Habari za Punde

CRDB Yafutarisha Wananchi wa Zanzibar Hoteli ya Verdev Mtoni Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB} Bwana Abdulmajid Muusa Msekela Kushoto akimuongoza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyepo Kati kati katika Futari ya pamoja waliyoandaa kwa ajili ya Wateja wao.Wa kwanza kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Baadhi ya Mawaziri na Viongozi wa Serikali, Wateja na Wananchi wakipata futari ya pamoja iliyoandaliwa na Uongozi wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB} hapo Hoteli ya Verde Mtoni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB} Bwana Abdulmajid Muusa Msekela katika futari ya pamoja iliyoandaliwa na Benki hiyo. 
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB} Bwana Abdulmajid Muusa Msekela akitoa Taarifa za Benki yake kwa Wananchi, Viongozi na Wateja mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Benki yake hapo Verde Mtoni.
 Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohamed Mahmoud akiwasilisha  salamu za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Benki yake hapo Verde Mtoni.

Baadhi ya Wateja wa Benki ya Maendeleo Vijijini CRDB pamoja na Viongozi na Wananchi mbali mbali wakipata futari ya pamoja iliyoandaliwa na Benki hiyo.
Balozi Seif  aliyekaa kati kati kwenye viti akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB} pamoja na wana Hisa wa Benki hiyo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ongezeko la huduma za Kibenki liliopo Nchini mbali ya kuongeza Mapato kwa Taifa lakini pia zitajenga mazingira mazuri kwa Wawekezaji walioonyesha nia ya kutaka kuwekeza Miradi yao Nchini.
Alisema kasi kubwa iliyopo hivi sasa katika sekta ya Uwekezaji hasa Makampuni yenye miradi mikubwa ya Kimataifa inahitaji kupata huduma sahihi za Kibenki zitakazosaidia njia ya haraka ya kufanikisha vyema Miradi yao.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo katika salamu zilizotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB}iliyofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Futari hiyo imejumuisha Wateja mbali mbali wa Benki ya CRDB, Viongozi wa Serikali, Kisiasa pamoja na baadhi ya Wananchi wenye nia ya kutaka kupata huduma kutoka Beki hiyo.
Alisema Utamaduni wa Mabenki wa kuwakusanya Wateja na Wananchi kwenye mikusanyiko tofauti ikiwemo Futari ya pamoja ni azma njema inayotoa ushawishi wa kujenga mapenzi kati ya pande hizo mbili zinazohitajiana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi na Wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB}hasa ule wa Tawi la Zanzibar kwa uamuzi wake wa kusikiliza ushauri na maoni ya wanaowahudumia kama ujumbe wao unavyoelezea wa Benki Inayosikiliza.
Akigusia suala la Biashara hasa kipindi hichi cha mpito cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Balozi Seif  aliwakumbusha Wafanyabiashara Nchini waendelee kufuata maamuzi ya Serikali Kuu ya kutaka wawahudumie Wananchi bila ya kuwakomoa.
Alisema inapendeza kuona wapo baadhi ya Wafanyabiashara waliozingatia ushauri huo na vyema Wafanyabiashara wengine wakaiga mfano huo kwa kuonyesha huruma kwa Wananchi wenzao hasa kipindi hichi ili wapate  baraka katika Biashara zao.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Vijijini {CRDB} Bwana Abdulmajid Mussa Msekela alisema Benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kujumuika pamoja na Wananchi katika masuala mbali mbali ya huduma za Kijamii.
Bwana Abdulmajid alisema kama ilivyo Falsafa ya Benki hiyo ya kumsikiliza Mteja Uongozi wake hupenda kusikilia ushauri na malalamiko ya Wateja na baadae kuyafanyia kazi kama ilivyofanya kwa Tawi lao kulilohamishwa kutoka Mkunazini na kupelekwa Mtaa wa Kisiwandui.
Alisema kwa vile Zanzibar ni moja ya sehemu muhimu na pana katika masuala ya huduma za Kibenki CRDB imeamua kuongeza Tawi jengine katika Mtaa wa Mwanakwerekwe ili kuwasogezea kwa karibu zaidi huduma hizo Wananchi wanaohitaji huduma za Kibenki.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa CRDB alifafanua kwamba wakati wakijipanga kuongeza huduma katika Visiwa vya Unguja na Pemba kwa sasa wako mbioni kutoa huduma za Benki ya Kiislamu sambamba na ifikapo Mwezi Juni Mwaka huu wanatarajia  kulipa Hisa kwa Wateja wao.
Bwana Abdulmajid Mussa Msekela ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano inayotoa kwa watendaji wa Benki yake ambayo huwawezesha kuendesha huduma za Kibenki katika kuwahudumia Wananchi Visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.