Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Uongozi wa TASAF

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akibadilishana mawazo na Uongozi wa Juu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman.Khamis.OMPR.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Awamu ya 3 kipindi cha Pili umejikita zaidi kufanya kazi na walengwa katika masuala ya uimarishaji wa Elimu, Afya, pamoja na mafao kwa Walemavu waliomo ndani ya Kaya Maskini kupitia Shehia mbali mbali Unguja na Pemba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo Nd. Ladislas Mwamanga alisema hayo wakati akitoa Taarifa ya matayarisho ya kuanza kwa Awamu hiyo katika Kikao cha Wakurugenzi na Maafisa wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mkutano uliofanyika Vuga Mjini Zanzibar.
Ndugu Ladislas Mwamanga alisema Awamu ya Tatu kipindi cha Pili ambayo Fedha za Mfuko huo jumla ya shilingi Trilioni 2.1 sawa na Dola za Kimarekani Milioni 880 zimeshatiwa saini inategemewa kuwafikia Wananchi wote katika Vijiji mbali mbali hadi vile visivyopata huduma ya Tasaf na Awamu zilizopita.
Alisema Uongozi wa Tasaf  utasimamia vyema miradi yote iliyopendekezwa na Wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mabwawa ya kufugia Samaki pamoja na Miundombinu ya Umwagiliaji Maji kwenye Mashamba ya Wana Tasaf kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} aliwahakikishia Wakurugenzi na Waratibu hao wa Tasaf wa Zanzibar kwamba mafao yote yanayolalamikiwa katika kipindi cha nyuma yatalipwa mapema kabla ya muendelezo wa Awamu ya kipindi cha Pili kuanza rasmi.
Nd. Mwamanga alifahamisha kwamba yapo mabadiliko ya muundo mzima wa Tasaf Awamu ijayo yatakayozingatia zaidi maboresho ya shughuli za mfuko huo ili miradi yake iweze kufanya kazi kwa ufanisi kupitia mfumo wa kisasa wa Mtandao wa mawasiliano katika kutanua wigo wa maendeleo ya Kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} alielezea faraja yake kutokana na mafanikio makubwa ya Awamu zilizopita za Mfuko huo zilizowezesha Wanafunzi Mia 277 wa Kaya Maskini Zanzibar kupata mikopo iliyowawezesha kuendelea na masomo yao ya Vyuo Vikuu.
Wakitoa michango yao katika Kikao hicho cha matayarisho ya kuanza kwa Awamu ya Tatu sehemu ya Pili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Wajumbe wa Kikao hicho walisema Tasaf Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili inapaswa kutoa upendeleo zaidi kwa Wananchi wenye mahitaji maalum ili kuwapunguzia utegemezi.
Wajumbe hao pia wakaelezea changamoto zinazowakumba Watendaji wa Mfuko huo  ambazo zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi wakizitaja kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa Taarifa, udanganyifu kwa baadhi ya Watendaji pamoja na ufinyu wa Elimu kwa Walengwa.
Akitoa nasaha zake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed aliushukuru Uongozi Mzima wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} kwa jitihada zake za kuunga mkono Miradi ya Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini.
Waziri Aboud aliwakumbusha Viongozi na Watendaji wanaosimamia Mfuko huo kuangalia zaidi uimarishaji wa Miradi ya maendeleo hasa katika Sekta ya Elimu, na Kilimo ambayo inasaidia kukwamua Kaya Maskini katika kujiletea maendeleo yao.
Katika Kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alimkabidhi rasmi Uenyekiti wa Kamati ya Mfumo wa Tasaf Unguja Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Hassan Khatib Hassan.
Mapema asubuhi Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Nd. Ladislas Mwamanga alikutana kwa mazungumzo ya kubadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Balozi Seif aliwapongeza Viongozi wa Mfumo wa Tasaf kutokana na kazi nzuri wanayoifanya hususan kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuendeleza kuwatumikia Wananchi ili waweze kujikomboa Kiuchumi.
Aliwataka na kuwashauri Watumishi hao wa Tasaf waendelee kutoa Elimu kwa Wananchi kutokana na faida zinazopatikana kupitia miradi na mafao ya Tasaf katika kusukuma gurudumu la Maendeleo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza ufuatiliaji wa Taarifa sahihi za Wananchi ili kuhakikisha kila mstahiki anapatiwa fursa hiyo na kuitumia ipasavyo.
Nao Wananchi kwa upande wao wanapaswa kutoa taarifa zilizo sahihi kupitia Sheha wa Shehia zao ili ziweze kusaidia katika ugawaji wa mafao ndani ya Kaya zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.