Habari za Punde

NHC YAKUSANYA MILIONI 618.2 KIGOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kigoma Samson Anga (wa pili kulia) kuelekea kuangalia  sehemu ya eneo lililokuwa likimilikiwa na Shirika la National Milling lililopo Kibirizi Kigoma, alipolitembelea jana baada ya kuelezwa kuwepo madai ya udanganyifu kwenye hati ya umiliki wa ardhi katika eneo hilo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua moja ya Jalada la Ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Kigoma jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Dkt Sebastian Siwale na kulia ni Karani wa Masijala ya Ardhi Haiba Mramba.

Na Munir Shemweta, WANMM KIGOMA
Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kigoma limekusanya kiasi cha shilingi 618,246,592 sawa na asilimia 70 ya makusanyo ya mwaka ambapo matarajio ya shirika hilo ilikuwa kukusanya asilimia 50 kufikia Desemba 2019.
Akitoa taarifa ya makusanyo ya kodi kwa miradi ya Shirika lake kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa mwaka 2019/2020 wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wa Kigoma jana, Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Kigoma Ramadhani Sadick alisema Shirika hilo ilipangiwa kukusanya 886,732,105 na kubainisha kuwa ziada iliyopatikana ilitokana na mahusiano mazuri na wateja wake pamoja na huduma bora zinazotolewa.
Kwa mujibu wa Sadick, Shirika la NHC limekuwa likifanya jitihada za dhati kuhakikisha linaboresha mahusiano na wapangaji ili kuhakikisha panakuwepo maridhiano kati ya shirika na wateja wake jambo alilolieleza linasaidia kupunguza migogoro baina ya pande hizo hasa kipindi ambacho ilipaji kodi ulikuwa ukisuasua.
‘’Shirika limekuwa lifanya  mazungumzo na wateja ili kuona namna bora ya kuwasaidia kutekeleza majukumu ya kiupangaji ilhali wakiendelea na biashara zao na tunatoa fursa ya kulipa kodi kwa awamu tofauti na utaratibu uliozoeleka wa kulipa kodi kwa mara moja’’ alisema Sadick.
Akielezea hali ya soko, Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Kigoma, alisema Shirika lake limekuwa likifanya tafiti mara kwa mara ili kuhakikisha bei inazotoza kwenye nyumba za kupanga zinaendana na hali ya soko pamoja na mazingira halisi ya soko la nyumba.
Akigeukia nyumba za kuuza katika mradi wa Mlole, Kaimu Meneja huyo wa NHC mkoa wa Kigoma alisema, Shirika lilijenga nyumba 36 za makazi na nyumba 26 kati ya hizo ziliuzwa huku nyumba 13 zikipangishwa kwa wateja ambao walipewa fursa ya kununua nyumba hizo pale watakapohitaji.
Aidha, alibainisha kuwa, fursa hiyo inatolewa pia kwa mwananchi yeyote anayetaka kununua nyumba zilizopangishwa ambapo mkataba wa upangishaji unatoa fursa kwa mnunuzi asiye mpangaji kununua nyumba yoyote aitakaye.
Kwa upande wale Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka shirika la nyumba la taifa mkoa wa kigoma kuangalia namna bora ya kushirikiana na halmashauri zilizopo nje ya miji katika kujenga nyumba za watimishi badala ya kuangalia halnashauri za mjini pekee.
Alisema, katika kuhakikisha Shirika la Nyumba linajenga nyumba za bei nafuu kwa watumishi katika halmashauri mbalimbali nchini Naibu Waziri Mabula alitaka shirika hilo kukabidhiwa viwanja huku kazi ya kuweka miundombinu na gharama nyingine ikibaki halmashauri husika.
Aidha, amelitaka shirika la nyumba la Taifa kujenga nyumba kwa kuingia makubaliano na halmashauri kulingana na mahitaji au aina ya nyumba inazohitaji ili kuepuka ujenzi wa nyumba zitakazokosa wanunuzi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga (Kushoto) nje ya Ofisi ya Mkuu wa mkoa jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo. 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa baadhi ya nyaraka na Mchunguzi Mwandamizi wa TAKUKURU Kigoma Leonida Mshema kuhusiana na madai ya kuwepo udanganyifu kwenye hati ya ardhi ya umiliki wa eneo lilikuwa likimilikiwa na Shirika la National Milling eneo la Kibirizi Kigoma. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kigoma Samson Anga na kushoto ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Magharibi Thomas Antapa.
(Picha na Wizara ya Ardhi)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.