Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,
akimsikiliza mgeni wake (kulia) Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu
na Watu.Mhe. Jaji Sylvain Ore, akiwa na Ujumbe wake wa Majaji, walipofika Ikulu
Zanzibar kwa mazungumzo leo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Zanzibar imeweza kupiga hatua kiuchumi, kijamii
na kisiasa kutokana na ushirikiano wa Mihimili yake mikuu mitatu ambayo ni Serikali,
Mahakama na Baraza la Wawakilishi.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazunguzo na Rais wa Mahakama ya Afrika ya
Haki za Binaadamu na Watu Jaji Sylvain Ore aliyefika Ikulu mjini Zanzibar akiwa
amefuatana na ujumbe wa Majaji wa Mahakama hiyo.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imeweza kupiga hatua kwa kiasi
kikubwa hali ambayo imepelekea kukuza na kuimarisha amani na utulivu na umoja uliopo kutokana na mashirikiano mazuri wa mihimili
hiyo.
Rais Dk. Shein
alimueleza Rais huyo wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu kuwa mafanikio
hayo makubwa ya kimaendeleo yameweza kufikiwa hapa Zanzibar kutokana na mihimili
hiyo mitatu mikubwa kutoingiliana katika kazi zao na badala yake kuweza
kushirikiana pamoja.
Alieleza kuwa kila
muhimili kati ya mihimili hiyo mitatu mikuu ya Zanzibar imekuwa ikifanya kazi
zake bila ya kuingiliwa na muhimili mwengine hatua ambayo imezidisha
mashirikiano na kuendelea kuipa sifa kubwa Zanzibar ndani na nje ya nchi.
Rais Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo pamoja na ujumbe wake kuwa kipaumbele kikubwa
kilishowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha amani, utulivu
na umoja uliopo vinadumishwa na kuendelezwa kwa nguvu zote ikiwa ni pamoja na
kutekeleza azma ya Dira ya 2020.
Aliongeza kuwa
Zanzibar imeweza kupata mafanikio katika kutilia mkazo suala zima la haki za
binaadamu na watu hali ambayo imepelekea Zanzibar kuimarika kiuchumi, kijamii
na kisiasa.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Mahakama hiyo na kupongeza wazo zuri la
kuja kufanya mkutano wao hapa Zanzibar hasa kwa kutambua kuwa Zanzibar ni
sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Dk. Shein aliwakaribisha
viongozi hao Zanzibar na kuwaeleza kuwa Zanzibar iko salama na hivi sasa
inaendelea kuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka pande zote za dunia.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliwaeleza viongozi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea
kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wanaotaka kuja kuekeza Zanzibar.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Mahakama hiyo Sylvain Ore kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu huku akimtakia yeye pamoja na ujumbe
wake mkutano mwema ulioanza Novemba 4 hadi 29 na ule utakaoanza Disemba 2 hadi
Disemba 6.
Sambamba na hayo,
alimkaribisha Zanzibar yeye na ujumbe wake na kuwataka kuitembelea Zanzibar
kwani ina vivutio vingi vikiwemo vile vya kitalii.
Nae Rais wa Mahakama
ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu Jaji Sylvain Ore alimpongeza Rais Dk.
Shein kwa mafanikio makubwa yaliopatikana Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuweko
mazingira mazuri ya amani,utulivu pamoja na misingi ya sheria na haki za
binaadamu.
Jaji Ore alieleza kuwa
Zanzibar ni sehemu ambayo imekuwa ikiwavutia watu wengi kuja kuitembelea
kutokana na vivutio vingi vilivyopo lakini kivutio kimoja wapo kikubwa ni
kuwepo kwa amani na utulivu.
Sambamba na hayo,
kiongozi huyo alipongeza hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa Zanzibar na
kusisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na kufuata misingi ya Haki za
Binaadamu na Utawala Bora.
Alieleza kuwa Mahakama
ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu yenye Makamo Makuu yake Arusha nchini
Tanzania imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuhakikisha inatekeleza vyema
matakwa kwa nchi za Umoja wa Afrika (AU).
Aliongeza kuwa
mahakama hiyo imeweza kufanikiwa katika kuendesha programu mbali mbali
zinazolenga kutoa elimu ya uwepo wake pamoja na shughuli zake katika nchi mbali
mbali za bara la Afrika.
Kiongozi huyo alieleza
kuwa uwepo wao hapa Zanzibar unaenda sambamba na vikao mbali mbali vya Mahakama
hiyo ikiwa ni pamoja na Kikao cha 10 cha dharura cha mahakama hiyo
kitakachoanza Disemba 2 hadi Disemba 6 mwaka huu.
Pamoja na hayo,
viongozi hao wanatarajiwa kuwa na kikao ambacho kitatoa elimu juu ya uendeshaji
wa mahakama na utoaji wa hukumu zikiwemo hukumu za wazi kikao kitakachowahusisha
Mawakili na Majaji mbali mbali ambapo pia, wananchi nao watapata fursa ya
kushiriki na kutoa maoni yao pamoja na changamoto walizonazo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
No comments:
Post a Comment