Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza na Viongozi wa UWT wa Afisi Kuu ya Zanzibar Ikulu leo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ukiongozwa na Makamu Mwenyekiti UWT.Bi.Thuwaiba Editon Kisasi,wakiwa katika ukumbi wa Ikulu wakiwa katika mazungumzo hayo.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amepongeza azma ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kufanya Kongamano la Kitaifa la kupongeza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)kwa kipindi cha miaka 3 ya uongozi wake.

Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wakiwemo Wajumbe wa Kamati Tekelezaji ya Umoja huo Ikulu mjini Zanzibar ambapo Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kupongeza rai na azma hiyo ya Umoja huo wa (UWT).

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar alieleza kuwa Kongamano hilo litatoa mwanga katika kutambua juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kutekeleza majukumu yake ambayo ni pamoja na kuimarisha miradi ya maendeleo Unguja na Pemba, mjini na Vijijini kwa manufaa ya wananchi wote ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani hiyo ya CCM.

Hivyo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza Umoja huo kwa kufikiria kufanya jambo hilo muhimu ambalo litatoa taswira nzuri kwa jamii ambayo inatambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali yao katika kuwaletea maendeleo endelevu.

Aidha, Rais Dk. Shein alipongeza kwa maandalizi ya Kongamano hilo ambalo litaanzia Kisiwani Pemba na baadae kufanyika Unguja huku akisisitiza haja ya kuendelea kuungwa mkono Jumuiya hiyo ili izidi kuimarika na kuleta mafanikio kwa Taifa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelezwa kwa umoja na mshikamano ndani ya Jumuiya hiyo ambayo imeweza kupata mafanikio makubwa na kuimarika zaidi tokea kuanzishwa kwake.

Nao ungozi wa Jumuiya ya (UWT) ukiongozwa na Makamo Mwenyekiti wake Thuwaiba Edington Kisasi ulieleza azma na malengo ya Kongamano  la Kitaifa la kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka 3 pamoja na kutangaza yale yote yaliyoyomo ndani ya Ilanin hiyo ya mwaka 2015-2020.

Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Rais Dk. Shein ametekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi katika uongozi wake tena kwa kiwango kikubwa  Mjini na Vijini katika nyanja mbali mbali hivyo, kuna kila sababu ya kuendelea kumpongeza kutokana na juhudi zake hizo ambazo ni za mfano.

Katika maelezo yake Kisasi alieleza kuwa Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika tarehe 9 Machi 2019 kwa upande wa Pemba na tarehe 16 Machi 2019 kwa upande wa Unguja ambalo litawashirikisha kikamilifu akina mama.

Alieleza kuwa Kamati ya kufanikisha Kongamano hilo inaongozwa na Mwenyekiiti wake Mgeni Hassan Juma Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Wajumbe wengine.

Aidha, Makamu huyo Mwenyekiti wa (UWT), alieleza kuwa Makongamano hayo yote yatakayofanyika Unguja na Pemba yataambatana na ziara maalum za viongozi hao wa Jumuiya hiyo katika Mikoa yote ya Zanzibar.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa (UWT), ulimueleza Rais Dk. Shein mikakati iliyoiweka katika kuhakikisha wanafanikisha Makongamano hayo wakatayofanya Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na ziara wanazotarajia kuzifanya.

Viongozi hao walitumia fursa hiyo kuendelea kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuujali na kuuthamini Umoja huo sambamba na kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa vitendo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.