Habari za Punde

HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI ALIYOITOA WAKATI WA KUAKHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA TANO WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI TAREHE 04/10/2019


Mheshimiwa Spika,
Naomba nianze hotuba yangu hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwenye wingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na Tano wa Baraza la Tisa ulioanza tarehe 18 Septemba, 2019 hadi leo tarehe 04 Oktoba, 2019 tunapouakhirisha. Mkutano ambao tumeweza kukamilisha shughuli zote zilizopangwa kwa mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika,
Baraza lako tukufu limepokea na limejadili Miswada mitatu na imepitishwa kuwa sheria. Miswaada yenyewe ni :
· Mswada wa kufuta Sheria ya Viongozi wa Kitaifa nam. 10 ya mwaka 2002 na         kutunga Sheria inayoweka Utaratibu wa Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa.
·  Mswada wa Sheria ya Utawala wa Baraza.
·   Mswada wa Sheria wa Kuanzisha Jumuiya ya Mawakili Zanzibar, Kuweka Malengo, Utekelezaji wa Shughuli za Jumuiya.
Mheshimiwa Spika, 
Miswada hiyo itaiwezesha Nchi yetu kuwa na utaratibu mzuri zaidi wa kisheria wa Kuwaenzi Viongozi wetu wa Kitaifa. Mswada wa Sheria ya Utawala wa Baraza umetungwa ili kutekeleza Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyolipa mamlaka Baraza ya kutunga Sheria na italiwezesha Baraza lako Tukufu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika kuimarisha Utawala Bora Nchini.Mheshimiwa Spika,
Aidha, Baraza lako tukufu limepokea Ripoti za Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya utekelezaji wa maelekezo wa kamati za kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2018/2019 zinazohusiana na Wizara zao. Ripoti zote hizo zilichangiwa kwa kina na maoni kutolewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu na hatimae Ripoti hizo zilipokelewa.
Mheshimiwa Spika,
Nachukua nafasi hii kuzipongeza Kamati zote za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa utekelezaji wa majukumu yao kwa umakini, weledi na umahiri mkubwa. Pia nazipongeza Wizara zote kwa  uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa maelekezo ya Kamati hizo. Nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe kwa michango waliyoitoa ambayo itaisaidia sana Serikali katika utekelezaji wa shughuli zake.

Mheshimiwa Spika,
Natoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa Uongozi wao mahiri na makini katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Serikali zetu, ikiwemo kufanya mabadiliko ya Uongozi katika ngazi mbali mbali ndani ya Chama na Serikali kwa lengo la kuendeleza ufanisi katika utendaji na usimamizi wa Demokrasia na Utawala bora.
Kadhalika, nawapongeza viongozi wetu hao kwa namna wanavyoendelea kufuatilia Utekelezaji wa shughuli za Serikali, hatua ambazo zinaendelea kutuletea mafanikio makubwa yanayoonekana. Vile vile, natoa pongezi maalum na za aina yake kwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuteuliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya za nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) katika Mkutano wa 39 uliofanyika tarehe 17 hadi 18 Agosti Jijini Dar es Salaam ambao ulifana sana. Kufanyika kwa mkutano huo nchini kwetu nchi yetu ilipewa heshima kubwa. Aidha kufanikiwa kwake kumeonyesha ni kiasi gani nchi yetu inaweza kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukuwa fursa hii kukupongeza wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza letu Tukufu, Naibu Spika Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma pamoja na Wenyeviti wote wa Baraza kwa kuviendesha vyema vikao vyetu kwa hekima, busara na weledi mkubwa na kukifanya kikao hiki kumalizika kwa amani, salama na mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kikao hiki jumla ya maswali ya msingi 137 na maswali ya nyongeza ........yaliulizwa na yalijibiwa kwa ufasaha na ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Spika,
Tunatoa pongezi za dhati kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa utekelezaji wa kazi zake na kuwaelimisha Viongozi wa Umma kutekeleza Sheria na agizo la Ujazaji wa Fomu za maadili.  Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa imeeleza kwamba mwaka 2018/2019 fomu zilizowasilishwa 1,702 sawa na asilimia 103% ambao viongozi waliwasilisha ndani ya muda 1,672 na ambao walichelewa ni 26 sawa na asilimia 2%. Tunapenda kuwakumbusha watendaji wote wanaopaswa kujaza fomu za maadili katika mwezi wa Disemba wajitahidi kukamilisha kuzijaza na kuziwasilisha kwa wakati fomu hizo ili kukidhi matakwa ya kisheria. Tunawaomba ile asilimia chache iliyobakia wajitahidi kutekeleza agizo hilo la Kisheria kwa wakati, kabla ya sheria kuchukua mkondo wake.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi ni matendo yasiyovumilika ndani ya nchi yoyote, kumekuwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu bado wanaendelea kuhujumu uchumi kwa kupokea au kutoa rushwa na kuisababishia nchi hasara au wananchi wake kuwafanya kuwepo katika mazingira magumu wakati wanapohitaji huduma za kijamii. Hadi kufikia mwaka 2018 kumekuwa na tuhuma za uhujumu uchumi na rushwa zipatazo 108 ambazo upelelezi wake bado haujakamilika. Nawaomba wafanyakazi na Watumishi wa Umma na Sekta binafsi na wale wote wanaotoa huduma kujiepusha na utoaji na upokeaji wa rushwa pamoja na uhujumu uchumi. Hivyo, natoa maelekezo kwa vyombo vinavyohusika kuondoa muhali na kuharakisha upelelezi wake ili wahusika wafikishwe katika vyombo vya sharia na sharia ichukue mkondo wake haraka.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa majimbo yote 54 ya Unguja na Pemba. Dhamira ya Serikali kutoa fedha hizo ni kuwapa fursa wananchi wa Zanzibar ili waweze kuchagua aina ya Shughuli za maendeleo wanazozihitaji katika maeneo yao, hasa katika kutatua changamoto zinazowakabili. Nachukua nafasi hii kuziomba Kamati za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kuendelea kuzitumia fedha hizo kwa kufuata matakwa ya Sheria iliyopo ili tuzidi kupiga hatua za maendeleo. Pia, nawaomba Wawakilishi wote warudi Majimboni na kukamilisha ahadi walizozitoa na kuzisimamia zile zilizotolewa na Serikali, ili kukamilisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015/2020 iliyojiwekea. Kama tujuavyo ahadi ni deni, na deni hulipwa.

Aidha, nazitaka Kamati zote za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kufanya marejesho kwa wakati ili hatua nyengine ziendelee kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika,
Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini – TASAF Awamu ya Tatu umeendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa ambapo Walengwa wa Mpango huu wameweza kuongeza vipato vya kaya zao kupitia miradi mbali mbali inayotekelezwa na Mpango huu pamoja na kuongeza kasi ya upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya kibinaadamu. Katika kipindi cha kwanza cha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III -1), jumla ya Shehia 204 kwa Unguja na Pemba zilitekeleza Mpango huu ambapo tayari umeshakamilisha kipindi cha miaka mitano ya awali. Kutokana na umuhimu wake na mafanikio yaliyoonekana kwa wananchi katika Shehia hizo zilizotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini hapo awali, Serikali zetu zimeamua kupeleka utekelezaji wa Mpango huu kwa vijiji vyote vya Tanzania bara na Shehia zote za Zanzibar na matayarisho ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kwa miaka mitano ijayo ya kipindi cha pili yanaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika,
Matumaini yetu kuwa wale wote watakaotimiza vigezo vya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kwa kipindi cha pili watapata fursa ya kujumuishwa katika Mpango huu. Natoa wito kwa Viongozi wa ngazi zote kuendelea kutoa mashirikiano ya kuyaenzi na kuyatunza mafanikio yaliyopatikana pia tushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Miradi hii mara tu utakapoanza muendelezo wake.
Mheshimiwa Spika,
Waheshimiwa Wajumbe na wananchi, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Ofisi ya Zanzibar kwamba hivi karibuni nchi yetu inategemea kuanza kupata mvua za wastani na juu ya wastani katika msimu wa vuli. Tunawaomba wananchi wazitumie vizuri mvua hizo wakisaidiwa na maelekezo ya wataalamu wa kilimo. Vile vile, wananchi wanaoishi katika maeneo yenye hatari yanayoweza kukumbwa na mafuriko, wahame katika maeneo hayo ili kujiepusha na athari zitakazotokana na mafuriko ambayo huwakumba katika msimu wa mvua unapowadia. Aidha, tuendelee kufuatilia taarifa za kitaalamu zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kupitia vyombo vya habari nchini na tufuate maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya ili kujikinga na maafa na maradhi ya mripuko yanayoweza kutokea.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na maradhi ya mripuko imezindua Mpango Shirikishi wa miaka kumi (10) wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar ‘’Zanzibar Comprehensive Cholera Elimination Plan 2018-2027’’ wenye lengo la kuondosha kabisa usambaaji wa vimelea vinavyoeneza maradhi ya kipindupindu hapa Zanzibar. Katika kufanikisha azma hiyo mikakati ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu itakayolenga katika kukinga na kudhibiti miripuko na kutokomeza kabisa maradhi hayo hapa nchini imewekwa.
Aidha, mpango huu pia unalenga katika kujenga mazingira yatakayowezesha kutokomeza maradhi ya kipindupindu Zanzibar, kuongeza ufanisi wa huduma dhidi ya maradhi hayo na maradhi mengine ya kuharisha. Vile vile, mpango huu utaweza kuimarisha uwezo wa kukabiliana na kudhibiti miripuko ya kipindupindu. Nawataka Waheshimiwa Wawakilishi tushirikiane na wananchi wote katika kuendeleza utaratibu wa kusafisha mazingira yetu na kufuata sheria na kanuni za afya ili kuepukana na maradhi haya.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo vya udhalilishaji bado vinaendelea kuwa tishio katika nchi yetu vikitoa sura mbali mbali ikiwa ni pamoja kupiga na kubakwa kwa wanawake na watoto wadogo, kutelekezwa kwa watoto wachanga, talaka zisizofata utaratibu, ushirikishwaji wa watoto wenye umri mdogo katika biashara zikiwemo biashara haramu za madawa ya kulevya. Vitendo hivyo vinakwenda kinyume na mila, silka, desturi, na utamaduni wetu. Kwa mara nyengine tena nawakumbushia wazee, jamii na viongozi wa ngazi na nyanja mbali mbali pamoja na wananchi, kwa kila mmoja wetu kuendelea kutekeleza wajibu wake katika kupinga suala hili. Serikali inavisisitiza vyombo vyote vinavyohusika pamoja na wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, tukumbuke Zanzibar bila ya unyanyasaji na udhalilishaji inawezekana mradi tu kila mmoja wetu atimize wajibu wake ipasavyo.
Mheshimiwa Spika,
Changamoto ya madawa ya kulevya duniani bado inaendelea kutishia maisha ya watu wengi.Takwimu zinaonesha kuwa kutoka Januari hadi June mwaka 2019 Jumla ya kesi zote za madawa ya kulevya nchini ni 269. Kesi zilizofika Mahakamani ni 56 tu, na kesi ambazo ziko chini ya upelelezi ni 163. Kesi ambazo ziko chini ya Mkurugenzi wa Mashataka ni 10, kesi zilizopo kwa Mkemia ni 23, na kesi zilizoondolewa polisi ni 17. Ukubwa wa tatizo hilo unaendelea kuonekana kwa matokeo tofauti yanayoendelea kuibuka siku hadi siku ikiwemo vitendo vya kihalifu wanavyofanya watumiaji wa madawa hayo.
Mheshimiwa Spika,
Hata hivyo, nachukua nafasi hii kuzipongeza taasisi zote zinazoshughulikia kudhibiti kwa madawa hayo ikiwemo Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, taasisi binafsi pamoja na raia wema kwa namna wanavyoshirikiana na Jeshi la Polisi katika kudhibiti maovu mbali mbali yakiwemo madawa ya kulevya na rushwa. Nalikumbusha Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha mapambano yatakayokwenda na wakati  ili tuweze kupata mafanikio zaidi katika vita hivi.
Mheshimiwa Spika,
Nawakumbusha Waheshimiwa Wajumbe na ndugu wananchi sote ambao ni mashahidi kwamba ajali za barabarani bado zinaendelea kutishia maisha yetu, kutuachia simanzi, majonzi na athari kubwa hali ambayo inahitaji kudhibitiwa kwa kuimarishwa mashirikiano ya pamoja na wahusika wote. Katika kukabiliana na hali hiyo natoa wito kwa wahusika wote wa matumizi ya barabara kuzingatia Sheria na Kanuni zinazoongoza na kuelekeza matumizi mazuri ya barabara. Serikali katika kuendelea kudhibiti ajali za barabarani imeendelea kuchukua hatua za uimarishaji wa miundombinu ya usafiri kwa ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja, vibomba, uwekaji wa taa na alama za barabarani mijini na vijijini, Unguja na Pemba. Kwa upande wa ujenzi wa barabara Serikali imekamilisha baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami kati ya hizo ni pamoja na barabara ya Kuyuni – Ngomeni, Msingini – Chake, Mkanyageni – Kangani, Mkoani – Ng’ombeni skuli, Wawi – Mabaoni, Magogoni – Kinuni – Nyarugusu na Fuoni – Mambosasa. Vile vile Serikali imekamilisha Kwa kiwango cha kifusi barabara ya Mfurumatonga – Mbuumaji, Mlilile – Kijibwe, Kizimbani – Kiboje na Pujini – Kibaridi. Aidha, Serikali inaendelea na Miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara katika sehemu tofauti Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na madaraja yake. Ujenzi huo unaoendelea ni pamoja na barabara ya Kwanyanya - Mkokotoni, Pale – Kiongole, Fuoni – Kombeni, Matemwe – Muyuni, Jozani – Ukongoroni – Charawe – Bwejuu, Gombani – Pagali, Fuoni Mambosasa – Mwera Wilayani, Koani – Jumbi na barabara ya Kilombero – Mgonjoni. Serikali inajenga barabara hizo ili kusaidia usafiri mzuri kwa wananchi na mazao yao. Hatutegemei na wala hatukusudii barabara hizo ziwe chanzo cha mauti au ulemavu wa kudumu kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua fursa hii kuwaonya wale watu wanaoendesha vyombo vya moto vya magurudumu mawili kuvaa kofia ngumu kama sheria inavyoelekeza kwani kufanya hivyo ni kwa faida yao wenyewe.  Nawaagiza askari wa barabarani kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka sheria inayohusika.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea na uwekaji wa taa za kuongoza matumizi mazuri ya barabarani (Trafic light) katika sehemu tofauti Unguja na Pemba. Miongoni mwa sehemu zilizokamilika ni kwa Biziredi, Mtendeni, Mtoni, Mlandege na Benki ya Watu wa Zanzibar Chake Chake Pemba.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeweka utaratibu mpya na maalum wa matumizi ya vituo vya daladala, hivyo ni vyema kwa taasisi husika kutoa elimu kwa wananchi juu ya mabadiliko hayo yanayoendana na mpango mji wa nchi yetu sambamba na kupunguza msongamano wa magari barabarani. Pia, utaratibu wa kupakia na kushusha abiria uzingatiwe kwa namna ulivyowekwa na Serikali ili kuondoa usumbufu usiyokuwa wa lazima kwa wananchi wetu au kusababisha msongamano wa magari barabarani.
Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) imekamilisha ujenzi wa skuli saba (7) kati ya skuli tisa (9) zilizojengwa kupitia Mradi wa Tatu wa Elimu (Third Education Project). Wizara tayari imeshakabidhiwa rasmi skuli nne kati ya hizo kutoka kwa wakandarasi wa ujenzi na mchakato wa kukamilisha makabidhiano ya skuli tatu zilizokamilika unaendelea. Skuli zilizokamilika na kukabidhiwa Serikalini ni Muembeshauri, Kinuni, Fuoni na Chumbuni. Aidha skuli zilizokamilika na ambazo zitakabidhiwa mwezi huu wa Oktoba ni Skuli ya Bububu, Wara na Micheweni. Skuli mbili ambazo ujenzi utakamilika Novemba ni Kizimbani na Mwambe Pemba. Skuli hizi zote zitakuwa na madarasa 144 na hivyo kuongeza nafasi za masomo kwa watoto 11,520 kwa mikondo miwili kwa wastani wa wanafunzi 40 kwa darasa.
Mheshimiwa Spika,
Mahitaji ya rasilimali ya mchanga yameongezeka kutoka tani 200,000 mwaka 2011 hadi tani 1,026,660 mwaka 2018, matumizi ya mawe kutoka tani 38,182 mwaka 2011 hadi tani 61,761 mwaka 2017, matumizi ya Kokoto tani 15,072 mwaka 2011 hadi tani 43,260.50 mwaka 2017 na matumizi ya kifusi kutoka tani 14,943.35 mwaka 2011 hadi 38,081.50 mwaka 2017. Ongezeko hili ni kubwa na linapelekea upungufu wa maliasili hizo na uchafuzi wa mazingira, jambo ambalo linahitaji mazingatio makubwa hasa ikizingatiwa kwamba nchi yetu ni ya Visiwa. Kwa mantiki hiyo tunawaomba Waheshimiwa Wawakilishi na wananchi wote wawe wavumilivu wakati Serikali yao iko mbioni kutafuta suluhisho la kudumu kwa maslahi ya vizazi vilivyopo na vitakavyokuja pamoja na uhifadhi wa mazingira ya visiwa vyetu. Jana tulikuwa na Semina iliyohusu ardhi na mali zisizorejesheka. Watoa mada wetu walitueleza kwa kina juu ya athari ambayo nchi yetu inaweza kupata iwapo utumiaji wa rasilimali hizo hazitotumiwa vizuri. Haikuwa nia ya Serikali kuwasumbua wananchi isipokuwa ilikuwa inajaribu kudhibiti utumiaji wa rasilimali hiyo ili itumiwe vizuri.
Mheshimiwa Spika,
Malalamiko na migogoro ya ardhi bado yanaendelea kuikumba nchi yetu. Kumekuwa na kesi nyingi sana zinazojitokeza siku hadi siku kufuatia matumizi ya ardhi yasiyoeleweka. Leo hii, tunashuhudia kuona kiwanja kimoja kina nyaraka zaidi ya moja. Pia, kumekua na utashi na upendeleo baina ya mlalamikaji au mlalamikiwa, hususan  kwa watu waliouziwa maeneo au waliorithi kutoka kwa wazazi wao unaofanywa na wasimamizi wa sharia za ardhi. Hivyo tunapenda kuwatahadharisha watendaji wote wenye dhamana ya ardhi, kusuluhisha migogoro hii kwa kufuata sheria zote tisa (9) za matumizi ya ardhi zilizopo bila ya ubaguzi baina ya mtu mmoja na mwengine. Ili kuepusha kuibebesha Serikali lawama na kuijengea chuki na wananchi wake.
Mheshimiwa Spika,
Kumekuwa na utaratibu hapa nchini wa kuweka wanyama mchanganyiko kwenye maeneo ya watu binafsi (zoo). Kama vile, mbwa, farasi, kondoo, chui, mamba, simba, mbwa mwitu, chatu, na wengineo. Imegundulika kuwa baadhi ya maeneo hayo yanashindwa kuwadhibiti baadhi ya wanyama hao. Kitendo hiki hupelekea baadhi ya wanyama kutoroka na kukimbilia mitaani au kuingia kwenye mito, jambo ambalo linaleta taharuki kubwa kwa
wananchi waliokaribu na maeneo hayo. Hivyo, Wizara husika wayafanyie uhakiki wa mara kwa mara maeneo hayo na wahakikishe zinaakisi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria, ili kuepusha maafa makubwa yanayowezwa kusababishwa na wanyama hao wakali. Aidha, wamiliki wa maeneo hayo wajihadhari ili wanyama wao wasiingie mitaani, kama walivyoingia wale mamba waliogundulika katika mto wa barafu, na vile vile wahakikishe wana wataalamu wa kutosha katika udhibiti wa wanyama ndani ya maeneo yao.
Mheshimiwa Spika,
Tunawashukuru Waheshimiwa Wawakilishi kwa kutumia nafasi yao ya Kidemokrasia ya kuisimamia, kuishauri na kuihoji Serikali, jambo ambalo limeonesha nia thabiti mliyonayo ya kuitaka Serikali yenu kuwajibika ipasavyo kwa wananchi wake.  Kadhalika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kujibu maswali yote mliyoulizwa, mliweza kuyatolea ufafanuzi ambao uliwanufaisha Waheshimiwa Wajumbe pamoja na wananchi kwa ujumla. Nawaomba Waheshimiwa Wajumbe tuendelee kupendana, kuvumiliana na kushirikiana katika kuijenga nchi yetu kiuchumi na kijamii kwani mshikamano na umoja wetu ndio utakaoivusha nchi yetu kuelekea kwenye maendeleo endelevu. Aidha, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ufafanuzi wake alioutoa katika mambo mbali mbali yaliyohitaji ufafanuzi wa kisheria.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwashukuru wale wote waliotuwezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Kumi na Mbili wa Baraza la Tisa la Wawakilishi kwa ufanisi.  Pongezi hizo zaidi ziwafikie Watendaji wote wa Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu, Ndugu Raya Issa Msellem.  Ni ukweli usiofichika kwamba tumeanza vizuri na ninaamini tutaendelea vizuri.  Mungu libariki Baraza hili, Mungu ibariki Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Pia nawapongeza Wakalimani wetu wa lugha ya alama ambao wamewawezesha  Wale  wote  wenye  ulemavu  wa  kusikia kuweza kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Baraza hili Tukufu.  Vile vile, nawashukuru Wanahabari Kwa kufanya kazi nzuri ya kuwapatia habari wananchi wetu kwa shughuli zote ambazo zilikuwa zikiendelea kufanyika Barazani hapa.
Mheshimiwa Spika,
Mwisho kabisa kwa mara nyengine tena nikupongeze wewe binafsi, Mhe. Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa kuliongoza vizuri na kwa ufanisi mkubwa Baraza hili.  Hekima na busara zenu zimesaidia sana katika kuumaliza mkutano huu kwa salama na amani.   Mungu libariki Baraza letu la Wawakilishi, Mungu Ibariki Zanzibar na watu wake, Mungu Ibariki Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liakhirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2019, saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
 Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.