Habari za Punde

Serikali kuendelea kuimarisha huduma za elimu kuleta maendeleo nchini

Na Maulidalid Yussuf WEMA.



NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma mbalimbali zikiwemo za Elimu ili kuleta maendeleo nchini.

Amesema kuimarika huduma za maktaba ni miongoni mwa juhudi za Serikali katika kuhakikisha sekta ya Elimu inakuwa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya kujua kusoma na kuandika, katika viwanja vya Shirika la Huduma za Maktaba Maisara Mjini Unguja, Mhe Simai amesema maktaba ni sehemu muhimu katika kujiendeleza kielimu,kwani mbali na kusoma vitabu pia kuna masuala mengi uanaweza kumsaidia mtu katika kuelimika.

Mhe Simai amewataka wazazi kuwahimiza watoto wao kusoma pamoja na kuzitumia maktaba zilipo katika Wilaya zao kwa kujiendeleza  ili waweze kuwa wataalamu bora wa baadae.

Aidha amewataka watoto kuzitumia huduma za maktaba pamoja na kuwa makini kwa kuvitunza vitabu vilivyomo ndani ya maktaba ili viweze kudumi kwa muda mrefu na kuweza kuwasaidia na wengine.

Hata hivyo amewataka wazazi kuwafuatilia kwa makini watoto wao maendeleo ya Elimu katika Skuli zao na kuwa tayari kuitikia wito wakati wanapohitajika Skuli kwa lengo la kuleta maendeleo ya Elimu kwa watoto wao.

Pia amewataka wazazi kuwasimamia watoto juu ya maadili mema na kuwa heshima kwa kujali utamaduninwa nchi yao hasa katika mavazi kwani vijana wengi wanaonekana kuharibika kwa kufuata utamaduni wa nje.

Nae Mkurugenzi wa Shirika la Huduma za Maktaba bi Sichana Haji Foum amesema kufanyika kwa maadhimisho hayo kunatoa nafasi ya kujadili changamoto zinazopelekea kuwepo kwa watu wengi kutojua kusoma na kuandika ikiwa miongoni mwao ni watoto, vijana na watu wazima.

Amesema kwa muibu wa tafiti zilizofanywa na Shirika la maendeleo ya Elimu UNESCO mwaka 2016, zinaonesha kuwa watu wazima milioni 775 sawa na asilimia 20 ya watu wote duniani  hawajui kusoma wala kuandika ambapo idadi ambayo ni kubwa.

Hivyo amesema juhudi madhubuti zinahitajika kuchukuliwa ili kupunguza au kuondosha kabisa tatizo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakutubi bw Khamis Hamadi Mwintumbe amesema lengo la kuundwa kwa jumuiya yao ni kuhakikisha Wakutubi pamoja na maktaba vinapiga hatua katika kuleta maendeleo ya kielimu kwa kutoa Mafunzo mbalimbali katika taasisi zao.

Hata hivyo amewahamasisha wanafunzi kuzitumia maktaba ili ziweze kuwasaidia na kusonga mbele katika ukuaji wa Elimu. 

Siku ya Kimataifa ya kujua kusoma na kuandika itafikia kilele chake tarehe 8 Septemba ambapo Mataifa mengi Duniani yataadhimisha, ikiwa na ujumbe wa mwaka Huu ni "Kujua kusoma na kuandika kuendane na kujifunza lugha mbalimbali."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.