Habari za Punde

Bodi ya chakula na dawa Zanzibar yaangamzia Tani 520 za sukari isiyokuwa na Kiwango

 Gari zikiwa zimepakia sehemu ya tani 520 za sukari bandarini Malindi zikisubiri kupelekwa mashimo ya mchanga Zingwezingwe, Wilaya Kaskazini B, kwa ajili ya kuangamizwa baada ya kugundulika kukosa kiwango kwa matumizi ya wananchi.
 Shehena ya sukari ikiwa imemwagwa katika mashimo ya mchanga ya Zingwezingwe Wilaya Kaskazini B ikisubiri kuangamizwa baada ya kukosa kiwango kwa matumizi ya wananchi.
 Wafanyakazi wa Bodi ya Chakula na Dawa wakimwaga sukari katika mashimo ya mchanga ya Zingwezingwe Wilaya ya Kaskazini B wakiwa katika zoezi la kuiangamiza sukari iliyokosa kiwango kwa matumizi ya wananchi.
 Wafanyakazi wa Bodi ya Chakula na Dawa wakimwaga sukari katika mashimo ya mchanga ya Zingwezingwe Wilaya ya Kaskazini B wakiwa katika zoezi la kuiangamiza sukari iliyokosa kiwango kwa matumizi ya wananchi.

Gari aina ya kijiko ikiangamiza sukari katika mashimo ya mchanga ya Zingwezingwe Wilaya Kaskazini B baada ya kugundulika kukosa kiwango kwa matumizi ya wananchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chakula na Dawa Zanzibar Dk. Khamis Ali akizungumza na waandishi wa habari kwenye mashimo ya mchanga Zingwezingwe wakati wa kuangamiza sehemu ya tani 520 za sukari iliyoingizwa nchini ikiwa haina kiwango kwa matumizi ya wananchi.
PICHA NA RAMADHANI ALI MAELEZO ZANZIBAR

Na Maryam Kidiko  - Maelezo.      02.03.2019                                         
Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Hassan  Khamis Hafidh amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukuwa hatuwa kali kwa Mfanyabiashara yoyote atakaeingiza bidhaa isiyokuwa na kiwango kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
 Aliyasema hayo Bandari ya Malindi Zanzibar alipofika kuangalia zoezi la kuhamisha tani 520 za sukari kwenda kuangamizwa kwenye mashimo ya mchango katika kijiji cha Zingwezingwe baada ya kugundulika kukosa kiwango kwa matumizi ya binaadamu.
Alisema kuwa Serikali ipo makini kulinda afya za Wananchi wake hivyo haitakubali kuingizwa bidhaa yoyote isiyofaa kwa matumizi ya wananchi  ili kuwaepusha na maradhi.
Aidha alisema ulinzi mkali wa vikosi vya ulinzi na usalama umeandaliwa kwa ajili ya kusimamia sukari hiyo ili kuhakikisha hakuna mtu atakaefanya mbinu ya kuipata mpaka zoezi zima la kuiangamiza limalizike.
Aliwataka Wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa njia za halali na kuacha tabia ya kununua bidhaa za gharama nafuu bila ya kuangali ubora wake kwa lengo la kutafuta faida kubwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Chakula na Dawa Dk. Khamis Ali Omar alisema Makontena 20 ya sukari isiyo na kiwango yenye uzito wa Tani 520 ya Kampuni ya Rashid Ali Trader yaliingizwa Zanzibar mwaka uliopita kwa awamu mbili na alipewa tahadhari kuhusu tatizo la sukari hiyo alipoingiza kwa mara ya kwanza lakini aliendelea kuiingiza.
Alisema baada ya sukari hiyo kufanyiwa uchunguzi ilionekana haina kiwango na kuchukuwa hatua za kisheria ili isiweze kufika kwa wananchi kwa matumizi mbali mbali.
Alisema baada ya kugundulika kasoro hiyo, mmilikiwa huyo Rashid Ali  alishauriwa kuirejesha ilikonunua ama kuiingamiza lakini mashauri yote mawili aliyakataa.
Katika siku ya kwanza ya zoezi la kuangamiza sukari hiyo katika mashimo ya mchanga ya Zingwezingwe makontena matatu kati ya 20 yaliharibiwa chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya ulinzi na usalama
Kwa Upande wake Mrakibu Muandamizi wa Jeshi la Polisi Khamis Ramadhan alisema zoezi la kusafirisha sukari hiyo kutoka Bandari ya Malindi na kufika katika sehemu ya kuangamizwa limeenda vizuri na hakuna tatizo lolote lililojitokeza hadi lilipomalizika kwa siku ya kwanza.
Alisema zoezi hilo lililoongozwa na maafisa wa Bodi ya Chakula na Dawa Zanzibar limeshirikisha Vikosi vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wa kitengo cha Mazingira Zanzibar.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.