Habari za Punde

Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Redio DunianiNa Mwashungi Tahir     Maelezo Zanzibar.
WAZIRI wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe.Mahmoud Thabit Kombo amezitaka radio jamii kuhakikisha wanatoa habari zisizo na uchochezi hasa katika kipindi hiki kunachokaribia uchaguzi nchini.
Hayo ameyasema huko kwenyen ukumbi wa Hoteli ya   Zanzibar Beach Resort Mazizini wakati alipokuwa akifungua maadhimisho ya Radio Duniani  na kuwataka kutumia radio zao vizuri kwa lengo la kuelimisha jamii.
Alisema radio ni chombo kinachohabarisha  kwa kuwapa habari wananchi popote wanapokuweko kwa urahisi hivyo kuwepo umakini kuzitangaza habari zisiwe  za uchochezi kwani zinaweza kuvunja amani.
Pia alisema radio nyingi huwa zinabadilika wakati unapokaribia uchaguzi hivyo mjitahidi kutayarisha vipindi vizuri vitakavyoelimisha jamii  na vitavyokuwa na haiba nzuri kwa wasikilizaji wake.
“Wito wangu jitahidini  kuweka vipindi vya radio vya kuelimisha na epukeni kutangaza habari za uchochezi ambazo zinaweza kuondosha amani na utulivu  uliyotawala nchini hasa kipindi hiki kinachokaribia  uchaguzi”alisema Waziri huyo.
Hivyo amezitaka radio kujitahidi kufuata misingi ya kisheria  iliyowekwa na kuepuka kuvunja sheria  pia kuzitaka  kuendeleza amani na utulivu uliyopo katika  nchi zote mbili.
Aidhaalisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha radio ili jamii iweze kuelewa matokeo mbali mbali yanayotokea ndani ya Nchi na nje ya Nchi.
Nae Mwenyekiti wa Bodi TADIO Community media  Prosper Kwigize  alisema bado kuna watu wachache wasojua kusoma wala kuandika hivyo uwepo wa radio kunaweza kuwapa fursa ya kujua mambo mengi yanayotokea.
Alisema katika kuifanya radio kuwa mjumuisho ni vyema Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar zipunguze vikwazo vya sera na sheria ili radio ziweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wa washiriki wameishukuru viongoziwa Serikali jinsi walivyoweza kueneza radio mjini na vijijini kwani kumeweza kuwafanya kuzisikia habari kwa wakati  ambapo hapo zamani kulikuwa na radio moja tu na jamii ilikuwa haifaidiki.
Pia walisema radio ina uwanja mpana wa kueneza habari kwa mara moja na watu wengi kusikia ukiwa shamba , njiani unafanya shughuli zako huku unasikiliza taarifa.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.