Habari za Punde

Walimu watakiwa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu

 Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwalim Moh’d Nassor Salim akizungumza na walimu wa Skuli mbali mbali za Sekondari walioajiriwa mwezi Oktoba 2018 na mwezi Mei 2019
 Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Massoud Ali Mohamed akizungumza na walimu wa Skuli mbali mbali za Sekondari walioajiriwa mwezi Oktoba 2018 na mwezi Mei 2019 katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake Pemba.

Walimu wa Skuli mbali mbali za Sekondari kisiwani Pemba walioajiriwa mwezi Oktoba 2018 na mwezi Mei 2019 wakiwa katika Ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake Pemba.

Na Ali Othman, Pemba

WALIMU kisiwani Pemba wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku wanapokua katika mazingira ya kazi.


Wito huo umetolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mwalim, Mohamed Nassor Salim katika semina elekezi kwa walimu wapya  iliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake Pemba.

Mwalimu Moh’d amwataka walimu hao kuwa mfano nzuri wa kuigwa katika nidhamu na uwajibikaji ili waweke kumbukumbu ya huduma njema kwa jamii.

Aidha aliwataka walimu hao kukemea vitendo vya udhalilishaji pamoja na kutojihusisha katika mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na misingi ya ualimu na kanuni za utumishi wa umma.

“Walimu ni kioo cha jamii hivyo mnapaswa kufanya kazi kwa umakini mkubwa” alisema Mwalimu Moh’d

Akiendelea kutoa nasaha zake kwa walimu haoAfisa Mdhamini pia  amewataka walimu hao kuwa na utamaduni wa kujisomea na kujiandaa vizuri kwa masomo wanayofundisha ili kuepusha sintofahamu na wanafunzi wao.

Kwa upande mwengine Mwalimu Moh’d amewaasa walimu hao kutojihusiha na masuala ya kisiasa badala yake wajikite kufundisha ili kuendelea kuinua kiwango cha ufaulu nchini ambacho kimekua kikipanda kila mwaka.

Ameeleza kuwa walimu hawana budi kutambua kuwa wapo kwa ajili ya kutoa elimu kwa watoto hivyo wanapaswa kutambua jukumu na wajibu huo.

Amebainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, imekua ikichukua juhudi za makusudi katika kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwemo ujenzi wa skuli za kisasa kila wilaya Unguja na Pemba pamoja na kutoa scholarship kwa wanafunzi wanaofaulu vizuri katika mitihani yao ya kidato cha sita.

Naye, Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Massoud Ali Mohamed amewashauri walimu hao kutobadilisha fani zao wanapojiendeleza kitaaluma kwani kufanya hivyo kunapekelekea tatizo la uhaba wa walimu.

Katika hatua nyengine , Bwana  Massoud amewasihi walimu hao kutumia nafasi walizonazo katika kukemea vitendo vya rushwa na udhalilishaji ambavyo vimekithiri katika jamii.

Aidha amewataka walimu hao kuwa na moyo wa uzalendo na kuipenda nchi yao pamoja na kuthamini juhudi mbalimbali za serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo kuboresha sekta hiyo ya elimu.

Mafunzo hayo elekezi ya siku mbili kwa walimu wapya yameandaliwa na Wizara ya Elmu na Mafunzo ya Amali Pemba yakishirikisha walimu wapya 101 kutoka Skuli mbali mbali za Sekondari kisiwani Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.