RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John
Pombe Magufuli leo amekabidhiwa rasmi Uwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) baada ya aliekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Dk. Hage Geingob
Rais wa Namibia kumaliza muda wake.
Tukio hilo limefanyika
leo katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi hizo za (SADC) uliofanyika katika
ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar-es-Salaam
ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka nchi za (SADC) wakiwemo Marais 11
kutoka nchi hizo pamoja na viongozi wote wakuu wa Tanzania akiwemo Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Mara baada ya
kukabidhiwa wadhifa huo, Rais John Pombe Magufuli akisoma hotuba yake alitoa
shukurani kwa viongozi wote wakuu wa Jumuiya huo kwa kuonesha mashirikiano nae katika
kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa rais wao.
Rais Magufuli alisema
kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari na itaendelea kushirikiana na
nchi zote za (SADC) huku akiwahakikishia viongozi hao kuwa katika uongozi wake
atahakikisha Tanzania haitoyumba.
Alieleza kuwa
atahakikisha anafuata nyayo za waasisi wote wa nchi za (SADC) akiwemo Hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kueleza kuutumia uzoefu wa
mwenyekiti aliyepita Dk. Hage Geingob, Rais wa Namibia.
Rais Magufuli
alimpongeza Mwenyekiti huyo mstaafu kwa juhudi kubwa alizozichukua katika
kupigania ajira kwa vijana huku akimpongeza kwa kuhakikisha nchi sita za (SADC)
zimefanya uchaguzi kwa salama na Amani huku akiwa pole wananchi wa nchi
zilizokuwemo katika Jumuiya hiyo ambazo zilipata maafa kutokana na kimbunga.
Aidha, Rais Magufuli
alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Antoine Tshisekedi
kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu mkubwa hali ambayo imeonesha wazi
kukuwa kwa demokrasia.
Alitumia fursa hiyo
kuushukuru uongozi wa (SADC) akiwemo Katibu Mtendaji wa (SADC) Dk. Stergomena
Lawrence Tax pamoja na Sektarieti ya Umoja huo kwa kazi kubwa ulioifanya na
kusisitiza kuwa akina mama wakipewa uongozi wanaweza.
Alieleza kuwa hatua hiyo
imeweza kuonekana na Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania na ndio maana mwaka 2015
ikamchagua Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Makamo wa Rais wake na tokea kupewa
wadhifa huo amekua akitekeleza kazi zake vizuri.
Rais Magufuli alieleza
kuwa tangu kuanzishwa kwa Umoja huo mafanikio makubwa yameweza kupatikana ikiwa
ni pamoja na kupambana na ukoloni sambamba na kupambana na ubaguzi wa rangi.
Alisisitiza kuwa tangu
kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mnamo mwaka 2008 biashara imekuwa kutoka asilimia
16 mwaka huo hadi kufikia asilimia 22
mwaka 2017 hiyo ni kutokana na kuwepo wka utamaduni wa kidemokrasia.
Sambamba na hayo. Rais
Magufuli alieleza kuwa licha ya mafanikio yalipptikana katika Jumuiya hiyo pia,
kuna baadhi ya changamoto zikiwemo amani na usalama katika baadhi ya nchi, njaa
na ukame.
Katika hilo, Rais
Magufuli alieleza kuwa katika nchi hizo za (SADC) kuna haja ya kufanya kazi kwa
pamoja sanjari na kuendeleza amani na usalama kwani vitu hivyo pia huimarisha
uchumi.
Alieleza kuwa katika
kuhakikisha nchi za Jumuiya hiyo zinapata mafanikio ni vyema zikahakikisha
hazina migogoro huku akimnukuu Rais mstaafu wa Zimbwabe Robert Mugabe pale
aliposema “kamwe tusije tukakata tamaa katika eneo lolote la Afrika”.
Pamoja na hayo, Rais
Magufuli alieleza jinsi uchumi wa nchi za (SADC) zilivyodorora katika
kuimarisha uchumi wake hadi kuweza kupelekea baadhi ya nchi za Jumuiya hiyo
zikawa na upungufu wa chakula.
Alieleza kuwa kutokana
na kutokuwepo kwa mawasiliano katika nchi za Jumuiya hiyo kumechangia kuagizia
bidhaa nje ya nchi wakati bidhaa hizo zimejaa katika nchi za (SADC) hali ambayo
pia, inazidisha kuongezeka kwa gharama za uagiziaji.
"Rais Dk. Shein alieleza
haja ya kujiendeleza katika viwanda na kusisitiza kuwa sio jambo la busara
kuuza malighafi na badala yake ni vyema zikauzwa bidhaa zinazotokana na mali
ghafi hizo kwani zinapouzwa malighafi soko la ajira linaondoshwa".
Aliongeza kuwa katika
uongozi wake atahakikisha suala la viwanda linapewa kipaumbele katika uongozi
wake na kusisitiza kuwa nchi za (SADC) sio masikini ni tajiri sana kwani zina
rasilimali za aina zote.
“Ni lazima tuhakikishe
kuwa nchi zetu zinanufaika na rasilimali zilizopo ndani ya nchi zetu waasisi
wetu walionesha umoja ni nguvu na tunaweza kufika pazuri na kuleta ushindi
mkubwa katika kujenga nchi zetu” alisisitiza Magufuli.
Sambamba na hayo, Katika
hotuba yake Rais Magufuli aliwaeleza viongozi wa Umoja huo kuwa vikwazo
vilivyowekwa kwa nchi ya Zimbabwe si vyao peke yao bali ni vya nchi zote za
(SADC) hivyo, kwa mashirikiano ya pamoja ya nchi hizo kuna haja ya kupambana
katika kuviondoa.
Pia, alieleza kuwa ajira
zenye staha zitapatikana kama nchi hizo zitafanya kazi kwa pamoja sambamba na
kuimarisha amani na utulivu kwani hatua hiyo pia, itaondosha changamoto zote
ziliozopo.
Nae Mwenyekiti wa (SADC)
aliemaliza muda wake Rais Hage Geingob
alimkabidhi Uwenyekiti huo Rais Magufuli na kumuelezea kuwa anaimani na
kiongozi huyo kuwa wadhifa huo utautendea haki kutokana na ujasiri na mchapa
kazi katika utendaji wake wa kazi.
Rais Hage Geingob
alitumia fursa hiyo kuitangaza lugha ya Kiswahili kuwa ni lugha rasmi katika
Jumuiya hiyo ya (SADC).
Alitumia fursa hiyo
kupongeza Amani na utulivu inavyoendelea kuoneshwa katika nchi za (SADC) na
kuonesha kukua kwa demokrasia katika ukanda huo huku akisisitiza kuwa amani na
utulivu ni msingi wa maendeleo.
Mapema baadhi ya
viongozi wa (SADC) walitoa hotuba zao kwa ufupi na kueleza jinsi mashirikiano
mazuri yaliopo katika Umoja huo wakiwemo Rais Azali Assoumani wa Comoro, Rais
wa Madagascar Andry Nirina Rajoelina, Rais wa Congo Felix Tshisekedi na
viongozi wengine.
Pia, katika mkutano huo
zilitolewa tunzo na vyeti kwa washindi wa insha pamoja Makala na vipindi vya
redio na televisheni kwa waandishi wa habari wa nchi za (SADC).
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment