Habari za Punde

TANTRADE KUENDELEA KUJENGA MAZINGIRA WEZESHI KWA WAFANYABIASHARA NA WAJASIRIAMALI WADOGO NCHINI.


Na Mwandishi Wetu, MAELEZO DAR ES SALAAM 11. JULAI, 2019
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imesema itaendelea kuimarisha mitandao ya wadau na makampuni mbalimbali wafanyabiashara ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchini wanapatiwa fursa za masoko ili kuweza kukuza sekta ya biashara nchini.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi (Julai 11, 2019) na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Zanzibar, Latifa Khamis wakati wa mkutano wa ana kwa ana baina ya wafanyabiashara, wazalishaji na wanunuzi wa bidhaa za ngozi na shule katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.
Latifa alisema kuwa Serikali kupitia TANTRADE itaendelea kutumia majukwaa na fursa mbalimbali za kibiashara kwa ajili ya kuwawezesha wajasirimali na wafanyabiashara kuweza kutumia fursa zilizopo ikiwemo kupata masoko ya uhakika ya biashara zao kupitia kwa wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya nchi.
“TANTRADE imeandaa mkutano huu maalum kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo kuweza kupata fursa za masoko ya kuuzia masoko yao ambapo utaratibu huu utakuwa endelevu, hivyo kampuni ya  DHL kupitia Market Plaze Africa wametoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa hapa nchini kutangaza biashara zao” alisema Latifa.
Aidha Latifa alisema mara baada ya kuisha kwa maonyesho ya 43 ya DITF, TANTRADE imeandaa mkakati maalum wa kuwaunganisha wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara kupitia maonesho ya bidhaa za wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchi nzima ambapo wataanzia katika Mkoa wa Ruvuma na baadae Zanzibar.
Aidha Latifa alisema katika mkutano huo pia TANTRADE imewakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki ya NMB ambayo imekuwa na utaratibu wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali kuanzia kiwango cha Tsh 500,000 hadi Milioni 50,000,0000.
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Kampuni ya DHL Tanzania, Paul Makolosi aliwataka wajasirimali na wafanyabiashara wadogo kutangaza bidhaa zao katika taasisi hiyo kwa kuwa masoko ya bidhaa zao yapo kwani nchi nyingi za mabara ya Ulaya na Amerika yamekuwa wakivutiwa na bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo ina uzoefu wa miaka 30 ya kufanya biashara duniani, ambapo katika utendaji kazi wake imekuwa ikiwasaidia zaidi wajasiriamali wadogo waliopo katika Bara la Afrika, hivyo ujio wa taasisi hiyo hapa nchini ni fursa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara hao.
“Katika Nchi za Bara la Ulaya na Amerika, bidhaa za ngozi hususani viatu vimekuwa na soko kubwa sana, na kwa kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wa hapa Tanzania wamekuwa wakizalisha bidhaa hiyo, sisi DHL kupitia Market Place Africa tupo tayari kuwasaidia ili kupata masoko ya uhakika” alisema Makolosi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.