Na. Mwandishi Wetu -Bagamoyo.
MSANII wa muziki wa kizazi kipya anayefanya vizuri katika muziki wa kizazi kipya, Elias Barnabas ‘Barnaba’ amewapa somo wasanii wenzake na kuwaeleza watenganishe Ustaa na Umaarufu.
Akizungumza akiwa katika jukwaa la tamasha la 38 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Barnaba alisema kuna baadhi ya wasanii wanachanganya mambo hayo mawili, jambo ambalo linasababisha baadhi ya wasanii kufanya mambo ambayo yanachafua kazi hiyo.
Barnaba alisema baadhi ya wanaofanya mambo machafu kwa kutumia sanaa, wanakuwa hawana muda mrefu katika fani kwa sababu ya kutafuta ‘kiki’ badala ya kusaka namna ya kuboresha kazi zao.
“Sitaki kuwasema wanaochafua taswira ya sanaa, lakini mnawajua, msifanye siasa za namna hiyo ambazo hazileti maana katika kuelimisha jamii,”alisema Barnaba.
Alisema msanii ili afikishe ujumbe kwa jamii sio lazima afanye mambo ya ajabu kama yanayotendeka, mambo mengine ni baadhi ya wasanii kuvaa mavazi ambayo yanavuruga maadili.
Aidha kabla ya Barnaba kupanda jukwaani, walioanza kufikisha ujumbe kwa jamii katika tamasha hilo ni kundi la Mazingaombwe la Ngome la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliogawa soda na kuonesha uwezo wa kutafuna nyembe sita.
Burudani nyingine iliyooneshwa katika tamasha hilo linaloendelea ni maigizo ya kundi la Magic Bean Theatre Company la nchini Zimbabwe ambalo lilijikita katika utoaji elimu wa ulinzi kwa wanyama pori wakiwemo Tembo.
Pia kulikuwa na maonesho mengine kama igizo la kulinda ngoma zetu, lililotolewa na wanafunzi wa shule ya msingi Mwambao.
No comments:
Post a Comment