Na
Jonas Kamaleki, Dodoma
Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameweka nguvu zao pamoja kupambana na ugonjwa
wa Corona na kuweka itikadi zao za kisiasa pembeni.
Akizungumza leo Bungeni
jijini Dodoma katika kikao cha kwanza cha Bunge la Bajeti la 2020/21, Spika wa
Bunge, Mhe. Job Ndugai amewataka wabunge na wadau wengine waweke umbali kati ya
mtu na mtu (sociali distance) ili kuepuka maambukizi ya Corona.
Kwa kuzingatia hilo,
jumla ya wabunge wasiozidi 150 ndio wanaoruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa
Bunge. Muda wa vikao vya Bunge nao umebadilishwa na kufanya vikao vya bunge hilo
kuanza saa 8:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni badala ya saa 3:00 asubuhi.
Baadhi ya wabunge
waliofanya mahojiano na Idara ya Habari (MAELEZO) wameonyesha kuondoa tofauti
zao za vyama, itikadi na mitazamo na kuweka nguvu ya pamoja kupambana na
Corona.
Mhe. Joseph Selasini
(Mb) Rombo CHADEMA amesema anamuunga mkono Spika asilimia 100 na kuongeza kuwa
mbunge au mtu yeyote anayefanya siasa katika janga hili huyo atakuwa na
upungufu wa kifikira.
“Ugonjwa huu
ukisambaa utamkumba mwanasiasa wa chama chochote, mfanyabiashara wa aina yoyote
na mwananchi wa mazingira yoyote”, amesisitiza Mhe. Selasini.
Akitoa maoni yake
kuhusu vita dhidi ya Corona, Mbunge wa Mbozi CHADEMA, Paschal Haonga amesema
ugonjwa wa Corona hauna itikadi unaweza kumpata mtu yeyote yule na kuwataka
wautambue ugonjwa huo kuwa ni adui wa kila mtu.
Aidha, amewahimiza
watu wote wanaouza vifaa vya kujikinga na ugojwa huo kupunguza bei ili wananchi
wa kawaida waweze kumudu gharama za upatikanaji wa vifaa hivyo na kupunguza
kasi ya maambukizi na kusambaa kwake.
Naye Anthony Komu, Mbunge
wa Moshi Vijijini CHADEMA anasema, “Tuungane pamoja kama viongozi wa nchi kupambana
na janga la Corona bila kujali vyama vyetu vya siasa”. Amewaasa viongozi
wenzake wawe makini katika kufuata masharti yanayoelezwa na wataalaam katika
kupambana na ugonjwa huo.
Kwa upande wake Rhoda
Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum Katavi, CHADEMA amesema ugonjwa wa Corona si
suala la kisiasa na ametoa wito kwa watanzania na Serikali kwa ujumla kuweka
vituo vya kupima ugonjwa huo hususan kwa watu wanaofanya kazi katika masoko
makubwa kama Kariakoo na ameiomba Serikali kupeleka vitendea kazi vya kupima ugonjwa
huo maeneo mengi ya nchi ili kuepusha maambukizi mapya.
Naye Aida Kenani, Mbunge wa Viti Maalum Rukwa
CCM ameitaka jamii ya watanzania kuacha mizaha na ugonjwa wa Corona na kuweka
siasa kando kwa vitu vya msingi ili taifa na maisha ya watanzania yapewe
kipaumbele.
Bunge la Bajeti kwa
mwaka wa Fedha 2020/21 limeanza leo jijini Dodoma na linafanyika kwa aina
tofauti na mikutano iliyopita, hatua hiyo inatokana na uwepo wa ugonjwa wa
Corona, ndiyo maana wabunge wachache wanaruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa
bunge ambapo vikao hivyo vitafanyika kwa saa nne tu kwa siku.
No comments:
Post a Comment