Habari za Punde

Jaji Mwaimu atembelea ofisi za THBUB Zanzibar

Mwenyekiti wa (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiongea na wafanyakazi wa tume pamoja na wageni wengine waliohudhuria hafla fupi. 

Na. Mbaraka Kambona,
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ametembelea ofisi za taasisi hiyo zilizopo visiwani Zanzibar, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipokabidhiwa  dhamana hiyo Novemba 4, 2019.

Jaji Mwaimu alifanya ziara hiyo mapema leo (Novemba 30, 2019) kwa lengo la kutambuana na wafanyakazi wa tume waliopo katika ofisi hizo zilizopo Mbweni, visiwani Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Jaji Mwaimu akiongozana na Makamishna na viongozi wengine wa tume alifanya ukaguzi wa ofisi hizo ambazo hivi karibuni zilifanyiwa ukarabati mkubwa kwa lengo la kuziboresha.  

Akiongea baada ya kumaliza ukaguzi wa jengo hilo, Jaji Mwaimu alieleza kuridhishwa kwake na ukarabati huo uliofanyika, na kusema kuwa watajipanga vizuri katika majukumu yao ili kuhakikisha wanazitumia vizuri  ofisi zote mbili za Tanzania bara na hizo za visiwani ili kutatua kero za  wananchi.

Aidha, Jaji Mwaimu aliwashukuru Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) kwa ufadhili wao ambao umewezesha kufanikisha ukarabati huo.

Katika ziara hiyo Jaji Mwaimu aliambatana na viongozi wafuatao; Makamu Mwenyekiti, Mohamed  Khamis Hamad, Mheshimiwa, Dkt. Fatma Rashid Khalfan, Mheshimiwa Thomas Masanja,  Mheshimiwa Amina Talib Ali, Mheshimiwa Khatib Mwinyi Chande  na Mheshimiwa Nyanda Josiah Shuli.
Jaji Mwaimu (kushoto) akiongea na Kamishna Mkaazi wa tume visiwani Zanzibar, Khatib Mwinyichande wakati wakikagua ofisi hizo za tume. 
Afisa Mfawidhi wa  tume Zanzibar, Hussein Mbarouk akimuonesha kitu Mwenyekiti (wa kwanza kushoto) wakati wa ukaguzi wa jengo hilo.

Mwenyekiti wa (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (aliyeinama) akiwaongoza viongozi wengine wa tume kuwatunza waburudishaji wa kikundi cha ngoma ya kibati kutoka Zanzibar katika hiyo hafla fupi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.