Habari za Punde

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Kuhudumia Abiria Mil.8 Kwa Mwaka

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa  mara baada ya uzinduzi rasmi wa jengo la abiria (Terminal  3) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, akipata maelezo katika moja ya sehemu za kushushia mizigo katika jengo la abiria (Terminal 3) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam baada ya kulizindua rasmi leo 10 Agosti 2019. Kushoto ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim  Majaliwa.

Na Lilian Lundo - MAELEZO
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere umeongeza idadi ya abiria watakaokuwa wakihudumiwa na Uwanja huo kutoka abiria milioni 2 mpaka abiria milioni 8 kwa mwaka. Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Uwanja huo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.
"Mradi huu umekamilika na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 720. Kukamilika kwa mradi huu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya fedha za Serikali na nidhamu ya kutumia fedha hizo," amesema Rais Magufuli.
 Rais Magufuli amesema asilimia 100 ya fedha za ujenzi wa jengo hilo ni fedha za Watanzania ambapo asilimia 15 imelipwa fedha taslimu na asilimia 85 imekopwa na itarejeshwa kupitia kodi.
"Watanzania tunaweza, tunachotakiwa ni kujiamini na kuamua kufanya. Bila kuamua Tanzania tutaendelea kuwa wategemezi katika miradi ya maendeleo ya nchi yetu," amesema Rais Magufuli.
Aidha, ameitaja miradi mingine inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutumia fedha za ndani kuwa ni mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji wenye thamani ya shilingi trilioni 6.5, daraja la Selander lenye thamani ya shilingi bilioni 270, ujenzi wa viwanja vya ndege 15 nchini vyenye thamani ya shilingi ya trilioni 1.868, ujenzi wa vituo vya afya 352, zahanati 30, hospitali 67 na ukarabati wa hospitali za zamani 21 wenye gharama ya shilingi bilioni 321.6 pamoja na  ujenzi wa barabara wa nchi nzima wenye jumla ya kilomita 2105 yenye gharama ya shilingi trilioni 5.37.
Miradi mingine ni ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi katika ziwa Victoria, barabara ya njia ya nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi Kibaha, ununuzi wa rada, utanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, ununuzi wa vifaa vya hospitali pamoja ukarabati wa shule kongwe.
Rais Magufuli amesema kuwa, heshima ya miradi yote hiyo iwaendee Watanzania na kuwataka Watanzania kulifuta kabisa neno la kujiita masikini kwani Tanzania ni nchi tajiri.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema Jengo la pili la abiria nalo linahitaji kukarabatiwa na kuongezwa uwezo wa kubeba abiria mara mbili ya sasa, ambapo kwa sasa lina uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama amesema taasisi yake imeshahamishia shughuli za uendeshaji wa ndege katika Jengo hilo kutoka Jengo la abiria la pili.
Vile vile amesema, jumla ya vijana 130 kati ya vijana 241 waliokuwa wanahitajika wameajiriwa, ambapo kwa sasa wapo katika mafunzo ya nafasi walizopangiwa kufanya kazi.
Vile vile Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patric Mfugale amesema ujenzi wa jengo la abiria la kwanza ulijengwa mwaka 1956 ambapo unauwezo wa kuhudumia abiria laki 5 kwa mwaka. Mwaka 1984 ilikamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria ambalo linauwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka.
Amesema baada ya kuonekana jengo la pili la abiria kutotosheleza abiria wanaohudumiwa uwanjani hapo, ndipo Serikali ilipoamua kuanza ujenzi wa jengo la tatu la abiria, ambalo ni jengo la kisasa zaidi ukilinganisha na majengo yote ya abiria hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.