Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza (wa
kwanza kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Ndaki ya Sayansi na Elimu Kampasi ya
Solomon Mahlangu Prof. Allen Malisa akiwa kwenye ziara ya kikazi siku mbili
alipotembelea eneo la Mazibu Morogoro lililotumiwa na wapigania uhuru wa
“African National Congress” (ANC) wa Afrika ya Kusini.
Na. Eleuteri Mangi, WHUSM Morogoro
Serikali inawahimiza wadau
na jamii nzima kutunza, kulinda na kuhifadhi maeneo ya kihistoria ambayo
yalitumika wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ili
historia hiyo isipotee na iweze kutumika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza alisema hayo jana mkoani wakati
akiwa kwenye ziara ya kikazi siku mbili alipotembelea maeneo Dakawa na Mazibu
yaliyotumiwa wapigania uhuru wa “African National Congress” (ANC) wa Afrika
Kusini.
“Kazi ya kulinda, kuhifadhi
na kuendeleza urithi wa Ukombozi wa Afrika uliopo Tanzania ni jukumu la jamii
nzima, mashirika ya umma na watu binafsi ili kuthamini na kuenzi urithi huu
muhimu wa Afrika” alisema Naibu Waziri Shonza.
Ili kutunza na kuhifadhi
maeneo, nyaraka, vifaa na vielelezo vingine vilivyotumiwa na Wapigania uhuru,
Serikali kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeanzisha
Programu ya uhifadhi na uendelezaji wa historia ya Ukombozi wa Afrika ambayo
pamoja na mambo mengine;inalenga kuthamini na kuenzi mchango wa Tanzania katika
kuongoza harakati za mapambano ya kudai uhuru.
“Tunawashukuru sana wenzetu
wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kutumia na kuhifadhi
maeneo haya, tumeona pamoja na kwamba yalitumika katika harakati za ukombozi,
lakini kimsingi miundombinu mikubwa imebaki ikiwemo shule za msingi na
sekondari, zahanati pamoja na vyuo katika maeneo yote ya Dakawa na Mazimbu
ambayo yanaendelea kuhifadhiwa na kutumika ili kuhakikisha historia hii
haipotei” alisema Naibu Waziri Shonza.
Aidha, aliwasisitiza na
kuwahimiza Watanzania kutumia fursa ya kuwepo kwa utajiri huo wa kihistoria kwa
kuya tembelea maeneo hayo wakiwemo wanafunzi wa ngazi za shule ya msingi,
sekondari, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu ili kujifunza historia hiyo sio tu
kwa nadharia, bali kwa kujionea maeneo halisi pamoja na vifaa vilivyotumiwa na
wapaingania uhuru hao.
Kwa upande wa eneo la
Dakawa, upo utajiri mkubwa wa kihistoria ambao una manufaa kwa vijana na Watanzania
kwa ujumla. Eneo hilo lina taasisi tano ambazo zinatumika hadi sasa
ikijumuisha; shule ya msingi na shule ya sekondari ya wasichana Dakawa, chuo cha
VETA, Chuo cha ualimu pamoja na Kituo cha afya.
Naye Mkuu wa Ndaki ya Sayansi
na Elimu Kampasi ya Solomon Mahlangu Prof. Allen Malisa alisema Kampasi hiyo ilianzishwa
mwaka 1978, wakati huo eneo hilo likijulikana kama makazi ya wapigania uhuru wa
ANC wa Afrika ya Kusini.
Wapigania uhuru hao ambao
wengi wao wakiwa ni vijana, walilazimika kukimbia Afrika ya Kusini ili kukwepa
kukamatwa na Utawala wa Makaburu, kufuatia mgomo wa vijana wa Soweto wa mwaka
1976 hatua iliyopelekea vijana wengi kukimbilia Tanzania, ambapo awali
walijikuta wamekuwa wengi kwenye mji wa Dar es Salaam kiasi cha kuhatarisha
usalama baina yao na vijana wazawa.
Katika kutatua tatizo hilo,
mamlaka ya utawala wa wakati huo iliwahamishia wapigania uhuru hao Mkoani
Morogoro, na kwa vile kulikuwepo na haja ya kuwalinda na Makaburu ambao
walikuwa wanafanya kila mbinu kuwatafuta popote walipo, waliwekwa jirani na
kikosi cha jeshi la wananchi cha Mzinga kwa muda. Hatimaye, walihamishiwa eneo
la Mazimbu ambalo liko uwanda wa chini na hivyo kutokuonekana kirahisi kutokea
mjini Morogoro.
Kwa kuwa idadi ya vijana hao
ilikuwa ni kubwa, na kutokana na ugeni katika makazi hayo mapya, hawakuwa na
kazi za kufanya, hivyo kutumia muda mwingi kufundishana; wakubwa wakichukua
nafasi ya ualimu na kuwafundisha wadogo.
Jambo hilo liliporipotiwa
kwa uongozi wa ANC kule Afrika ya Kusini, liliwagusa Viongozi na kufanya
aliyekuwa Rais wa chama, Ndugu Oliva Tambo, kuagiza makazi hayo waliyopewa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ijengwe shule. kwa kutekeleza
maagizo hayo ya ANC, eneo hilo lilijengwa shule iliyojulikana kama “ANC school”
Mazimbu.
Kufuatia kijana aliyekuwa
mpigania uhuru machachari, aliyejulikana kwa jina la Solomon Kalushi Mahlangu,
kukamatwa na kutiwa kizuizini mwaka 1977 na hatimaye kunyongwa hadi kufa mwezi
Aprili 1979, Uongozi wa ANC ulibadilisha jina la Mazimbu “ANC school” kuwa
“Solomon Mahlangu Freedom College”
(SOMAFCO) ili kutambua mchango wa wapigania uhuru wa ANC kwenye kutafuta uhuru.
Naibu Waziri Shonza yupo
katika ziara ya kikazi kutembelea maeneo ya ya historia ya ukombozi wa Afrika
katika mikoa ya Dodoma wilaya ya Kongwa, Morogoro wilaya Kilosa, Manispaa ya
Morogoro pamoja na Mkoa wa Pwani wilaya za Chalinze na Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment