Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Kimataifa ya Elimu na Sayansi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Elimu na Sayansi kupitia Mfumo wa Kisasa wa Mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano {VM Ware} kutoka California Nchini Marekani.Kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi Mkurugenzi Muandamizi wa Mipango na Mikakati anayesimamia Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Kampuni hiyo Bwana Thomas Mackay, Msaidizi wake Bwana Kamau na Bibi Evan.Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanziar Mh. Simai Mhamed Said, Naibu Katibu Mkuu Nd. Abdullah Mzee Abdulla na Mkurugeni wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Wizara ya Elimu Nd. Omar Said Ali.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Kampuni ya Kimataifa ya Elimu na Sayansi kupitia Mfumo wa wa Kisasa wa Mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano {VM Ware} kutoka California Nchini Marekani tayari imeonyesha nia ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini.
Mkurugenzi Muandamizi wa Mipango na Mikakati anayesimamia Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Kampuni hiyo Bwana Thomas Mackay alitoa kauli hiyo wakati akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Thomas Mackay alisema Taasisi yake imejitolea  kusaidia nguvu za Kitaaluma katika Miradi ya Elimu kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika uimarishaji wa Miundombinu ndani ya Sekta hiyo muhimu kwa Maendeleo ya Taifa lolote Duniani.
Alisema mazingira ya maumbile ya Watu wa Visiwa vya Zanzibar yaliyojaa ukarimu yameushawishi Uongozi wa Kampuni hiyo kujitolea kusomesha mbinu na mikakati itakayowezesha kuibua kwa fursa za Taaluma kwa Vijana na Wasomi wa Zanzibar kupata mwanga zaidi wa hatma yao ya baadae katika mfumo wa Kisasa wa Teknolojia.
Bwana Thomas Mackay alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo inayokwenda Kitaalamu zaidi imekuwa ikitoa mafunzo katika Mataifa mbali mbali Ulimwenguni na mkakati wao kwa sasa ni kuona fursa hiyo adhimu inawanufaisha Wananchi wa Zanzibar.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wazo la Uongozi wa Kampuni ya VM Ware limekuja wakati ambao Zanzibar imeshaanza hatua za awali katika kuhakikisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano inawafikia Wananchi walio wengi Mjini na Vijijini.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa inaendelea kujenga miundombinu ya Madarasa ya masomo ya Mtandao wa Teknolojia katika ngazi ya Msingi ili kuwarahisishia ufahamu wa awali Wanafunzi wake wa kujiandaa na Taaluma hiyo waingiapo Elimu ya juu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mfumo wa sasa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano unaotumika Duniani umekuwa ukirahisisha kazi za Mwanaadamu katika harakati zake za Kimaisha na kuifanya Dunia hivi sasa kuwa Kiganja badala ya Kijiji.
Mapema Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Simai Mohamed Said alisema Teknolojoa ya Habari na Mawasiliano inayobadilika kwa kasi Duniani kamwe haiwezi kuiacha nyuma Sekta ya Elimu ambayo ndio mzizi wa Maendeleo yoyote.
Mh. Simai alisema katika kuthamini ujio wa Viongozi hao wa Kampuni ya VM Ware ya Marekani Vikao maalum vimendaliwa vitakavyo washirikisha Watendaji wa Masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Taasisi za Umma na zile Binafsi kujadili fursa zitakazopatikana kutokana na ujio huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.