Habari za Punde

Waziri Dkt. Kigwangala ahitimisha Tamasha la Urithi Wetu


Mgeni Rasmi ambaye pia ni Waziri wa Mali asili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa kwaya ya Mt. Benedict kutoka Parokia ya Bugando jijini Mwanza Leonidas Kabagambi (aliyevaa shati jeupe) mfano wa ufunguo wa gari inayojulikana kama “Kirikuu”mara baada ya kuibuka washindi wakati wa kufunga Tamasha la Urithi Wetu kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.



Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mwanza.
Serikali imewataka waandaaji wa Tamasha la Urithi Wetu kuwa wabunifu kwa kuongeza michezo mbalimbali ya jadi ambayo itasaidia kukuza kazi za sanaa na utamaduni wa Mtanzania ili kukuza fursa za utalii na kuwaongezea wananchi kipato.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mali Asili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala leo jijini Mwanza wakati wa kufunga Tamasha la Urithi Wetu kwa naiaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.

“Nimepita kila mabanda, wananchi wamepata fursa ya kutangaza kazi zao mbalimbali za kiuchumi zinazowasaidia kukuza kipato chao na uchumi wa taifa kwa ujumla. Rais Dkt. John Pombe Magufuli yupo mstari wa mbele katika kuinua na kusimamia utamaduni wetu” alisema Dkt. Hamis Kigwangala.

Dkt. Kigwangala amesisistiza kuwa Tanzania inafursa nyingi za kiutamaduni ambapo amebainisha kuwa ni nchi pekee barani Afrika inayojumuisha zaidi ya makabila 128 ambayo yapo kwenye makundi makuu manne ya makabila yanayopatikana Afrika yanayojulikana kama Wakushi, Khoisan, Wabantu na Waniloti.

Aidha, Dkt. Kigwangala alibainisha kuwa tamasha la urithi wetu lina lengo la kuendeleza falsafa ya nchi yetu ambayo Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kulinda utamaduni wa Mtanzania.

Ili kulifaya tamasha la urithi liwe endelevu, Dkt. Kigwangala amesema kuwa ni lazima wananchi wawe na furaha ambapo tamasha hilo linaongeza hamasa katika michezo, sanaa na utamaduni hatua itakayowapelekea wananchi wawe wabunifu, wenye furaha na wenye mawazo mazuri yanayowashirikisha wadau wote wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Watanzania wanahaki ya kumshukuru Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ambapo mara baada ya kupata uhuru Desemba 9, 1961 alikuwa mstari wa mbele katika kusimamia utamaduni wa Mtanzania.

Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwl. Nyerere Waziri Dkt. Mwakyembe alisema “‘Taifa lisilo na utamaduni wake, ni taifa mfu.’ Watanzania tumeamka, tamasha hili linatukumbusha tujitambue sisi ni akina nani. Namshukuru Mungu tumejitambua ndio maana nawashukuru wana Mwanza, wizara zetu za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Mali Asili na Utalii kwa kurejesha na kusimamia tamasha hili linalotukumbusha sisi ni ni Watanzania, tujivunie Uafrika wetu.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela amesisitiza kuwa Mwanza ndio kitovu cha nchi za maziwa makuu ambapo kuna mfanano wa mambo ya kijiografia yanayoifanya Mwanza kuwa katikati ya nchi za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Hii ni sifa inayoifanya mkoa huo kuendelea kuwa mwenyeji wa tamasha la utithi wetu.

Jiografia hiyo inaipa mwanza nafasi kubwa zaidi ambayo itatoa fursa kwa nchi zote za Afrika mashariki kushiriki katika tamasha hili kwa ufanisi zaidi ambapo Mkuu huyo wa mkoa amewahakikishia washiriki wote ulinzi na usalama wakati wa tamashaha hilo mwakani 2020 ambalo litafanyikia tena jijini Mwanza.

Tamasha la Urithi wetu lilianza Oktoba 31 na kuhitimishwa Novemba 02 ambapo liliongozwa na kauli mbiu “Urithi wetu, Fahari yetu. Tamasha hilo lilpambwa na kushereheshwa kwa michezo mbalimbali ikiwemo ngoma za asili, kwaya, mbio za baiskeli, mbio za mitumbwi pamoja na mchezo wa bao. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.