Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Afunguzi wa Mkutano Maalum wa Kimataifa wa Wawakilishi wa Shirika la (WFP)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akibadilishana mawazo na Wakuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani {WFP} mara baada ya kuufungua Mkutano wa Wawakilishi wa Shirika Hilo Kanda ya Kusini mwa Bara la Afrika.Wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa  Shirika la Mpango wa Chakula Duniani {WFP} Kanda ya Kusini mwa Bara la Afrika Bwana Michael Danford na wa kwanza Kulia ni Mkurugenzi Kanda wa WFP Bibi Margaret Malu.

Na.Othman Khamis.OMPR. 
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani {WFP} Bado litaendelea kubeba dhima ya kuhakikisha Jamii za Walimwengu zinaishi katika mazingira yatayowawezesha kuwa na Afya bora katika maisha yao ya kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo akitoa baraka zake wakati akiufungua Mkutano Maalum wa Kimataifa wa Siku Nne uliowakutanisha Wawakilishi wa Shirika hilo la {WFP} wa Kanda ya Mataifa ya Kusini na Kaskazini mwa Bara la Afrika pamoja na Mashariki ya Kati.
Mkutano huo unaopokea Ripoti za Majukumu ya Wawakilishi wa Kanda hizo kwa Mwaka na kupanga Mikakati ya uwajibikaji kwa Mwaka ujao ulifanyika katika Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Kama Wilaya ya Magharibi “A”.
Balozi Seif Ali Iddi alisema bado yapo Mataifa Mengi Duniani Wananchi wake wanaendelea kukumbwa na lishe Duni inayosababishwa na uwepo wa Wakimbizi kutokana na vita, Ukame, Mafuriko pamoja na Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoiathiri pia Dunia Kimazingira.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitolea mfano hai wa matukio ya mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyoukumba Ukanda wa Bara la Afrika kwa mujibu wa Repoti za Shirika hilo ya Mwaka 2018/2019 ambao umebainisha uwepo wa uzalishaji mdogo wa chakula katika sekta ya kilimo.
Alisema hitilafu hiyo iliyotokana na upungufu wa uzalishaji wa mazao umepelekea Watoto wadogo kukumbwa na lishe duni inayoathiri Maendeleo ya Bara zima la Afrika kutokana na upungufu wa Chakula unaowakumba zaidi ya Watu Milioni Mia Mbili na Ishirini.
Akizungumzia uwajibikaji wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikakati yake ya kuimarisha ustawi wa lishe bora, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema upo ushirikiano mwema kati ya Tanzania na WFP katika kuona lishe bora inatengamaa.
Alisema Shirika la Mpango wa Chakula Duniani  bado linaendelea kuiunga mkono Tanzania katika kuwapatia Wananchi wake mafunzo ya Elimu ya lishe bora, kusaidia moja kwa moja Wakulima Wadogo sambamba na huduma za usafiri zinazosaidia kurahisisha mfumo mzima wa muelekeo wa kukua zaidi kwa Uchumi wa Taifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi mzima wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani {WFP} kwa uamuzi wake wa busara ulioamua Wawakilishi wake wa Kanda ya Kusini mwa Bara la Afrika kukutana Zanzibar kitendo ambacho kitatoa nafasi kwa Zanzibar kufaidika na matunda ya Shirika hilo.
Mapema Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani {WFP} Kanda ya Bara la Afrika Bwana Michael Danford alisema Shirika hilo limependekeza kuanzisha Miradi Mitatu Visiwani Zanzibar itakayosaidia kusukuma mbele masuala ya Ustawi wa Wananchi.
Bwana Danford alisema uamuzi huo wa Shirika hilo  umekuja kufuatia mchango mkubwa uliotolewa na Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimwa Samia Suluhu Hassan wakati alipokuwa Kiongozi wa ngazi ya juu ya Shirika hilo miaka ya nyuma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.