Habari za Punde

Balozi Seif afanya ziara ya ghafla Skuli ya Maandalizi ya Msingi ya Mbuyu Maji, Mkwajuni

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akifanya ziara ya ghafla kukagua Skuli ya Maandalizi na Msingi ya Kijiji cha Mbuyu Maji ndani ya Jimbo la Mkwajuni.
  Balozi Seif Ali Iddi wa Tatu kutoka Kulia akimuuliza Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Maandalizi ya Msingi ya   Mbuyu Maji Mwalimu Juma Mcha Ussi changamoto zinazoikabili Skuli yake alipotembelea ghafla
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” Nd. Hassana Mcha Hassan akimueleza Balozi Seif hatua inayochukuwa Halmashauri yake katika kupunguza changamoto zilizomo ndani ya Majengo mapya yanayojengw
 Balozi Seif  akionya Kiongozi au Mtendaji wa Halmashauri anayeshindwa kuwajibika bora aachie ngazi ili kupisha wengine alipokuwa akikagua Skuli ya Maandalizi na Msingi ya Mbuyu Maji ndani ya Jimbo la Mkwajuni.
 Balozi Seif akiwahidi Wananchi wa Mbuyu Maji na Mililile kwamba Serikali itaendelea kubeba dhamana ya kuwapatia maendeleo kwa yale mambo yaliyo nje ya dham,a ya Halmashauri yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuwasogezea Maendeleo yaliyojikita katika upatikanaji wa huduma muhimu za Elimu, Afya, Kilimo pamoja na Maji safi na salama unajenga Historia ya kudumu kwa Wananchi walio wengi wa Vijiji vyilivyomo ndani ya Jimbo la Mkwajuni Mkoa Kaskazini Unguja.
Kauli hiyo imetolewa na Bibi Kazija Mazi kwa niaba ya Wananchi wa maeneo hayo kufuatia ziara ya ghafla ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Blozi Seif Ali Iddi aliyefika Jimboni humo kukagua Utekelezaji wa Agizo la Rais wa  Zanzibar Dr. Ali Mohamed la kuamuru uimarishwaji wa Huduma za Kijamii.
Agizo hilo la Rais lililengwa kwa Halmashauri ya Wizara ya Kaskazini “A” kujenga miundombinu ya upatikanaji wa Huduma za Elimu ya maandalizi na Msingi, Afya, Bara bara na Maji safi na salama ili kuwaondoshea usumbufu wa muda mrefu ananchi hao.
Bibi Kazija Mazi alimueleza Balozi Seif  aliyepata wasaa wa kukagua maendeleo ya Muindombinu ya Skuli za Mbuyu Maji na Milile kwamba Vijiji vya Mbuyu Maji na Mlilile vimebadilika kimaendeleo kwa kuzunguukwa na huduma za Maji, Elimu na Afya kiasi kwamba hawana budi kuishukuru Serikali yao kwa hatua iliyochukuwa ya kusogeza Maendeleo hayo.
Alisema Wananchi na hasa Watoto wa Vijiji hivyo hivi sasa wamepata faraja na kuwa na muda wa kutosha wa kushughulikia masuala mengine ya Kijamii na kuepuka nguvu zao hasa kina mama kuzitumia katika kufuata huduma ya Maji safi masafa marefu.
Hata hivyo Bibi Kazija Mazi akionyesha furaha na bashasha ya uwepo wahuduma hizo aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Balozi Seif na Taasisi inayosimamia Huduma za Maji kutatua tatizo la kukatika katika kwa huduma hiyo kwa baadhi ya wakati.
Mapema Viongozi wa Halmashauri pamoja na Serikali wa Wilaya ya Kaskazini “A” walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua za kuiendeleza Miradi ya Kijamii ndani ya Wilaya hiyo zinaendelea vyema licha ya mabadiliko makubwa ya Mfumo wa Madaraka Mikoani maarufu Ugatuzi.
Walisema ipo Miradi ya Elimu katika Ujenzi wa Majengo Mapya ya Skuli za Maandalizi na Msingi ambayo bado hayajakabidhiwa kwa Halmashauri kutoka Wizara ya Elimu katika Mfumo wa Ugatuzi lakini hatua zinachukuliwa katika kukamilisha kazi za usambazaji Maji, ukamilishaji wa vyoo pamoja na Madawati.
Viongozi hao walimueleza Balozi Seif kwamba zipo changamoto zilizorithiwa kutoka Taasisi za awali na kuingizwa katika usimamizi wa Halmashauri mara baada ya kuanza kwa mfumo wa Ugatuzi ambazo nyengine bado nguvu za Serikali kuu zitaendelea kuhitajika katika kuzitafutia ufumbuzi.
Akizungumza na Viongozi, Walimu, Watendaji wa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” pamoja na Wananchi wa Mbuyu Maji na Mlilie katika mikutano Miwili tofauti Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba Kiongozi wa Serikali au Halmashauri ya Wilaya hiyo asiyekubali kuwajibika kwa kujichunga mwenyewe ni vyema akaachia ngazi mapema.
Balozi Seif alikemea kwamba zipo changamoto zinazoendelea kuota mizizi katika miradi iliyoanzishwa ya huduma za Kijamii ambazo zimo ndani ya uwezo wa Watendaji na Viongozi hao wa Serikali wa Wilaya lakini bado zinakwaza Maendeleo ya Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Halmashauri lazima ziangalie  njia sahihi za kuzitafutia dawa changamoto za Maji Safi na Salama, Vikalio vya Maskuli pamoja na baadhi ya huduma za Afya ambazo ni jukumu linalopaswa kulichukulia dhamana kwa vile liko ndani ya mamlaka yao.
Alisema Serikali Kuu itajitahidi kuongeza nguvu zake katika masuala muhimu yaliyomo ndani ya Sekya za Afya, Elimu na Kilimo, lakini akasisitiza suala la kuimarishwa zaidi Sekta ya Elimu inayomfunua macho Mtoto katika muelekeo wa Hatma yake njema.
Aliwakumbusha Viongozi hao wa Serikali na Halmashauri kuelewa kwamba zipo changamoto zitazooendelea kujichomoza wakati wa utekelezaji wa Mfumo wa Ugatuzi katika Halmashauri mbali mbali Nchini, akini kinachohitajika zaidi ni uvumilivu na uchapakazi utakaweza kuzikabili changamoto hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alipata wasaa wa kuikagua Skuli ya Maandalizi na Msingi ya Mbuyu Maji ambayo jumla ya Wanafunzi 102 wameanza masomo yao licha ya ukosefu wa vikalio.
Baadae Balozi Seif  alitembelea Majengo ya Skuli ya Milile yanayoendelea kujengwa yakiwa katika hatua za mwisho umaliziaji wake yanayotarajiwa kuhudumia Wanafunzi zaidi ya 1,000 ili kuondosha kero zinazowakabili Watoto wa eneo hilo kufuata Elimu masafa marefu.
Majengo yote Mawili pamoja na uimarishaji wa Miundombinu ya Bara bara na Maji Safi yanajengwa na kutekeleza Agizo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alioutaka kwa Uongozi wa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” la kuwaondoshea kero Wananchi wa Maeneo hayo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.