Na.
Mwandishi Wetu.
Serikali imesema mabadiliko kwenye sekta ya sheria
nchini hususani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu yameanza kuleta tija baada ya kuongeza
ufanisi na kuokoa fedha ambazo hapo awali zilikuwa zikitumika kuwalipa mawakili
binafsi.
Akijibu swali la Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), Saed
Kuebenea ambae alitaka kujua kiasi cha fedha ambacho serikali imeokoa tangu maboresho
kwenye sekta hiyo yaanze kutekelezwa, ambapo pamoja na mambo mengine yalianzisha
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia, kuendesha
na kuratibu mashauri yote ya madai kwa niaba ya Serikali nchini.
Kwenye majibu yake Waziri wa Katiba na Sheria,
Dkt. Augustine Mahiga alimueleza mbunge hyo kuwa kwenye Mwaka wa Fedha 2018/19
pekee Serikali imeweza kuokoa zadi ya shilingi bilioni tisa (9,018,957,011),
ambazo kama sio maboresho kwenye sekta hiyo zingetumika kulipa makampuni
binafsi ya uwakili.
Aidha, Dkt. Mahiga aliendelea kulieleza Bunge kuwa
Serikali itaendelea kutumia Mawakili binafsi kwa kibali cha Mwanasheria Mkuu wa
Serikali pale itakapothibitika kuwa ni lazima kufanya hivyo. Alitoa mfano wa
vigezo vinavyotumika kutumia mawakili binafsi ni shauri kufunguliwa kwenye
mahakama ambazo sio za kimataifa na sheria za nchi husika haziruhusu uwakilishi
wa mwanasheria kutoka nje ya nchi hiyo.
Kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa Dkt.
Mahiga ameliambia bunge kuwa uendeshaji wa mashauri hayo utendelea
kuishirikisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye kila hatua ya mwenendo
wake tofauti na hapo awali.
Kuhusu baadhi ya mashirika ya umma kuendelea
kutumia mawakili binafsi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus
Kilangi amelieleza Bunge kuwa mashirika hayo ni yale ambayo mashauri yake
yalianza kabla ya maboresho kwenye sekta hiyo hayajaanza kutekelezwa na
uendeshaji wa mashauri utatekelezwa kwa kushirikiana na Wakili Mkuu wa
Serikali.
No comments:
Post a Comment