Habari za Punde

Jinsi Wanamichezo Afrika Wanavyoathiika Kiuchumi

Soka la wanawake limeathirika zaidi Afrika
Ni miezi minne tu imepita tangu mlipuko wa COVID-19 kuanza lakini gonjwa hili limesambaratisha kabisa shughuli za michezo kote duniani huku matukio makubwa kimichezo yakisimamishwa, kuahirishwa au kufutwa kabisa.
Kalenda ya mwaka 2020 ilikuwa imejaa mashindano makubwa ya michezo ikiwemo Olimpiki, Kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake, michuano ya soka ya mataifa ya ulaya, mashindano ya riadha barani Afrika, pamoja na michuano ya CHAN miongoni mwa mashindano mengine- lakini yote yameahirishwa au kufutwa.
Hali ya kukosekana kwa michezo inayoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni kote duniani inamaanisha wachezaji, makocha, vilabu na mashirikisho yamebakia bila kipato na akiba zilizokuwepo kumalizika. Kote barani Afrika hali hiyo imeleta changamoto nyingi. Makala hii inaangazia jinsi hali hii imeathiri soka katika bara la Afrika.
''Soka ni maisha yetu- wakati soka inaposimama, maisha kwetu yanakuwa yamesimama pia", ndivyo anavyosema David Juma, nahodha wa timu ya Kakamega Boyz kwenye ligi kuu ya Kenya.
Ingawa soka ni mchezo unaopendwa zaidi na kuwa na wafuasi wengi mno barani Afrika, kuna mapato madogo sana kifedha yasioendana na hamasa hiyo kubwa, ikilinganishwa na ligi za barani ulaya na Marekani.
Kwa mujibu wa ligi kuu ya Kenya- mojawapo ya ligi kongwe zaidi katika Afrika mashariki- asilimia 50% ya wachezaji katika ligi hiyo wanapata kwa wastani mshahara wa dola 200 za Kimarekani. Kwa sababu hiyo, wachezaji wengi hutegemea pesa za ziada wanazopata baada ya mechi, posho za usafiri na malipo ya ziada wanayopata kutokana na ushindi a mataji.
Bila kuwepo na mechi zozote za kucheza, njia hizo za mapato ya ziada zinakuwa hazipo pia. Zaidi ni kwamba wafadhili wa ligi hiyo- SportsPesa wamejiondoa.
Wapo wachezaji wengine katika ligi hiyo ya Kenya wasiopata ujira wowote kutokana na kucheza, pesa zozote wanazopokea ni kutokana na kupata kazi katika kampuni inayomiliki klabu. Wakati huu wa janga la Korona, kampuni nyingi kama hizo haziendelei vizuri.
"Tuliambiwa mishahara yetu itapunguzwa kwa asilimia 50%- mwenyekiti wetu naye ni mfanyabiashara, na kutokana na corona biashara yake haifanyi vizuri,"Juma anazidi kuelezea.
"Kama mfanyabiashara, alijua hataweza kumudu kulipa mishahara kamili- kwa hivyo anachukua hatua hiyo badala ya kuwafukuza wachezaji bila malipo yoyote."
Mishahara ya wachezaji wa soka nchini Cameroon inafanana na nchini Kenya, lakini kunao mwongozo wa kuwalinda wachezaji unaoweka kiwango cha chini kabisa kuwa dola 200 kwa mwezi.
Klabu ya Coton Sport ndio klabu inayofadhiliwa na serikali kwenye ligi kuu ya Cameroon. Mchezaji wao Thomas Bawak anakiri mambo si mazuri kipindi hiki kwa sababu sawa na Kenya, ada za kiingilio zinazolipwa na mashabiki katika siku za mechi ni sehemu kubwa ya mapato ya klabu.
"Kunao mshahara uliowekwa lakini kufikia mwezi ujao sidhani kiasi cha mshahara kitakuwa kama sasa hivi," anasema.
Mbali na riziki kupungua, wachezaji pia wanakabiliwa na msongo wa mawazo unaosababishwa na mambo haya mawili -matatizo ya kifedha na wasi wasi kuhusu janga la corona.
Thomas anasema hali hii imewafanya wachezaji kujisikia "wamedhoofika kisaikolojia". Wengi wana wasi wasi kuhusu watawezaje kutunza familia zao.
Ni hali anayoielewa vyema Bolaji Simeon kutoka Nigeria, anayechezea klabu ya Horoya FC ya nchini Guinea, ambao wako kwenye nusu fainali zilizoahirishwa za Kombe la Shirikisho Afrika.
"Mbali na mke wangu na watoto, nawatunza kaka zangu ambao wako shuleni, mama mzazi na pia dada zangu,"anasema.
"Kwa kweli nina wasi wasi mkubwa wakati huu hakuna mechi, hatupati posho zozote."
Hata vilabu nchini Afrika Kusini na kaskazini mwa Afrika, ambavyo kawaida huwalipa wachezaji mishahara ya juu ikilinganishwa na maeneo mengine barani humo, pia havijaepuka athari za COVID-19.
Nchini Misri, vilabu vikubwa kama El Gouna, Arab Contractors na Pyramids vimetangaza vitapunguza mishahara ya wachezaji wao huku klabu ya Smouha pia ikitangaza itapunguza mshahara wa kocha kwa asilimia 50%.
Wizara ya michezo nchini Misri, hata hivyo, imesisitiza kuwa vilabu vya hadhi ya juu zaidi vinahitaji kusaidia vilabu vingine vya ngazi za nchini ambavyo vimekumbwa na matatizo makubwa kifedha. Miongoni mwa vilabu hivyo vya hadhi ya juu ni Al Ahly, iliyoshinda mataji mengi zaidi barani Afrika.
Lakini Al Ahly wenyewe wanajiandaa kupunguza mishahara ya wachezaji kutokana na ukosefu wa mechi. Wanaendelea kupata hasara kifedha, licha ya kuwa miongoni mwa timu nne zilizofikia hatua ya nusu fainali ya ligi ya klabu bingwa Afrika iliyoahirishwa.
Sio ligi ya klabu bingwa Afrika pekee iliyoahirishwa, mashindano mengine ya CAF pia yamejikuta katika hali hiyo. Michuano ya Kombe la mataifa ya Afrika kwa wanawake imeahirishwa, sawa na mashindano ya Afrika kwa wasichana wasiozidi miaka 17, na Kombe la dunia kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20.

Soka la wanawake pia limepata pigo, labda hata zaidi kuliko wengine.
Wanasoka wa kike barani Afrika hupata mshahara wa wastani wa dola 100 kwa mwezi, au chini ya kiasi. Kutokana na hali hiyo wengi wanajiandikisha kupata elimu ya juu au kutafuta kazi nyingine ili kumudu gharama za miasha.
Lakini pia kwenye ligi mashuhuru duniani, wachezaji wa Kiafrika hawajapona mkasi wa kupunguza mishahara.
Hata kwenye ligi kuu ya England, vilabu vimewaomba wachezaji kukubali kupunguza mishahara au kucheleweshwa malipo.
Hata hivyo, zipo hatua madhubuti zilizochukuliwa na nchi, mashirikisho, vilabu na wahisani katika jaribio la kupunguza athari za kifedha kwa wachezaji zilizoletwa na janga la corona.
Shirikisho la soka duniani Fifa limetangaza mfuko wa dharura ili kutoa fedha kwa mataifa wanachama kushughulikia matatizo ya kifedha ya sasa hivi".
Mashirikisho kadhaa ya soka barani Afrika tayari yametumia fedha hizo kutoka Fifa pamoja na hazina zao wenyewe kusaidia vilabu.
Chama cha Soka nchini Sierra Leonne, kwa mfano, kimetoa kiasi cha dola 67,500 kwa ligi kuu, ligi ya daraja la kwanza na ligi ya daraja la pili nchini humo kama njia ya kuonyesha mshikamano wakati huu wa janga la corona. Kiasi cha dola 42,000 kitakwenda kwa timu za ligi kuu, ilhali dola 25,500 zitakwenda kwa vilabu vya madaraja ya chini.
Katika hatua nyingine sawa na hiyo, chama cha soka nchini Misri kimeamua kuanzisha mpango wa kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji wa ligi za daraja la tatu na nne.
Na Afrika Kusini imetenga kiasi cha dola milioni nane kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wanamichezo na wasanii.
Hatua zingine zilizochukuliwa kote barani Afrika ni pamoja na Liberia kuidhinisha kiasi cha dola 4,200 kutolewa kwa vilabu kwenye ligi za wanaume na wanawake; wachezaji nchini Algeria kutoa sehemu ya mishahara yao kuchangia mfuko wa kupambana na corona; na shirikisho la soka nchini Uganda kutoa tani 12.5 za mpunga kwa wachezaji, maafisa na mashabiki.
Wahisani pia wamechukua nafasi yao: Mark Twinamatsiko, kocha wa klabu ya ligi ya daraja la tatu Kitara FC ameahidi kutoa nusu ya mshahara wake kwa wachezaji wake, huku mmiliki wa klabu ya Wazito FC katika ligi kuu ya Kenya Ricardo Badoer, akisema wachezaji wake na wahudumu wataendelea kupokea mishahara kamili.
Badoer anasema mwenyewe alishawahi kuishi maisha bila ajira na hataki waajiriwa wake wapitie madhila aliyopitia.
Hata hivyo idadi kubwa ya vilabu na wachezaji wamezongwa na athari za COVID-19.
"Lazima timu zifikirie nje ya taratibu za kawaida za kila siku," anasema David Juma.
"Ni vipi tunaweza kutengeneza pesa zetu wenyewe kama timu? Hapa ndipo tunapotengeneza pesa zetu. Posho hizi zinapotoweka tunateseka sana."
Mateso hayo yanawakuta wengi kutokana na mikataba kukatishwa, na pia mapato ya vilabu kupungua. Ingawa afya na usalama wa wachezaji ni muhimu zaidi, bila mipango mbadala, ukosefu wa fedha miongoni mwa wanasoka barani Afrika utaendelea kuwepo hadi pale viwanja vitaacha kukaa kimya bila mashabiki kutokana na janga la corona.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.