Habari za Punde

MPINA ATOBOA SIRI YA ONGEZO LA GHAFLA LA VIWANDA VYA NYAMA


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina  (mwenye kizibao chekundu) akitoa maelekezo kwa  mmiliki wa kiwanda cha nyama cha Eliya Foods Overseas LTD kilichopo Longido  ndugu Shabbir Virjee(mwenye shati jeupe), kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (Mwenye nguo nyeusi) akishuka kwenye gari maalum ya kubebea maziwa baada ya kulikagua gari hilo la kiwanda cha maziwa cha Kilimanjaro Fresh alipotembelea kiwanda hicho kuangalia utendaji wake hivi karibuni.

Na John Mapepele

Serikali imewahakikishia wawekezaji wa viwanda vya mazao ya mifugo nchini kuwa hakuna atakayechezea masoko yao kwa kuingiiza bidhaa hizo sokoni kwa njia isiyo halali na badala yake serikali imetaka jitihada zinazofanywa na wawekezaji lazima zilenge kuwainua wafugaji kote nchini na kutoa majawabu ya changamoto zinazowakabili wafugaji ikiwa ni pamoja na ajira, masoko na nyama bora ili uwekezaji huo uwe wenye tija na endelevu.

Hayo amesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina alipofanya ziara ya kikazi mkoani Arusha leo kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya mifugo ambapo amesema Serikali ya awamu ya tano imejipanga kikamilifu  kuhakikisha  kuwa  hakuna mtu atakayekwepa kufuata taratibu za  biashara ya mazao ya mifugo kutoka ndani na nje ya nchi ili kuwa na ushindani wa halali.

Amesema  kutokana na udhibiti uliofanywa na serikali wa kuzuia ukwepaji wa kodi, uingizaji wa mazao ya mifugo na kwa udanganyifu na utoroshaji mkubwa mifugo kwenda nje ya nchi kwa njia za panya umesaidia kuwavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vikubwa vya nyama na maziwa  kwa wingi kuliko kipindi chochote kuanzia nchi yetu ilivyopata uhuru hadi sasa.

“Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukitorosha  mifugo kwenda kuuza nchi za jirani kwa kuwa hapa kwetu  palikuwa hakuna soko la uhakika la kuuzia lakini sasa tunaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutusaidia kupata kiwanda hiki hapa Longido ambacho kitakuwa mkombozi wa soko la uhakika la mifugo yetu” alisisitiza  Mzee maarufu wa kimasai, Olesiyanda Sidala wakati Waziri Mpina alipomaliza kukagua kiwanda cha kusindika  nyama cha Eliya Foods Overseas LTD kilichopo eneo la Longido mkoani Arusha.

Mkurugezi Mtendaji wa Kiwanda hicho Shabbir Virjee alisema Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 hadi 1000 na  mbuzi na kondoo 2000 hadi 5000 kwa siku na kinatarajia kutoa zaidi ya ajira 300,ambapo pia aliiomba serikali eneo la ekari  100 kwa ajili ya kupumzishia mifugo kabla ya kuchinjwa na kuahidi kuwa ifikapo Oktoba mwaka huu kiwanda kitakuwa kimekamilika na kuanza kufanya kazi.

Aidha Waziri Mpina aliongeza kwamba hivi sasa wananchi na wawekezaji wengi wanajitokeza kuwekeza kwenye sekta ya mifugo baada ya muda mrefu kukimbia uwekezaji kwa sababu walikuwa wanafika mahala  wanachinja na kukosa masoko ya kuuza nyama hizo.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wote kwa sheria na kwamba  Wizara itaendelea na operesheni muda wote kila mahali kuanzia  bandarini,mipakani, viwandani, kwenye  maduka na katika  vya ndege  kukagua na kuona kama kuna mtu ameingiza  bidhaa kwa kufuata sheria na ubora wake.

Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi hivyo inaweza kutoa malighafi ya kutosha kwa viwanda  vya mifugo vinavyoanzishwa na kwamba asilimia 1.4 ya mifugo yote duniani ipo Tanzania na asilimia 11 kwa Afrika, ambapo ina jumla ya Ngombe milioni 30.5, Mbuzi milioni 18.8 na Kondoo milioni 5.3.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe  amepongeza jitihada zinazofanywa na Wizara ya mifugo ambapo amesema  Wizara  imeonyesha kuwa siyo ya kupokea misaada kama ilivyokuwa inatazamwa awali bali inayoweza hata kusaidia wizara nyingine zisizozalisha na kuifanya nchi yetu isonge mbele.

“Mheshimiwa Waziri naomba kusema wazi kuwa umekuwa bega kwa bega kudhibiti utoroshaji na ukwepaji wa kodi na umeonyesha uwezo mkubwa wa kuitendea haki sera ya viwanda kwa kuweka mazingira mazuri ya kuvutia viwanda vingi kujengwa  naamini wizara nyingine zige mfano kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi “ aliongeza Mwaisumbi.

Mpina aliongeza kuwa Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha kosaafu za mifugo ili kupata mifugo bora itakayoweza kushindana na mifugo mingine katika masoko ya kimataifa ambapo alisema  tayari madume bora ya ngombe yanayozalisha  mbegu bora yameletwa na serikali kwenye Kituo cha Uhimilishaji cha Taifa  Usariver jijini Arusha ambayo yanauwezo wa kutosha kwa nchi nzima.

Katika kuhamasisha wafugaji wanawapeleka watoto wao kwenye mafunzo maalum ya ufugaji, Waziri Mpina alitoa nafasi kwa mtoto mmoja wa mfugaji anayeongoza kwa mifugo mingi kuweza kusomeshwa  bure na serikali kwenye Wakala wa Mafunzo ya Mifugo Tengeru na Kituo cha Uhimilishaji cha Taifa  Usariver jijini Arusha.

Katika ziara hiyo Waziri Mpina alitembelea  bwawa lililobomoka la Kimokowa  na kuelekeza kuwa Wizara na Halmashauri ya Longido  kukarabati bwawa hilo mara moja pia alimwelekeza katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo kukarabati majosho 8 kati ya 16 ya Wilaya ya Londigo kabla ya Julai mwaka huu, ambapo pia alisema tayari Wizara imeshatoa kiasi cha Shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukarabati soko la kimataifa la mnada wa mpaka wa Longido.

Kaimu Msajiri wa Bodi ya Nyama nchini Imani Sichalwe alimhakikishia Waziri Mpina kuwa Bodi ya nyama itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika kuwatafutia masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine  Waziri Mpina alitembelea kiwanda cha maziwa  cha Kilimanjaro Fresh chenye uwezo wa kuzalisha  lita 5000 hadi 50000 kwa siku ambapo kwa sasa kimeanza kuzalisha lita 5000 baada ya kuanza rasmi uzalishaji Februari 2, mwaka  huu,ambapo aliwahakikishi kuwapa ushirikiano na aliwataka  wamiliki kuangalia bei wanaonunua maziwa kwa wafugaji zisiwe kandamizi.

Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Irfhan Virjee amesema kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikiuza jumla ya lita 4000 kwa siku na kwamba kiwanda kinatarajia kuongeza uzalishaji wa mazao mengine ya maziwa ikiwa ni pamoja na jibini na siagi ndani ya miezi miwili ijayo, ambapo kwa sasa kinaendelea kutoa maziwa yenye radha tofauti za matunda.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Mifugo, Daktari  Asimwe Lovince alimshukuru Waziri Mpina na kumhakikishia kuwa amepokea maelekezo yote na kwamba atayafanyia kazi kikamilifu katika kipindi kifupi ili sekta ya mifugo iweze kukua kwa kasi  na kuleta mapinduzi yanayohitajika kwa sasa. 

Aidha alisema kufanya kazi kwa viwanda vya nyama na maziwa nchini kutasaidia kuliingizia taifa fedha za kigeni ambapo kwa upande wa viwanda vya nyama  vitasaidia kutoa mazao mengi zaidi kwenye damu(vyakula vya mifugo),pembe na ngozi.

Katika kipindi cha  miaka miwili sasa wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa  na mikakati mbalimbali ya kuleta  mageuzi ya sekta kuanzia mapato, kutafuta ufumbuzi wa migogoro baina ya wafugaji wa watumiaji wengine wa ardhi, kudhibiti magonjwa, kuboresha kosaafu za mifugo kwa njia mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.