Habari za Punde

Wakulima wa Karafuu Mkoa wa Kusini Unguja Kutathimini Juhudi Zinazochuliwa na Wizara ya Kilimo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Hassan Khatib amewashauri Maafisa wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) kuwa karibu na wakulima wa Karafuu ili kuwasaidia na kuliimarisha zaidi zao hilo.
Amesema utaratibu wa sasa wa kuendelea kujifungia ofisini kusubiri msimu wa kununua karafuu kutoka kwa wakulima uanze bila ya kuchukua juhudi ya kuwasaidia katika kulikuza zao hilo sio jambo zuri.
Mkuu wa Mkoa alitoa ushauri huo katika mkutano wa wakulima wa zao la Karafuu wa Mkoa wa Kusini ulioandaliwa na ZSTC kwa lengo la kuangalia maendeleo ya zao hilo kwa mwaka 2018/2019 katika Ukumbi wa Kituo cha Walimu Dunga.
Alisema uwamuzi wa Shirika hilo kukutana na wakulima mwaka mara moja, baada ya kumalizika msimu wa kuchuma karafuu, haumsaidii sana mkulima katika kuimarisha na kuliendeleza zao hilo.
Aliwataka wakulima wa karafuu kwa upande wao kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Wizara ya Kilimo za kupewa miche ya mikarafuu bila malipo kwa kuitunza na kuhakikisha wanafutilia ukuaji wake ili lengo la kupewa miche hiyo liweze kufikiwa.
Aidha aliwashauri wananchi wa Mkoa Kusini kuangalia kilimo chengine cha biashara hasa  pilipili hoho huku wakijua kwamba eneo kubwa la Mkoa huo lina mawe na zao hilo linastawi sana katika maeneo hayo.
Akitoa tathmini ya zao la karafuu kwa mwaka 2018/2019, Mkurugenzi wa Masoko wa ZSTC Salum Abdalla alisema msimu huo mavuno hayakuwa makubwa lakini aliwataka wakulima wasivunjike moyo na matokeo hayo bali waendelee kuitunza mikarafuu na kufanya juhudi ya kupanda mipya.
Aliwaeleza wakulima wa zao hilo wa Mkoa Kusini Unguja kuwa ZSTC Iliweka makisio ya kununua karafuu tani 3,000 lakini waliweza kununua tani 195.16  ambapo Pemba zilinunuliwa tani 161 na Unguja tani 34.
Alitoa wito kwa wakulima wa karafuu wanaochukua mikopo kwa ajili ya maandalizi ya kuchuma karafuu wakati wa kuanza msimu kila mwaka kurejesha mikopo hiyo ili kujenga imani kwa Shirika na waweze kukopeshwa katika msimu uanaofuata.
Kwa upande wao wakulima wa karafuu wa Mkoa Kusini Unguja wamelishauri Shirika la ZSTC kusimamia ugawaji wa miche ya mikarafuu kwa wakulima na kwa wakati bila ya kufanya upendeleo ili kila anayestahiki kupata aweze kuipata.
Katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa alitoa kadi za usajili kwa wakulima  wapya wa karafuu wa Mkoa huo na kuwataka wakulima ambao bado hawajapata usajili kufanya utaratibu wa kupata ili maslahi yanayopatikana kwa wakulima waliopata usajili waweze kuyapata.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.