Habari za Punde

Ujio wa Mashua ya Mazingira Zanzibar na Uzinduzi wa Usafi wa Mazingira Ufukwe wa Forodhani Zanzibar.

 Kikao cha Washirika wanaosimamia na kushughulikia masuala ya Mazingira kutoka Taasisi za Umma, Binafsi pamoja na zile za Kimataifa  wakikutana kujadili ujio wa Mashua ya Mazingira chini ya Mwenyekiti wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi kilichofanyika Vuga Mjini Zanzibar.
Ofisa wa Uratibu katika masuala ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bibi Clara Makenya akitoa maelezo ya masuala yatakayofanyika wakati wa uzinduzi wa kampeni ya mazingira katika eneo la Forodhani.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji DCI Nasra Juma Mohamed akifafanua jambo kwenye kikao cha washirika wa masuala ya usimamizi na ushughulikiaji wa mazingira.
Baadhi ya wajumbe wa Kikao cha Washirika wanaosimamia na kushughulikia masuala ya Mazingira kutoka Taasisi za Umma, Binafsi pamoja na zile za Kimataifa  wakikutana kujadili ujio wa Mashua ya Mazingira.
Baadhi ya wajumbe wa Kikao cha Washirika wanaosimamia na kushughulikia masuala ya Mazingira kutoka Taasisi za Umma, Binafsi pamoja na zile za Kimataifa  wakikutana kujadili ujio wa Mashua ya Mazingira.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Ujio wa Mashua ya Mazingira iliyotengenezwa kutokana na malighafi ya Plastiki kutoka Nchini Kenya chini ya ushauri wa Taasisi ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa unaiweka Zanzibar katika Ramani ya Dunia kwenye mapambano yake dhidi ya uchafuzi wa mazingira.
Mashua hiyo ambayo tayari imeshaondoka jana kutoka Mombasa Nchini Kenya inaingia Wete Kisiwani Pemba, Kupitia Mkoani Pemba, Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja na kutarajiwa kuingia  Forodhani Mjini Zanzibar mnamo Tarehe 6 Mwezi huu.
Kikao cha Washirika wanaosimamia na kushughulikia masuala ya Mazingira kutoka Taasisi za Umma, Binafsi pamoja na zile za Kimataifa  walikutana kujadili ujio wa Mashua hiyo chini ya Mwenyekiti wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi kilichokutana Vuga Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Nd. Juma Mjaja aliwaelezea Wajumbe wa Kikao hicho kwamba lengo la Mashua hiyo ni kuihamasisha Jamii juu ya kuelekeza nguvu zao katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira yanayoleta Mabadiliko ya Tabia Nchi Duniani.
Nd. Mjaja alisema Tarehe 7 Febuari siku Moja baada ya kuwasili Mashua hiyo kutakuwa na uzinduzi wa usafi wa Mazingira katika Ufukwe wa Forodhani utakaoshirikisha Taasisi tofauti zinazojishughulisha na masuala ya Mazingira Zanzibar.
Alisema pamoja na mambo mengine kwenye uzinduzi huo pia kutakuwepo Maonyesho madogo ya Wajasiri amali yatakayohusisha bidhaa zinazotengenezwa na vitu vinavyotokana na taka taka za Plastiki.
Naye kwa upande wake Ofisa wa Uratibu katika masuala ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bibi Clara Makenya alisema usafishaji wa Mazingira katika Pwani ya Forodhani itaongozwa na Muungano wa Taasisi za Kimazingira ya Les Do It Company Zanzibar.
Bibi Clara alisema yapo matarajio makubwa kwa Rais wa Taasisi ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa kuhudhuria Kampeni hiyo ya Kidunia ya uzinduzi wa usafi wa Mazingira hapa Zanzibar.
Alisema inapendeza kuona wakati watu mbali mbali wameshaonyesha nia ya kushiriki Kampeni ya uzinduzi huo hata Uongozi wa Mahoteli yaliyopo Visiwani Zanzibar yameshaonyesha nia pia ya kupunguza matumizi ya plastiki katika shughuli zao za kila siku.
Akitoa shukrani zake Mwenyekiti wa Kikao hicho akiwa pia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi alisema Zanzibar kama vilivyo Visiwa vyengine Duniani imepata Heshima hiyo kutokana na mikakati yake ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki.
Nd. Mitawi alisema Zanzibar imeanza kupiga marufuku mifuko ya plastiki tokea mwanzoni mwa Miaka ya 90 licha ya kupata vikwazo mbali mbali vilivyosabishwa na baadhi ya wafanyabiashara lakini imeweza kufanikiwa vyema na kuwa mfano kwa Nchi ilizo ukanda wa Afrika Mashariki.
“ Zanzibar imekuwa darasa kubwa  la mapambano dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki katika ukanda wa Afrika mashariki”. Alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huto Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Alieleza kwamba Mataifa mengi Ulimwenguni hivi sasa yako katika kampeni Maalum ya mapambano dhidi ya bidhaa zinazotokana na plastiki ambapo alizishukuru Taasisi za Umoja wa Mataifa kwa msimamo wake wa kuunga mkono Kampeni hizo.
Nd. Mitawi alifahamisha kwamba harakati hizo zitaendelea kuiwezesha Zanzibar kuelekea katika mafanikio ya kujitangaza Kiutalii Duniani kutokana na ujio wa Viongozi Waandamizi wa Umoja wa Mataifa wanaoshughulikia Mazingira kushiriki kwenye uzinduzi huo muhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.