Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Ndg. Mussa Aboud Jumbe, akitowa maelezo ya michoro ya majengo ya Soko la Samaki na Bandari inayojengwa katika eneo la Malindi Wilaya ya Mjini Unguja.ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika eneo la ujenzi huo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar
imo katika mchakato wa kutekeleza uchumi wa buluu na tayari hatua kubwa zinachukuliwa
kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya uwekaji wa jiwe
la msingi la ujenzi wa soko la samaki na
bandari ya uvuvi linalojengwa huko Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ikiwa
ni shamrashamra za sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Alisema kuwa uchumi wa
buluu ni chochote kiliopo baharini na katika ufukweni wa bahari ambapo tayari
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imenza kushughulikia uchumi huo na haiko
tayari kuachwa nyuma.
Alisema kuwa Zanzibar
inajiandaa na uchumi wa bahari na tayari imeanzisha Kampuni ya uvuvi ya
Zanzibar (ZAFICO), ikiwa ni tayari imeshazindua boti mpya ya uvuvi na nyengine
iko njiani inakuja na boti nyengine nne za uvuvi zimeshatengewa fedha zake huku
akisisitiza kuwa Kampuni hiyo imejiandaa vizuri sana.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Serikali inajenga bandari pamoja na soko huko Malindi ambalo idadi ya
wastani ya watu 6000 watafanya kazi katika eneo hilo la soko jambo ambalo
litaleta tija sana katika sekta ya uvuvi.
Alisema kuwa watu wa
Zanzibar wamezungukwa na bahari lakini bahari hiyo haijatumiwa vizuri na badala
yake wamekwua wakija watu kutoka nje ya nchi na kuwaiba samaki wa Zanzibar
wakiwemo samaki wa jodari.
Alisema kuwa samaki
wakubwa na wazuri wako bahari kuu ambako kufikia huko kunahitajika uwezo wa
vifaa vya kuvulia.
Alisema kuwa
haiwezekani Zanzibar kuwa imezungukwa na bahari lakini haivui samaki ipasavyo
sambamba na kutokuwa na kiwanda hata kimoja cha kusindika samaki.
Rais Dk. Shein
alisisitiza kuwa haiwezekani kuwepo bahari lakini hakuvuliwi hivyo, ni lazima kuimarishwe
uvuvi ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vya kusarifu samaki Unguja na Pemba.
Alisema kuwa historia
ya Zanzibar inaonesha kwamba watu wa Zanzibar walianza kuvua kwanza kuliko
kulima, hivyo uvuvi una historia kubwa hapa Zanzibar na kueleza kuwa histira ya
Zanzibar ni uvuvi.
Alisisitiza kuwa
lazima kuvuliwe kisasa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa bandari, soko pamoja na
vifaa vyengine vya kisasa vya kuvulia samaki.
Uvuvi wa samaki ni
sehemu moja tu katika uchumi wa buluu lakini pia, katika uchumi huo ni vyema
kukawpo maandalizi ya usafiri wa uhakikia wa baharini, boti za kisasa sambamba
na kuwawezesha wavuvi wa hapa nchini.
Uchumi wa bahari pia,
unapaswa katika kuimarisha utalii hali ambayo imekuwa ikishuhudiwa hapa
Zanzibar ambapo watalii wamekuwa wakiingia nchini kwa njia ya anga na baharini.
Aidha, alisisitiza
haja ya kuendeleza bandari za kisasa kama Serikali ilivyoamua kujenga bandari
mpya ya Mpigaduri pamoja na kujenga bandari ya gesi na mafuta huko Mangapwani
na kuyaondosha matangi yote ya mafuta yaliopo Mtoni.
Aliongeza kuwa
Serikali itakapojenga bandari mpya ajira na biashara vyote vitaongezeka kwa
kiasi kikubwa hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina historia ya biashara.
Rais Dk. Shein aliendelea
kuwataka wananchi kuendelea kufanya subira katika kusubiri matokeo ya utafiti
wa mafuta na gesi hapa Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa
ni lazima uvuvi hapa Zanzibar ufanyike kisasa na taratibu zote zifanyike kisasa
ili na wageni pia, wakija kutembea wafurahi na wasiudhike pale watakapotembelea
masoko ya samaki.
Alisisitiza haja ya
kufuga samaki na kueleza hatua za Serikali katika kuimarisha mradi huo ili kila
mwananchi aweze kufuga samaki.
Rais Dk. Shein alitoa
pongezi kwa Serikali ya Japan kwa msaada huo mkubwa ulioutoa kwa Zanzibar na
kuwaahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya na itaweza.
“Zanzibar tunapendwa
sana na rafiki zetu na wanatusaidia kutokanana kodi za wananchi wao na
wanatuletea sisi, hivyo lazima tuwashukuru sana”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein
kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar aliwaahidi Serikali ya Japan pamoja na
Shirika la (JICA) kuwa mradi huo wa soko pamoja na ujenzi wa bandari utatunzwa
na kuenziwa vizuri ili ulete tija kwa wananchi wa Zanzibar.
Mapema Rais Dk. Shein
alifika katika eneo linalotarajiwa kujengwa soko hilo pamoja na bandari huko
katika eneo la Malindi na kupata maelezo juu ya ujenzi huo kutoka kwa
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Mussa Aboud Jumbe.
Nae Waziri wa Kilimo ,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mmanga Mjengo Mjawiri alisema kuwa Wizara
hiyoimeweka utaratibu maaluma wa kufaiutaia miradi yao ilikuhakikisha inamaliza
kwa wakati na inakuwa bora.
Alisema kuwa kila mwisho
wa mwezi wamekuwa wakitembelea miradi hiyo kwa lengo la kufahamu matatizo yaliopo
kwa pande zote na kuahidi kuwa miradi yote inayotekelezwa na Wizara hiyo
itamaliza kwa wakati
Alisema kuwa Serikali
itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wavuvi ili waweze kuvua uvuvi wenye
faida na kipato ili waondokane na uvuvi wa mazoea.
Alisema kuwa tayari
wameshaanza kutoa elimu pamoja na kukutana na Kamati za wavuvi kwa lengo la
kutoa elimu huku akisisitiza kuwa soko la samaki linakuwepo iwapo kutakuwa na
wavuvi na wavuvi wanaweza kuvua iwapo kutakuwa na bahari kwani bahari ndio
makaazi ya samaki.
Hivyo, alisisitiza
haja ya kuyahifadhi na kuyatunza mazingira ya samaki hasa matumbawe na kuachana
kabisa na uvuvi unaochafua bahari na kusisitiza kuwa iwapo wataachana na kadhia
hiyo mafanikio makubwa zaidi yatapatikana.
Alisema kuwa wananchi
wameshaanza kuelewa juu ya uvuvi haramu na tayari wamekuwa wakitoa taarifa kwa
watendaji wa Wizara wakiwemo viongozi na baada ya hapo hatua madhubutizimekwua
zikichukuliwa katikamkupambana na kadhia hiyo ambapo hiyo ni dalili njema ya
kufahamu kuwa wananchi wanaanza kufahamu.
Alisema kuwa Serikali
itaendelea kuweka Sera na taratibu nzuri kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
hali ambayo itapelekea kuongezeka kwa samaki hapa nchini na kutosheleza soko la
utalii huku akieleza azma ya Wizara hiyo kujenga viwanda vya kusarifu samaki.
Alitumia fursa hiyo
kumpongea Rais kwa kuanzisha taasisi ya utafiti wa uvuvi na kueleza kuwa
ujenziwa taasisihiyo unatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mariam
Juma Abdalla Saadalla katika risala yake ya kitaalamu alieleza kwamba
uwekaji wa jiwe la Msingi la ujenzi wa soko hilo la kisasa na bandari ya wavuvi
ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza kuwa jitihada
hizo ni katika kuhakikisha sekta ya uvuvi inaimarika kwa madhumuni ya kukuza
uchumi wa buluu pamoja na kuepuka kuuza samaki katika maeneo yenye mazingira yasiyostahiki
ya kuhifadhi samaki.
Alisema kuwa hali hiyo
iliwapelekea wavuvi kupata kipato kidogo kulingana na jitihada na kazi
wanazozifanya sambamba na kutishia afya ya jamii.
Aliongeza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi
baada ya kuona hali hiyo iliendelea na jitihada za muda mrefu za kuwasiliana na
Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), kupitia Serikali ya Japan kuangalia
uwezekano wa kusaidia ujenzi wa soko la kisasa la samaki lililopo Malindi
ambalo itawanufaisha wavuvi wanaotumia bandari hiyo ya Malindi.
Aidha, Katibu Mkuu
huyo alieleza kuwa jengo hilo la soko la kisasa na bandari ya uvuvi linajengwa
na Kampuni ya Rinkai Nissan Construction Co. Ltd kutoka nchini Japan
ikisaidiana na Kampuni ya SCI Co. Ltd ya Dar es Salaam na Coastal Dredging Co.
Ltd ya Zanzibar.
Alisema kuwa ujenzi
huo utagharimu TZS bilioni 26.491 ambapo
kati ya fedha hizo bilioni 22.776 ni msaada kutoka Serikali ya Japan kupitia
(JICA) na TZS bilioni 3.715 ni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Mkataba
wa ujenzi ulifungwa rasmi Machi 26,2019 na ujenzi kuanza mnamo mwezi Juni,
2019.
Alisema kuwa soko hilo
linajumuisha sehemu sita za kuendeshea mnada, meza 141 za wauzaji wadogo wadogo
kati ya hizo 76 vitakuwa ni vibaraza vya kudumu na 65 ni meza za kuhamisha na
sehemu 13 za kuchakatia samaki, mtambo wa barafu chenga wenye uwezo wa
kuzalisha tani tatu za barafu kwa masaa 24.
Vile vile, alieleza
kuwa soko hilo litakuwa na uwezo wa kuegesha
vyombo vya uvuvi wa kienyeji vipatavyo 24 kwa wakati mmoja ambapo pia,
litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyakazi 1,400 kwa siku watakaohusika katika
ushushaji na upakiaji samaki.
Pia, Katibu Mariam
alisema kuwa soko hilo litakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wafanyabiashara
6,500 watakaotumia eneo salama ndani ya soko hatua ambayo itakuwa chachu ya
kuongeza kipato kwa wavuvi kwa kuwapa fursa ya kuanza kuuza samaki wao kwa
wakati muwafaka kutokana na hali halisi ya miundombinu ya soko hilo.
Alieleza kuwa
madhumuni ya soko hilo ni kuwawezesha watumiaji wa diko la Malindi kuuza na
kununua samaki wao wakiwa katika hali ya ubora na salama kwa afya ya mlaji
pamoja na kuwepo mazingira mazuri ya kuweka vyombo vya uvuvi na biashara kwa
wavuvi, wachuuzi, madalali, wauzaji wadogo wadogo pamoja na wanunuzi.
Katibu Mkuu huyo
alieleza kuwa soko hilo linatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Oktoba mwaka huu ambapo kutakuwa na kazi
ndogo ndogo za kumalizia ambazo zitaufikisha ujenzi huo mwezi wa Januari
mwakani.;p
Nae Afisa Mdhamini wa
Masuala ya Uchumi na Maendeleo katika Ofisi ya Ubalozi wa Japan nchini Tanzania
Bwana Katsutoshi Dakeda ambaye alimuwakilisha Balozi wa Japan nchini Tanzania
alisema kuwa Serikali ya Japan imekuwa
mshirika mkuu wa kuisaidia Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Alisema kuwa Serikali
ya Japan imekuwa ikisaidia miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa
katika kukuza uchumi.
Alisema kuwa mradi wa
ujenzi wa soko pamoja na bandari ya Malindi utasaidia kwa kiasi kikubwa katika
kukuza uchumi wa Zanzibar sambamba na kukuza kipato cha wavuvi wa Zanzibar huku
akieleza kuwa zaidi ya miaka 50 Japan imekuwa na mashirikiano mazuri na Jamhuri
ya Muunganowa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Nae Mwakilishi wa
Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) Bwana Matsuyama SATORU alisema kuwa fedha
ambazo zimetolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la (JICA) ni kielezo cha
kutosha cha mahusiano na mashirikiano ya muda mrefu yalipo kati ya Japan na
Serikali ya Jamhuriya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa mradi huo
utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya uvuvi hapa Zanzibar hatua
ambayo itaimarisha uchumi wa Zanzibar huku akieleza matumaini yake makubwa kuwa
mradi huo utaleta tija kubwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment