Habari za Punde

WANANCHI WAFURAHIA KUFUNGULIWA KWA OFISI YA TRA KILOLO

Afisa Msimamizi Mwandamizi wa Kodi Bw. Barnabas Masika kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akitoa elimu ya kodi kwa mfanyabiashara wa eneo la Ilula Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo. Kampeni hiyo inatarajiwa kumalizika tarehe 22 Februari, 2020.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi Bi. Rose Mahendeka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiwaelimisha wananchi na wafanyabiashara (hawapo pichani) wa Kata ya Dabaga Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo. Kampeni hiyo inatarajiwa kumalizika tarehe 22 Februari, 2020.
Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa Kata ya Dabaga Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wakimsikiliza kwa makini Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi Bi. Rose Mahendeka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (hayupo pichani) wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani humo. Kampeni hiyo inatarajiwa kumalizika tarehe 22 Februari, 2020.
Na Veronica Kazimoto. Kilolo
Wananchi na wafanyabiashara wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wamefurahia kitendo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufungua ofisi wilayani humo na kusema kuwa, uwepo wa ofisi hiyo siyo tu umewasogezea huduma karibu bali utaongeza tija katika ukusanyaji mapato ya Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo, wananchi hao wamesema kuwa, awali walikuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda Iringa mjini kufuata huduma za TRA suala lililopelekea kutumia muda mwingi tofauti na ilivyo hivi sasa.
Prosper Mwinu ni mfanyabiashara wa duka la vipodozi wilayani humo ambaye ameeleza kuwa ufunguzi wa ofisi hiyo pia umewaondolea gharama walizokuwa wakizitumia kufuata huduma za TRA Iringa mjini.
“Kwakweli tunaishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania kutusogezea huduma karibu kwa kutufungulia Ofisi ya TRA hapa Kilolo maana tulikuwa tunatumia gharama za kusafiri kwenda Iringa mjini kuifuata TRA na wakati mwingine tulikuwa tunaingia gharama za kulala huko ikitokea tumeshindwa kupata huduma zote kwa siku moja,” alisema Mwinu.
Naye, Grace Barnaba mfanyabiashara wa duka la pembejeo alisema kwamba, wananchi wanapokuwa wamesogezewa huduma karibu wanakosa sababu ya kutokulipa kodi kwa wakati kwani hawakutani na foleni na hupata huduma hizo kwa haraka.
“TRA wamefanya jambo jema sana kutufungulia ofisi hapa wilayani yaani hatuna tena sababu ya kuchelewa kulipa kodi maana mwanzoni tulikuwa tunakutana na foleni kubwa Iringa mjini lakini kwa sasa tatizo hilo limekwisha na tutalipa kodi zetu kwa wakati,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Asiah Abdallah amesema kuwa, ufunguzi wa Ofisi ya TRA wilayani kwake, umewafurahisha sana wananchi kwa sababu walikuwa wakitembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 60 kwenda kutafuta huduma za kulipa kodi, hivyo ofisi hiyo mpya itawarahisishia wananchi hao suala zima la ulipaji kodi na hatimaye kuongeza uchumi wa wilayani hiyo.
“Kwahiyo ninachotaka kusema ni kwamba, tumepiga hatua kubwa sana kuwepo kwa Ofisi ya Mapato katika wilaya yetu ya Kilolo na hivyo tunategemea uchumi wa wilaya yetu utaongezeka kutokana na kwamba wananchi sasa watakuwa wanalipa mapato katika njia ambayo ni rafiki na rahisi”, alieleza Mkuu wa wilaya hiyo.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani Iringa ilianza tarehe 17 na inatarajia kumalizika tarehe 22 Februari, 2020 ikiwa na lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla masuala mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja na kupokea maoni yao, mrejesho na changamoto za ulipaji kodi walizonazo ili kuzitafutia ufumbuzi.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.