendeleo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020 ambayo katika
Ibara ya 145 inafahamisha jinsi ya kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa ufanya maboresho katika utendaji wa vyombo
vya maamuzi ikiwemo Mahkama, Ofisi ya Mwendesha Mashataka na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alieleza hatua zilizochukuwa na Serikali katika matengenezo ya majengo ya
Mahkama huku akieleza kuwa Serikali imo mbioni kujenga jingo la Mahkama Kuu
mpya pamoja na jingo la skuli ya sharia yaani “Law School,” huko Tunguu ambapo
jumla ya TZS bilioni 5.0 zimetengwa kwa kazi hiyo.
Akieleza masikitiko yake
Rais Dk. Shein alieleza kusikitishwa na Jeshi la Polisi inavyoingilia vyombo
vya Sheria katika suala zima la kupambana na rushwa.
Aliongeza kuwa hivi karaibuni kumetokea tokea
ambalo halileti picha nzuri hali iliyopelekea jeshi hilo la Polisi kuanza kuwatisha
wafanyakazi wa Taasisi ya Kupambana na rushwa ZAECA na kusisitiza kuwa taasisi
hiyo iwachwe ifanye kazi yake kwa uhuru na sheria zilizowekwa.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa katika kuhakikisha tatizo la kupata ushahidi kwa kesi za makosa
ya jinai yanayohitaji uchunguzi, Serikali imejenga Maabara mpya ya kisasa ya
Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo imenunua
vifaa vipya na nyenzo mbali mbali ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuchunguza
vinasaba vya urithi kwa kupima DNA na kutoa majibu ya uhakika.
Rais Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuongeza kasi zaidikatika kuliondosha tatizo la
ucheleweshaji wa kesi ili kuweza kupata ufanisi utakaooana na ajuhudi kubwa za
Serikali za kuimarisha taasisi hizo.
Alieleza kuwa Majaji,
Mahkama pamoja na Makadhi ni kioo cha jamii hivyo suala la kuzingatoa maadili
ya kazi ni wajibu wa kila mfanyakazi lakini jamii hupata mshtuko Zaidi pindi
inaposikia kuwa Jaji amam Hakimu Fulani ana tabia zinazokwenda kinyume na
maadili ya kazi na jamii anayoishi.
“Kwa hivyo ni vyema kwa
Majaji na Mahakimu mkaendelea kutekeleza wajibu wenu kwa kuzingatia maadili ya
kazi zenu ndani ya jamii mnayoishi katika maisha yenu ya kila siku, sina shaka
kwamba mtaendelea kujijengea sifa njema ili muendelee kwua mfano bora miongoni
mwa watumishi wa umma”alisema Dk. Shein.
Pia, alipokea ombi la
kutaka Mawakili kuandaliwa Sheria yao itakayowapelekea kufanya kazi zaokwa
ufanisi mkubwa Zaidi na kuitaka Serikali kuandaa mswada wa sharia juu ya ombi
hilo.
Alieleza kuwa mafanikio
ni makubwa yaliopatikana katika masuala ya kisheria hapa Zanzibar kuliko
changamoto zilizopo.
Nao viongozi mbali mbali
kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala
Bora walieleza mafanikio yaliopatikana katika suala zima la sharia hapa
Zanzibar na kueleza hatua zinazoendelea katika kuhakikisha mafanikio Zaidi
yanapatikana.
Pia, walipongeza wazo la
Rais Dk. Shein la kufanywa sherehe hizo kisiwani Pemba mwaka huu na kueleza
jinsi sherehe hizo zilivyofana.
Dk. Shein pia, alizindua
kitabu cha Sheria cha mwaka huu wa 2019 ambacho kila yanapofika maadhimisho ya siku
ya sharia huzinduliwa kitabu.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment