Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Awaapisha Mkuu wa Mkoa wa Kusini na Mjini Magharibi Unguja Ikulu leo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akimuapisha Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja hafla  leo katika    ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar kabla  Ayoub alikuwa Mkku wa Mkoa wa mjini Magharibi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akimuapisha Mhe.Hassan Khatib Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi hafla iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar kabla  alikuwa Mkoa wa  Kusini Unguja

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaapisha Wakuu wa Mikoa ya Kusini Unguja na Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja aliowateua hapo jana.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Dk. Shein amemuapisha Ayoub Mohammed Mahmoud kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja.

Mwengine ni Hassan Khatib Hassan aliyemuapisha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo kabla ya uteuzi wake alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja na Ayoub Mohammed Mahmoud alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Viongozi wengine waliohudhuria katika hafla hiyo ni Spika wa Baraza la Wawakilishila Zanzibar Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali Mitaa na Idara Maalum za SMZ Shamata Shaame Khamis.  

Viongozi wengine waliohudhuria  ni Washauri wa Rais, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib Wakuu wa Vikosi vya SMZ pamoja na Washauri wa Rais wa Zanzibar na viongozi wengine wa Serikali.

Nao Wakuu hao wa Mikoa kwa upande wao walieleza jinsi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alivyoendelea kuwaamini na kuwateua na hatimae kuwaapisha kushika nyadhifa hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud alitoa shukurani kwa wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa mashirikiano yao mazuri waliyompa wakati wote alipokuwa Mkuu wa Mkoa huo.


Aidha, alieleza kuwa anakokwenda hivi sasa anakwenda kujifunza na baadae atatekeleza na kuendeleza yale yote yaliyoachwa na mwenziwe aliyemtangulia katika Mkoa huo na kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Kusini wampokee na waendelee kushirikiana nae kwa azma ya kutekeleza majukumu ya Serikali sambamba na kutatua baadhi ya changamoto zilizopo kwa mashirikiano ya pamoja na Serikali.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Hassan Khatib Hassan aliahidi kuwa ataendelea kuilinda  Katiba ya Zanzibar  pamoja na maslahi ya wananchi wa Zanzibar na viongozi wake wote.

Mkuu wa Mkoa huyo alieleza kuwa Mkoa wa Mjini Magharibi ni wa wananchi wote hasa ukizingatiwa kuwa ndio wenye Mji wa Zanzibar hivyo, kuna kila sababu kwa wananchi kushirikiana kuutunza ili uendelee kuwa kivutio cha watalii na wageni wengine wanaoitembelea Zanzibar kwani miji ndio inayotoa taswira ya nchi.

Hivyo, Mkuu wa Mkoa huyo alisisitiza haja ya kuendelea kuutunza mjini huo ambao hivi sasa ni Jiji la Zanzibar pamoja na vivutio vyote vilivyomo ndani yake na kuahidi kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.