Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Afanya Ziara Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Muwekezaji Mzalendo ambae pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Al- Zara Agriculture Bwana Ahmed Saleh Mbarouk  akimpatia maelezo Balozi Seif juu ya mradi wao wa Kilimo cha Biashara katika shamba lao liliopo Kirombero.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimaliza ziara yake Mkoa wa Kaskazini kwa kukagua Nyumba zinazojengwa kwa ajili ya Wananchi wa Kijiji cha Dundua walioamua kupisha mradi mkubwa wa ujenzi wa Gati ya Mafuta na Gesi huko Mangapwani.

Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mpango wa Kuanzisha Shirika au Kampuni ya Ujenzi itakayovishirikisha Vikosi vyake vya Ulinzi ili kupunguza gharama katika masuala ya Ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Umma Nchini.
Alisema tabia iliyozoeleka ya kuyatumia Makampuni pamoja na Washauri elekezi wa nje ya Nchi katika kusimamia Majengo ya Taasisi za Serikali unapaswa kuepukwa kwa vile unasababisha kutumia gharama kubwa ambazo wakati mwengine zinaweza kutumika katika ujenzi wa majengo mengi zaidi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo akimalizia ziara yake Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kukagua Miradi ya Maendeleo na kuangalia changamoto zinazowakwaza Wananchi akimalizia Wilaya ya Kaskazini “B” kwa kuanzia ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Wananchi wa Kijiji cha Dundua walioamua kupisha Mradi Mkubwa wa Ujenzi wa Bandari huko Mwangapwani.
Alisema upo ushahidi wa wazi  unaoshuhudiwa na Serikali pamoja na Watendaji wa Taasisi za Umma wa jinsi Vikosi vya SMZ vinavyowajibika vyema wakati vinapopewa tenda za ujenzi wa Majengo ya Taasisi mbali mbali ambapo umefika wakati nguvu zao zikaunganishwa pamoja ili kuleta tija na faida zaidi.
Balozi Seif  alisema Wahandisi wa Vikosi hivyo vya Mafunzo, KMKM  na JKU wanastahiki kupongezwa kwa Uzalendo wao uliopelekea kuanza kuaminika wakatui wanapokabidhiwa kazi za Ujenzi pale inapofikia wakati Serikali au Taasisi za Umma na hata Binafsi zinapohitaji huduma hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru Wananchi wa Kijiji cha Dundua kwa mapenzi yao ya kuiridhia Serikali Kuu  kwa kupisha Mradi Mkubwa wa Ujenzi wa Gati ya Mafuta na Gesi kwenye Makaazi yao ambapo kwa kitendo hicho ndipo Serikali ilipoamuwa kuwajengea Nyumba za Kudumu katika Kijiji cha Gongoni.
Alisema Serikali iliamua kujenga Nyumba za kudumu badala ya kuwapa Fedha kama fidia ambazo hatma yake zingeishia katika matumizi mengine ya kawaida na kuziacha Familia za Wananchi wao kusambaratika bila ya kuwa na Makaazi ya Kudumu.
Balozi Seif  alisisitiza kwamba Wananchi hao wa Dundua ambao baadae watahamia katika Makaazi yao mapya  yaliyopo Kijiji cha Gongoni wameanza safari ndefu ya Maendeleo kwa vile eneo  lao limeshaingizwa ndani ya Mipango Miji itakayokiwezesha Kijiji hicho kuwa Mji Mdogo.
“ Wananchi mnapaswa kutokuwa na wasi wasi wowote  kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote inawajali Raia wake wote katika kuimarisha ustawi wao”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Wananchi wa Dundua Mhandisi Hawa Natepe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi huo unahusisha Nyumba 31 zinazosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti na usimamizi wa Mafuta {ZURA}.
Bibi Hawa alisema Nyumba hizo zinazojengwa kwa pamoja na Vikosi vya Mafunzo na KMKM vikitanguliwa na JKU kwa ufyatuaji wa Matofali ya Nyumba hizo zitakuwa na Vyumba Vitano kwa Nyumba 29 na Vyumba Vitatu kwa Nyumba Mbili.
Alisema ujenzi huo kwa awamu ya kwanza tayari umeshafikia asilimia 65% ambazo kwa sasa kazi ya uwezekaji inaendelea vyema licha ya changamoto ya upatikanaji wa Kifusi kuweka sawa Vyumba vya Nyumba hizo.
Alieleza kwamba Awamu ya Pili ya Mradi huo wa Ujenzi wa Nyumba za Wananchi wa Dundua inatarajia kuhusisha ujenzi wa Msikiti, Soko, Kituo cha Afya pamoja na uwekwaji wa mahitaji muhimu ya Kibinaadamu kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu Wananchi hao.
Akikagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Tangi la Kuhifadhia Maji safi na salama katika Kijiji cha Kitope uliofikia asilimia 40%, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alisema Serikali ina hamu kuona kwamba Mradi huo wa maji unamalizika kwa wakati ili kutoa huduma kama ulivyokusudiwa.
Balozi Seif alisema Sera ya Chama cha Mapinduzi iliyonadiwa kwa Wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi wa Mwaka 2015 – 2020 na hatimae kupata ridhaa ya kuongoza Dola Nchini Tanzania Bara na Zanzibar  iliweka wazi umuhimu wa wa Serikali kuwahudumia Wananchi katika upatikanaji wa Maji safi na salama sehemu zote Mijini na Vijijini.
Aliwataka wahandisi na wasimamizi wa Mradi huo muhimu kwa ustawi wa Jamii kuhakikisha kwamba kipindi kilichopangwa kumalizika ujenzi wake  kinazingatiwa vyema ili kuwapa moyo mkubwa Wafadhili waliojitolewa kugharamia ujenzi wa Mradi huo.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  pia alipata wasaa wa kulikagua shamba  la Muwekezaji Mzalendo la Kampuni ya Al- Zara Agriculture liliopo katika Kijiji cha Kirombero linalotarajiwa kujishughulisha na kilimo cha Biashara.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bwana Ahmed Saleh Mbarouk alimueleza Balozi Seif  kwamba mradi wao umechelewa kuanza kama ulivyokusudiwa kutokana na changamoto kadhaa zinazotokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu zinazopaswa kupata baraka kutoka kwa baadhi ya Taasisi.
Hata hivyo Bwana Ahmed alimuhakikishia Balozi Seif  kwamba  taratibu hizo zitakapokamilika Mradi huo wa Kilimo unaweza  kuanza ndani ya kipindi kifupi kisichozidi miezi Mitatu na kutoa ajira kwa Wakaazi wanaolizunguuka eneo hilo wasiopungua Mia Mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Wilaya ya Kaskazini “B” pamoja na Mkoa mzima wa Kaskazini Unguja kufuatilia changamoto hizo na kutafuta mbinu zitakazosaidia  kuanza kwa mradi huo ulioshindwa kuanza kazi zake kwa kipindi cha Miaka Tisa sasa.
Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Wananchi wa Dundua Mhandisi Hawa Natepe akimpatia maelezo Balozi Seif hatua iliyofikiwa ya Ujenzi wa Nyumba hizo.
Harakati za Ujenzi wa Tangi la Kuhifadhia Maji safi na salama katika Kijiji cha Kitope linakalosambaza Maji katika Vijiji vya Kitope Mbaleni na Vijiji jirani lililokaguliwa na Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Kaskazini B wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kujua changamoto zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.