Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Skuli ya Msingi na Maandalizi Fuoni Pangawe Wilaya ya Magharibi "B"Unguja, kulia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma na Mwakilishi wa Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Zanzibar Bi. Shen Qi,
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amewataka walimu kote nchini kuwa wabunifu na kujiendeleza
kitaaluma ili waweze kukidhi mahitaji ya kielimu na kwenda sambamba na wakati.
Dk. Shein amesema hayo katika ufunguzi wa
Skuli ya msingi ya Fuoni /Pangawe,
iliyopo Wilaya ya Magharibi B Unguja.
Ujenzi wa skuli hiyo uliogharimu zaidi ya silingi Bilioni tano
ni wa tatu kufanyika, ikiwa ni muendelezo wa misaada ya Serikali ya Jamuhuri ya
Watu wa China kwa Zanzibar, ikitanguliwa na
ujenzi wa skuli za Kijichi na Urafiki iliyoko Mwanakwerekwe.
Dk. Shein amesema elimu ni fani inayokuwa na kuendelea siku
hadi siku, hivyo ni vyema kwa walimu kwenda sambamba na mabadiliko hayo ili
kukidhi haja ya zama hizi, akibainisha umuhimu wa kuwa na mbinu mpya za ufundishaji.
Alizitaka mamlaka zinazosimamia uendeshaji wa skuli hiyo
kushirikiana na kuweka walimu wenye uwezo wa kitaaluma, wanaopenda kujituma na
wenye kuweka mbele uzalendo ili ufanisi unaotarajiwa uweze kupatikana.
“Ni busara tukaiwacha ile tabia ya kuwafundisha watoto wetu
yale tuliosoma sisi miaka iliyopita, tuelewe kuwa elimu si sawa na maji ya
vidimbwi yanayotuama, bali ni fani inayokuwa na kuendelea siku hadi siku”,
alisema.
Alisema ufunguzi wa skuli hiyo ni uthibitisho wa dhamira njema
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu inayochochea
maendeleo, ikiwemo ya elimu.
Aidha alisema ujenzi
huo umetokana na mipango ya serikali, iliozingatia ripoti ya sensa ya watu na
mkaazi ya mwaka 2012 pamoja an ripoti ya Utafiti ya watoto walio nje ya skuli.
Dk. Shein alibainisha kuwa ripoti hizo zimeonyesha ongezeko
kubwa la idadi ya watu, jambo lililopasa kwenda sambamba na mahitaji ya
kijamii, zikiwemo skuli na kusema kuwa Wilaya hiyo ina jumla ya watoto 36,666
wenye umri wa kati ya miaka sita na 11, ambao ni wajibu kwao kupata elimu ya
msingi.
“Ripoti hizo zimebainisha kuwepo msongamano mkubwa wa wanafunzi unaofikia wastani wa
wanafunzi 90 kwa darasa moja katika skuli za Wilaya hiyo, ikibainishwa ndio
zinazoongoza katika changamoto ya aina hiyo”, alisema.
Rais Dk. Shein alisema uwepo wa skuli hiyo utasaidia sana
upatikanaji wa nafasi za masomo kwa watoto wa maeneo hayo na hivyo kupunguza
msongamano katika skuli za Kinuni, kijitoupelea, Chunga na Fuoni ambazo hivi
sasa zina wanafunzi 17,054 ikiwa wastani wa wanafunzi 131 kwa darasa moja.
Alisema ujenzi wa skuli Fuoni /Pangawe utasogeza karibu sana
mahitaji ya kielimu watoto wanaoishi maeneo hayo, akibainisha muendelezo wa
juhudi za Serikali katika kupanua wigo wa miundombinu ya elimu Wilayani humo.
“Juhudi za serikali katika sekta ya elimu haziishi hapa, kuna
ujenzi unaotarajiwa kukamilika ndani ya mwaka hu, utazihusisha skuli mpya za
msingi Kwarara na ile ya Ghorofa ya Fuoni na Kinuni”alibainisha.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa skuli hizo za sekondari
kutaongeza idadi ya skuli za msingi na Sekondari Wilayani humo, kutoka skuli za
Sekondari 15 mwaka 2018 hadi kufikia 17,
wakati skuli za Msingi nazo zikiongezeka kutoka 24 mwaka uliopita hadi kufikia
26.
Aliwataka wananchi kote nchini kudumisha amani pamoja na
kuchangamkia fursa za kuendeleza elimu kwa kuwaandikisha watoto wote waliofikia
umri wa kuanza masomo sambamba na kuwashajiisha kushughulikia masomo yao kwa
maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
Alisema mafanikio ya kielimu yaliofikiwa nchini yanatokana na
juhudi na misingi bora uliyowekwa na mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati
Abeid Amani Karume, alielenga kuhakikisha vijana wote wanapata elimu bila
ubaguzi.
Alisema katika kipindi cha miaka 55 sasa, Zanzibar
imeshuhudiwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kijamii, ikiwemo uimarishaji wa
sekta ya elimu
Dk. Shein aliipongeza Serikali ya watu wa China pamoja na Kampuni ya China Qindao Construction (CNQC)
kwa kusaidia ujen zi wa jingo hilo zuri
la kisasa na lenye viwango vinavyokubalika.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliagiza uongozi wa Wizara
kwa kushirikiana na Kamati ya Skuli kuhakikisha skuli hiyo pamoja na samani
zilizomo zinatunzwa vyema ili ziwe endelevu, na kubainisha haja ya wanafunzi
kufunzwa uzalendo wa kuthamini mali za Taifa.
Aidha, alizitaka mamlaka hizo kuhakikisha michoro na mifumo
yote ya umeme na maji taka iko vizuri, ili pale wakandarasi watakapoondoka
kusiwepo na hitilafu zitakazojitokeza.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pemba Juma,
alisema ujenzi wa skuli hiyo ni moja lati ya skuli tatu zilizotanguliwa
kujengwa, ukiwa umevuka malengo ya Ilani ya CCM 2015 – 2020.
Alisema kupitia Ugatuzi Wizara hiyo itashirikiana an Wizara ya
Nchi, (OR), Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ katika
usimamizi wa suala zima la ufundishaji.
Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk.
Idrisa Muslih Hijja alisema ujenzi wa skuli hiyo uliogharimu zaiidi ya shilingi
Bilioni tano umetokana an msaada wa Serikali ya China, huku Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na mambo mengine imechangia msamaha wa ushuru wa
vifaa vya ujenzi, umeme pamoja na maji.
Alisema hatua ya ujenzi huo ni kuunga mkono juhudi za serikali
katika uimarishaji wa sekta ya elimu nchini, hivyo akawataka wazazi, walimu na
jamii inayozunguka kuitunza skuli hiyo ili iweze kuwa endelevu.
Aidha, Mwakilishi wa Ubalozi mdogo wa China nchini, Bi.Shen Qi
aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa iliotowa
hadi kufanikisha ujenzi huo.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa skuli hiyo kutasaidia
kuwaweka wanafunzi katika mazingira bora
zaidi ya kupata elimu na hivyo kuinua viwango vyao.
Bi.Qi alielezea dhamira ya Serikali ya Watu wa China kuendelea
kushirikiana na Zanzibar, ili kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii na
kubainisha ushirikiano wa Kihistoria uliopo kati ya mataifa hayo.
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment