Habari za Punde

Kamati za Utalii za Wilaya Kupatiwa Elimu ya Utalii

Na Ali Issa Maelezo 7/11/2019
Kamati ya kudumu ya Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi  imeitaka Kamisheni ya Utalii  kuzipatia elimu ya kutosha kamati za wilaya za utalii ili kufikia dhana nzima ya utalii kwa wote nchini.
Akizungumza na Kamati za Wilaya za Utalii huko katika Ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Mwenyekiti wa kamati hiyo Mwantatu Mbaraka Khamis, amesema kamati hizo zikipatiwa elimu ya kutosha zitaweza kufanyakazi kwa ufanisi na kutekeleza vyema majukumu yao.
Amesema kumekuwa na changomoto mbalimbalii zinazoikumba dhana nzima ya utalii kwa wote hivyo ni vyema kamati hizo kupatiwa mafunzo na kuelimisha jamii ili kufikia lengo lililokusudiwa.
“Fursa hii ya elimu itaufanya utalii kwa wote kuweza kufaidika wananchi wazawa kwani kamati zitaweza kufanya kazi kwa weledi na kuweza kutatua changamoto zilizopo”,alieleza Mwenyekiti huyo.
Nao wajumbe wa kamati za Wilaya wamesema  kamati zao zitafanya kazi kwa kuangalia maslahi ya wazanzibar na serikali kwa ujumla ili kufikia dhana ya utalii kwa wote na sio kuwanufaisha zaidi wageni kuliko wazawa.
Aidha wameomba kupatiwa mashirikiano na taasisi nyengine pamoja na wananchi ili kuweza kudhibiti biashara haramu katika fukwe, kulinda Mila, silka na Utamaduni wa Mzanzibari pamoja na maeneo ya kihistoria yasiharibiwe kwa lengo la kuongeza pato  nchini.
Mapema Katibu Mtendaji Kamisheni ya Utalii Abdalla Muhamed Juma amesema Kamati za Wilaya zitashirikiana na Kamisheni kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo ya utalii ndani ya wilaya.
Aidha Katibu Mtendaji huyo alisema kamati hizo zitakuwa na majukumu ya kuimarisha dhana ya utalii kwa wote, kudhibiti usalama na amani kwa wageni na wenyeji wa maeneo ya utalii, kuazisha mfumo wa fedha wa jamii kwa kutoa asilimia moja ya pato la muekezaji ambazo zitatumika kwa maendeleo ya vijiji.  
Alisema pia kamati hizo zitakuwa na jukumu la kulinda na kudumisha utamaduni za asili kama bidhaa ya utalii na kuthibiti thamani,maadili katika wilaya kudhibiti pamoja na kuunga mkono jumuiya za kiraia zinazofanya shughuli za utalii kwa kuzisaidia kwa kujishuhulisha katika mipango yao kwa kushirikiana na kamisheni na wadau wengine wa utalii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.