Habari za Punde

Kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar yagawa chakula kwa waathirika wa mvua za masika

 Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bi. Marina Joel Thomas akizungumza na wahanga wa Mvua za masika katika zoezi la kugawa msaada wa chakula wananchi wa shehiya 12 za Wilaya ya Mjini hafla hiyo imefanyika Skuli ya Msingi Jang’ombe Mjini Unguja.
 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mihayo Juma N’hunga, akitoa pole kwa wananchi walioathirika na mvua za masiki na kuwataka alipofika katika zoezi la kutoa chakula kwa wahanga hao.
  Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye foleni zao wakisubiri kupatiwa msaada wa chakula kilichotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
 Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame akimpa msaada wa chakula Delila Enock ambae ni miongoni mwa wahanga wa mvua za masika.
Baadhi ya wananchi wakielekea majumbani kwao na msaada wa chakula na mafuta walivyopewa.
Picha na Makame Mshenga.

Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, leo Mei 19, 2019 imeanza zoezi la kugawa msaada wa chakula kwa wananchi mbalimbali ambao nyumba zao ziliathirika kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha nchini kote.

Kwa kuanzia, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, imeanza kugawa chakula hicho kwa wakaazi wa shehia 12 za Wilaya ya Mjini waliohakikiwa na kupewa vitambulisho maalumu.

Mkurugenzi wa Kamisheni hiyo Makame Khatib Makame, akizungumza wakati wa zoezi hilo, alisema jumla ya nyumba 2,911 zimeathirika Unguja na Pemba kutokana na mvua hizo. 

Alieleza kuwa, baadhi ya nyumba hizo tayari zimekauka na wenyewe wameanza kurejea baada ya awali kulazimika kuzihama na kuhifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao.

Hata hivyo, alisema baadhi ya nyumba zilizokumbwa na kadhia hiyo bado hazikaliki.

Mapema, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mihayo Juma N’hunga, alisema serikali imeamua kuwafariji wananchi hao kwa kuwa inafahamu machungu wanayopata na kipindi kigumu wanachopitia hasa katika wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Aliwaomba wananchi wa maeneo mengine wawe na subira, kwani zoezi hilo litaendelea nchi nzima katika wilaya zote za Unguja na Pemba ili kuhakikisha kila aliyeathirika anafikiwa.

Zoezi hilo lilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bi. Marina Joel Thomas na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya  Makamu wa Pili wa Rais, Abdalla Hassan Mitawi.

Naidha mkurugenzi huyo aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwani bado mvua za masika zinaendelea kunyesha hadi mwezi wa Juni ambapo ndio zinatarajiwa kuisha. 

Kwa upande wao wahanga hao, waliipongeza serikali kutokana na msaada huo wa chakula ambapo kitaweza kuwasaidia hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi wa ramadhani. 


Vitu vilivyotolewa ili kuwasaidia wananchi hao ni mchele, unga wa ngano, sukari na mafuta ya kupikia ambapo zaidi ya shilingi milioni 200 zimetumika kwa ajili ya kuwafariji wahanga wa mvua hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.