Na.Mwandishi Wetu
Serikali imewahakikishia
wadau kuwa iko tayari kuendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika uandaaji
wa takwimu bora za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Mtakwimu Mkuu wa
Serikali Dkt. Albina Chuwa alieleza hayo wakati alipokuwa akifungua warsha ya
siku moja ya kuhariri Ripoti ya Kitaifa ya Takwimu za Mabadiliko ya Tabianchi
ya mwaka 2019 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) jijini Dodoma.
Warasha hiyo ambayo
iliratibiwa na kufadhiliwa na Ushirikiano wa Kimataifa wa Takwimu kwa Maendeleo
Endelevu (GPSDD),
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Serikali ya Ujerumani (GIZ) ilijumuisha
Wadau wa takwimu za mabadiliko ya tabianchi wa ndani na nje.
Katika hotuba yake ambayo
ilisomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Utawala na Masoko Andrew
Ulindula, Mtakwimu Mkuu wa Serikali alisifu ushirikiaono mzuri uliopo kati ya
NBS na wadau wa takwimu na kueleza kuwa Ripoti ya kwanza ya Takwimu za
mabadiliko ya tabianchi ya mwaka 2019 ni miongoni mwa matokeo ya ushirikiano
huo.
“Ushirikinao huu ni
dhahiri kuwa unaunga mkono jitihada na mipango mbalimbali ya Serikali ya usimamizi
wa hifadhi ya mazingiza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi” alieleza
Dkt. Chuwa.
Alibanisha kuwa pamoja na
ripoti hiyo kuwa ni ya kwanza kutolewa nchini lakini ni ya aina yake kwa kuwa
imeandaliwa kwa kutumia takwimu za
kiutawala kama chanzo kikuu cha takwimu hizo.
Dkt.
Chuwa alifafanua kuwa Takwimu za Kiutawala zimetawanyika kwenye Wizara,
idara na Wakala mbalimbali za Serikali
na kwa wadau wengine nje ya Serikali hivyo huleta ugumu kwa watumiaji kuzipata
kwa urahisi na kwa wakati.
“Hali
hii huleta ugumu wa kufanya uchambuzi wa hali ya mazingira kwa kipindi cha muda
mrefu, uchambuzi ambao ni muhimu ili kuweza kubaini picha halisi ya mwenendo wa
mabadiliko ya kimazingira hasa mabadiliko ya tabianchi” Dkt. Chuwa alisema.
Kwa
hivyo, kukamilika kwa ripoti hii kutawarahisishia watumiaji wa takwimu ikiwemo
serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuzipata kwa wakati na utimilifu
wake.
Mtakwimu
Mkuu wa Serikali aliwataka washiriki wote kuhakikisha kuwa
wanaijadili ripoti hiyo kwa kina ili iwe na ubora unaokusudiwa na kukidhi
matumizi ya wadau mbalimbali kwenye upangaji, ufuatiliaji na ufanyaji tathmini ya mipango mbalimbali ya
hifadhi ya mazingira nchini, hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
na athari zake.
Akizungumza kwenye
warsha hiyo mwalikilishi wa UNEP kutoka Ofisi ya Nairobi Bi. Diana Ngina alieleza
kuwa Ofisi yake imetiwa moyo sana na Tanzania kupitia NBS kwa namna ilivyo
mstari wa mbele katika kuandaa Takwimu za mazingira na mabadiliko ya tabianchi hivyo
kuziba pengo lililopo ya Takwimu za aina hiyo.
“Ripoti hii iwe
mwanzo mzuri… iwe mfano wa nchi nyingine kujifunza kutoka kwenu ili nao
watamani kufikia pale Tanzania ilipofikia”
alieleza Diana na kuipongeza NBS kwa kutoa ripoti hiyo na kuitaka kuendelea
na ari hiyo hiyo ili kutoa ripoti nyingi za aina hiyo.
Kwa upande wake,
mwakilishi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Takwimu kwa Maendeleo
Endelevu Karen Bett alisema taasisi yao imefarijika kuona Tanzania imeweza
kutoa ripoti hiyo kwa kutumia vyanzo vya takwimu za kiutawala.
“Kwa
kuweza kutoa ripoti hii maridhawa kwa kutumia vyanzo vya takwimu za kiutawala
inadhihirisha umuhimu wa takwimu za kiutawala katika kuzalisha takwimu rasmi.
Kilicho muhimu ni Takwimu hizo sasa kutumika katika kupanga sera na mipango yetu
kuboresha hali za maisha ya watu wetu ambao wengi wanakumbana na athari za
mabadiliko ya tabianchi” alisisitiza Karen.
No comments:
Post a Comment