RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa uongozi wa Wizara ya Fedha
na Mipango kuwa wabunifu katika
kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato.
Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi
cha Julai hadi Disemba kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Rais Dk. Shein alisema kuwa iwapo suala zima la
ubunifu litapewa kipaumbele kwa Wizara hiyo mafanikio Zaidi yataendelea
kupatikana hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo ndio tegemeo kubwa
kwa Serikali na wananchi kutokana na kusimamia miradi muhimu ya maendeleo
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza haja
kwa Wizara hiyo kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwani ni
jambo lenye manufaa kwao pamoja na Taifa lao.
Aidha, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara
hiyo kuendeleza uadilifu, uaminifu,uzalendo pamoja sambamba na kusaidiana na
kuendeleza udugu ili kuweza kupata manufaa zaidi katika kazi zao na Taifa kwa
ujumla.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza
viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo na kutoa pongezi za pekee kwa Waziri wa
Wizara hiyo, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa kwa kutekeleza vyema majukumu yake
kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Dk. Shein alieleza imani yake kwa uongozi wa
Wizara ya Fedha na Mipango na kusisitiza haja ya kuendelea kuvumiliana na
kushirikiana sambamba na kupendana huku akisisitiza kuwa ataendelea kutumia
hekima na busara katika uongozi wake.
Pia, aliipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri ya
uandaaji wa taarifa hiyo pamoja na uwasilishaji wake na kueleza jinsi
anavyofarajika na uwasilishwaji mzuri unavyofanywa hivi sasa na Wizara mbali
mbali ikilinganishwa na hapo siku za nyuma.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya
usimamizi mzuri wa Maghala ya Serikali na kusisitiza umuhimu wa Wizara hiyo
kuyafuatilia Maghala hayo ili kujulikana wasimamizi wake.
Alieleza haja kwa Wizara hiyo kuwatumia watafiti
wazalendo kufanya tafiti mbali mbali badala ya kutumia watafiti kutoka nje ya
nchi kwani tayari wapo watafiti wazalendo waliobobea katika shughuli hizo hapa hapa
nchini hivi sasa.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja
ya kuweka mikakati maalum ya kuyatangaza maeneo huru ya Vitega uchumi yaliopo
hapa Zanzibar likiwemo eneo la Micheweni Pemba.
Akieleza kuhusu Shirika la Bima pamoja na Benki ya
Watu wa Zanzibar, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelea kushindana kibiashara kwa kupanua
huduma zake ndani na nje ya nchi kwa azma ya kufikia lengo lililokusudiwa.
Dk. Shein, alisisitiza juu ya matumizi ya Takwimu
pamoja na kuandaa taarifa ya mafanikio yanayotokana na maazimio ya Semina ya
Takwimu na matumizi yake iliyofanyika Februari 2, mwaka 2017 iliyowashirikisha viongozi
mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akieleza haja ya kuwepo
mabadiliko katika suala zima la matumizi ya takwimu.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo na kupongeza kwa hatua za Wizara hiyo kwa kutoa
mishahara kwa wakati hatua ambayo imekuwa ikitoa faraja kubwa kwa wafanyakazi
wa sekta ya umma.
Mapema Waziri wa Wizara hiyo Balozi Mohamed Ramia
Abdiwawa alieleza kuwa uchumi wa
Zanzibar umeendelea kuimarika ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa Pato halisi la
Taifa na kufikia thamani ya TZS Bilioni 2,684 mwaka 2017 sawa na kasi ya ukuaji
wa wastani wa asilimia 7.1.
Alieleza kuwa kendelea kuwepo kwa Amani na
utulivuna kuongezeka kwa vivutio vya watalii kumepelekea kuimarika idadi ya wataalii
waliotembelea Zanzibar mwaka 2019 kufikia watalii 538,264 kutoka watalii
520,809 mwaka 2018 huku akieleza jinsi ukusanyaji wa mapato ulivyoimarika kwa
kiasi kikubwa katika mwaka 2019.
Pamoja na hayo, Balozi Ramia alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi zinazotolewa na wazee wastaafu kutokana na hivi sasa wastaafu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekuwa wakilipwa Pencheni yao mapema
ikilinganishwa na hapo siku za nyuma ambapo hivi sasa wanalipwa kuanzia tarehe
18 ya mwezi kabla ya wafanyakazi wa sekta ya umma.
Balozi Ramia pia, alitumia fursa hiyo kueleza
utekelezaji wa miradi mbali mbali ya Wizara ya Fedha na Mipango inavyoendelea
kwa kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2019 ukiwemo mradi wa Uimarishaji
Huduma za Jamii Mijini (ZUSP).
Mradi mwengine ni Uwekaji wa Taa za Barabarani
Unguja na Pemba, Ujenzi wa Jaa la Kibele,ujenzi wa Ofisi za Serikali, ujenzi wa
Mji Mpya wa Kwahani na miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Jamii (ZSSF) ukiwemo
Michenzani Mall, jengo la Sheikh Thabit Kombo Michenzani, Ofisi ya ZSSF Pemba
na mradi wa ujenzi wa Hoteli ya Mkoani.
Mradi mwengine ni ujenzi wa jengo jipya la Ofisi
ya Bodi ya Mapato (ZRB) Pemba pamoja na miradi inayotekelezwa na Benki ya Watu
wa Zanzibar (PBZ) ukiwemo ujenzi wa Tawi la Wete, Huduma za Utawala, Huduma za
Viza na mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Bima Pemba.
Nao viongozi wa Wizara hiyo walieleza juhudi
zinazochukuliwa katika kufanikisha miradi pamoja na shughuli mbali mbali
zinazofanywa na Wizara hiyo kupitia taasisi zake na akutumia fursa hiyo
kumpongeza Rais Dk. Shein kwa jinsi anavyowaongoza na kuwapa maelekezo.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango
Khamis Mussa Omar, alitumia fursa hiyo kueleza utekelezaji wa Malengo kwa robo
mbili kuanzia mwezi wa Julai hadi Disemba katika mwaka wa fedha wa 2019/2020
kwa Wizara hiyo ambapo kwa upande wa Tume ya Mipango Katibu Mtendaji wa Tume
hiyo Mwita Mgeni Mwita nae alitoa taarifa ya Tume hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment