Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Awasilisha Mapitio na Muelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge Kwa Mwaka 2020/2021.


HOTUBA YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE
KWA MWAKA 2020/2021

UTANGULIZI

1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Mfuko wa Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020  na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2020/2021. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2020/2021.

2.        Mheshimiwa Spika, wakati tunapojadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2020/2021 hatunabudi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutujaalia afya na uzima.

3.     Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Bunge lako Tukufu lilimpoteza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar. Pia naungana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wenzangu kutoa salam za pole kwa familia ya Marehemu na wanachama wa CUF kufuatia kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa Alhaji Khalifa Suleiman Khalifa. Pia kwa masikitiko makubwa niungane na wananchi wote, familia na wanahabari wote nchini kwa kifo cha Mwandishi wa Habari Mwandamizi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC) ndugu yetu Marin Hassan Marin kilichotokea leo alfajiri, Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi – Amina. Vilevile, Taifa letu lilikumbwa na majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko nchini kote na ajali za barabarani ambazo zilisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

4.               Mheshimiwa Spika, sambamba na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa misiba iliyotokea, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu awajaalie afya njema waliopata majeraha na azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina! Vilevile, nawashukuru kwa dhati wale wote waliojitolea kwa hali na mali katika kuwasaidia majeruhi na wahanga wa matukio hayo.


5.               Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu, mwaka huu Serikali ya Awamu ya Tano inahitimisha kipindi cha kwanza cha miaka mitano kilichoanza Mwaka 2015. Kwa msingi huo, hotuba yangu itaeleza kwa muhtasari baadhi ya mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata katika kipindi cha takriban miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

6.               Mheshimiwa Spika, hotuba hii inaainisha baadhi ya kazi zilizotekelezwa na Serikali kwa kuzingatia mipango na mikakati mbalimbali hususan Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025. Mikakati na Mipango hiyo, inatekelezwa sambamba na mipango mingine ya kikanda na kimataifa kama vile Agenda ya Mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika na Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030.

7.               Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu, huduma za kiuchumi na kijamii, utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na kuhamasisha uwekezaji. Ningependa kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya Tano katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 hadi 2020. Nawapongeza pia, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Balozi Seif Ally Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

8.               Mheshimiwa Spika, kipekee nakushukuru wewe binafsi, pia Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuliongoza vyema Bunge lako Tukufu na Wabunge wote katika kuisimamia Serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza wajibu wake ipasavyo wa kuhudumia wananchi. Vilevile, natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria chini ya uenyekiti wa Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Jimbo la Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI chini ya uenyekiti wa Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wa Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi. Maoni na ushauri wa Kamati hizo umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2020/2021.

9.               Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano mlionipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa na hivyo, kuwezesha Serikali kutekeleza kazi zake kwa tija na ufanisi. Vilevile, nawashukuru kwa michango yenu iliyowezesha kukamilisha Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021.

10.            Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa, namshukuru Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Mhe. Angellah Jasmine Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji); Mhe. Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira); Mhe. Stella Alex Ikupa, Mbunge wa Viti Maalum na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu); Makatibu Wakuu Bw. Andrew Wilson Massawe (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bibi Dorothy Aidan Mwaluko (Sera, Uratibu na Uwekezaji) na Bw. Tixon Tuyangine Nzunda (Waziri Mkuu na Bunge) na Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

11.            Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na kuiletea nchi yetu maendeleo. Mchango wao umekuwa muhimu kuwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.

12.            Mheshimiwa Spika, ninawashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha, nawashukuru wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kushirikiana nami na kwa kuniunga mkono. Niwapongeze na kuwashukuru kwa kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni kwa ufanisi. Kipekee, namshukuru sana mke wangu mpendwa, Mary; watoto wangu na familia yangu kwa ujumla kwa upendo wao, uvumilivu na maombi yao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ya kitaifa. Nawashukuru sana.

 

Homa Kali ya Mapafu

13.            Mheshimiwa Spika, hivi sasa nchi yetu na dunia kwa ujumla inapitia katika kipindi kigumu. Itakumbukwa kwamba, tarehe 11 Machi 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa Homa Kali ya Mapafu ijulikanayo kama COVID-19 inayosababishwa na virusi vya CORONA kuwa ni janga la Kimataifa. Aidha, tarehe 16 Machi, 2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilitangaza kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza nchini.

14.            Mheshimiwa Spika, tangu kugundulika kwa ugonjwa huo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukaguzi, upimaji na ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini ili kubaini wasafiri wanaoonesha dalili za ugonjwa au wenye viashiria hatari hata hivyo mashirika mengi yamesitisha ndege zao kwa kukosa abiria. Abiria waingiao wote hupelekwa nyumba ya kujitenga kwa gharama zao, tumetenga na hostel ili kuwapunguzia gharama. Kadhalika, katika kukabiliana na virusi vya CORONA, Serikali ilitoa maelekezo yafuatayo:
Moja:             Kusitisha Mbio za Mwenge wa Uhuru na kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya jukumu hilo zitumike kusaidia hatua za kukabiliana na janga la virusi vya Corona;
Mbili:            Kusitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo ligi kuu ya Tanzania Bara, ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na aina nyingine za   michezo;
Tatu:               Kusitisha shughuli zote za elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, Sekondari, vyuo vya kati hadi vyuo vikuu;
Nne:               Kusitisha Semina, Warsha, Makongamano na Mikutano yote ya ndani na ya hadhara yenye kuhusisha mjumuiko wa watu wengi;
Tano:              Kuwatenga abiria waingiao nchini kwenye maeneo maalum kwa siku 14 ili kufuatilia hali zao mpaka tutakapojiridhisha kuwa hana ugonjwa;
Sita:                Kuwasisitiza watanzania kufuata kanuni za kudhibiti maambukizi ikiwemo kunawa maji kwa sabuni, kukinga unapokohoa na kupiga chafya, kutopeana mikono bila sababu, kukaa au kusimama kwa umbali na jirani yako n.k; na
Saba:              Kuwaasa Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi ya virusi vya Corona, kusitisha safari hizo, na hatua zingine zitafuata.

15.            Mheshimiwa Spika, serikali inaendelea na usimamizi wa karibu sambamba na kufanya tathmini na kuchukua hatua kadhaa. Tumeunda Kamati za kitaifa tatu (3) zinazosimamia ugonjwa huu, niendelee kusisitiza kuwa sote tuzingatie maelekezo yaliyotolewa na Serikali toka tulipoanza kampeni ya kupambana na ugonjwa huu. Aidha, niwatake Watanzania kuzingatia masharti ya afya kwa kufuata ushauri unaotolewa na wataalam. Mgonjwa akithibitika, atapelekwa eneo maalum bila kujali cheo chake, atalala palipoandaliwa. Watanzania wenzangu tuendelee kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

 

16.            Mheshimiwa Spika, tarehe 20 Novemba 2015 wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaahidi wananchi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia na kuwajali.

17.            Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, ndani ya kipindi cha takriban miaka mitano mafanikio makubwa yamepatikana na yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi na kijamii kwenye Taifa letu. Ujenzi wa miundombinu muhimu ya kiuchumi hususan ya usafiri na usafirishaji sambamba na uimarishaji wa huduma muhimu za kijamii ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano.

18.            Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway), ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania, ufufuaji wa ushirika na mali za ushirika mfano, NCU, SHIRECU, WETCU na Mamlaka ya Mkonge Tanzania, ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, ulinzi wa maliasili na rasilimali zetu pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Elimu, Afya na Maji ni kati ya hatua za msingi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo Mwaka 2025.

19.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia miradi hiyo muhimu ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa mfano, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa ambao hadi Machi 2020 umetumia Shilingi trilioni 2.96 na kukamilika kwa asilimia 75 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na asilimia 28 kwa kipande cha Morogoro hadi Makutupora.

20.            Mheshimiwa Spika, Serikali inatumia gharama kubwa katika kujenga miundombinu hiyo wezeshi ya kiuchumi kwa lengo la kulifanya Taifa letu kuwa na uchumi imara wa kujitegemea na wenye kuhimili ushindani. Fedha hizo pia zimekuwa chanzo cha ajira na zabuni kwa Watanzania zinazowasaidia kuongeza kipato.

21.            Mheshimiwa Spika, mradi huu utakapokamilika utaongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria pamoja na kupunguza gharama za uchukuzi. Kadhalika, utachochea ukuaji wa miji na sekta nyingine kama vile kilimo, viwanda, utalii na biashara. Vilevile, mradi huu utakuwa chanzo cha ongezeko la mapato ya Serikali yatakayosaidia katika kuboresha maslahi ya watumishi na huduma za kijamii kama vile afya, elimu na maji.

22.            Mheshimiwa Spika, vilevile, ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere ambalo litakapokamilika litazalisha umeme wa Megawati 2,115. Hadi Machi 2020 mradi huo umegharimu Shilingi trilioni 1.28 na umekamilika kwa asilimia 10.74. Kukamilika kwa bwawa hilo kutalihakikishia Taifa letu umeme wa uhakika na wa nafuu zaidi. Aidha, ongezeko hilo la uzalishaji wa umeme litawezesha shughuli za uzalishaji viwandani kuwa za uhakika, tija, ufanisi na gharama nafuu. Vilevile, mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya nishati ya umeme kwa watu wengi.

23.            Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa kutekeleza Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) ambapo vijiji vilivyounganishiwa umeme nchini vimeongezeka kutoka vijiji 2,118 Mwaka 2015 hadi vijiji 9,001 mwezi Machi 2020. Mradi huo pia umezinufaisha Taasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, dini, mashine za kusukuma maji na huduma za biashara.

24.            Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga, Serikali inaendelea kuliimarisha Shirika la Ndege la Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2020 tayari ndege 8 mpya zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na kuanza kazi. Kadhalika, malipo ya awali ya Shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine 3 mpya yamefanyika. Ununuzi wa ndege hizi, umeongeza ufanisi katika usafiri wa anga, kuongezeka kwa mapato ya Serikali, kuimarika kwa utalii na kuongezeka kwa fursa za ajira katika sekta ya huduma.

25.            Mheshimiwa Spika, bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 31 kwa Mwaka 2015 hadi Shilingi bilioni 269 kwa Mwaka 2019. Serikali pia imegharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya kwa kujenga zahanati 1,198, ukarabati wa vituo vya afya 487, hospitali za Halmashauri za Wilaya 69 na hospitali za rufaa za mikoa 10 za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure, Mwananyamala, Mawenzi, Manyara, hospitali za rufaa za kanda 3 za Mtwara, Mbeya na Burigi-Chato na Hospitali Maalum ya Kibong’oto na Uhuru - Chamwino. Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020 jumla ya Shilingi trilioni 3.01 zimetumika kugharamia huduma za afya. Kuongezeka kwa bajeti ya dawa na uboreshaji wa miundombinu ya afya, kumeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuimarisha afya za Watanzania.

26.            Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kuwa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya, ununuzi wa dawa na vifaa vya kisasa vya tiba ni utekelezaji wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhakikisha kila Mtanzania anapatiwa haki yake ya kupata matibabu tena katika eneo alipo.

27.            Mheshimiwa Spika, katika eneo la elimu, Serikali imeongeza mikopo kwa ajili ya elimu ya juu kutoka Shilingi bilioni 365 Mwaka 2015 hadi Shilingi bilioni 450 Mwaka 2019. Elimumsingi bila Ada nayo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kupatiwa elimu.

28.            Mheshimiwa Spika, utekelezaji mzuri wa Mpango wa Elimumsingi bila Ada, uliwezesha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza. Kwa mfano, kabla ya kuanza kwa Mpango huo Mwaka 2015 ni wanafunzi 1,568,378 walioandikishwa. Aidha, baada ya kuanza utekelezaji wa Mpango Elimumsingi Bila Ada wanafunzi 2,120,667 waliandikishwa Mwaka 2016. Katika kipindi cha mwaka 2015 hadi Februari 2020 jumla ya Shilingi trilioni 1.2 zimetumika kugharamia Elimumsingi Bila Ada.

29.            Mheshimiwa Spika, maboresho yanayofanyika kwa upande wa elimumsingi yanazingatia uhitaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Kuanzia Mwaka 2015 hadi Februari, 2020 vyumba vya madarasa 166,627, maabara 5,801, nyumba za walimu 57,541, matundu ya vyoo 231,612 yamejengwa na madawati 2,886,459 yamenunuliwa. Aidha, idadi ya shule za msingi zenye madarasa ya elimu ya awali imeongezeka kutoka madarasa 16,889 Mwaka 2015 hadi kufikia madarasa 17,771 Mwaka 2020. Kadhalika, idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka shule 4,708 Mwaka 2015 hadi shule 5,330 Mwaka 2020.

30.            Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Elimumsingi Bila Ada unawahakikishia watoto wote wa kitanzania hususan wale wa hali ya chini kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu. Aidha, Mpango huo umewapunguzia wazazi mzigo wa ada na michango isiyokuwa ya lazima na hivyo kujielekeza zaidi katika kutafuta na kuwapatia mahitaji ya msingi vijana wetu kama vile sare za shule na madaftari.

31.            Mheshimiwa Spika, kama utakavyokumbuka, katika vikao vingi vya Bunge lako Tukufu vilivyotangulia, changamoto ya maji ni suala lililoongoza kuchangiwa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge. Katika kipindi cha takribani miaka mitano, Serikali yetu sikivu ya Awamu ya Tano imetekeleza ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji 1,423. Kati ya miradi hiyo, 792 imekamilika ikihusisha miradi 710 vijijini na miradi 82 mijini. Vilevile, Serikali ilipokea ombi la Waheshimiwa Wabunge na kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Maji na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Lengo la Serikali ni kuhakikisha vyombo hivi vinakuwa chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi ya maji na kusimamia utoaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira. Juhudi hizi kwa pamoja zitasaidia kusogeza huduma ya maji kwa kasi zaidi karibu na wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini.

32.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha takriban miaka mitano, Serikali imefanikiwa kulinda na kuendeleza rasilimali na maliasili za Taifa hususan madini na kuhakikisha zinatumika kwa maslahi mapana ya Taifa na watu wake. Mafanikio hayo, yametokana na Serikali kutekeleza kwa ufanisi mkubwa Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Utajiri na Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Utajiri na Maliasili za Nchi ya Mwaka 2017.

33.            Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mkakati na sheria hiyo umechangia kuongezeka kwa maduhuli ya Serikali yatokanayo na sekta ya madini mwaka hadi mwaka. Maduhuli ya Serikali yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 205.2 Mwaka 2015/2016, hadi Shilingi bilioni 346.6 Mwaka 2018/2019. Aidha, katika Mwaka 2019/2020 Serikali inatarajia kukusanya Shilingi bilioni 471.

34.            Mheshimiwa Spika, ukusanyaji wa mapato nao umeongezeka kutoka wastani wa Shilingi bilioni 850 kwa mwezi Mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa Shilingi trilioni 1.3 Mwaka 2019. Ongezeko hili limechangiwa na hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali hususan kuimarisha matumizi ya mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki, kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato. Aidha, ongezeko hilo limekuwa chachu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imesaidia kuimarisha utoaji wa huduma pamoja na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

35.            Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi na walipa kodi wote kwa kuendelea kuitikia wito wa Serikali wa kulipa kodi kwani hatua hiyo ni muhimu katika kulifanya Taifa letu kujitegemea. Serikali itaendelea kusimamia matumizi kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

36.            Mheshimiwa Spika, Serikali pia imefanikiwa kudhibiti matumizi ya hovyo ya fedha za Umma kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi sambamba na kuhakikisha kwamba wale wote wanaotakiwa kulipa kodi wanafanya hivyo. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitano (2015 – 2019), Serikali imeweza kuokoa Shilingi bilioni 19.83 ya mishahara kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo watumishi hewa 19,708 na wenye vyeti vya kughushi 15,411. Msingi huu tunaojenga ni muhimu katika kujenga uchumi imara na usio tegemezi.

37.            Mheshimiwa Spika, katika siku ya Mashujaa iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma tarehe 25 Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza na kusisitiza azma ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo alisema, nanukuu:
“.......ninazungumza kutoka kwenye dhamira yangu kabla sijamaliza kipindi changu cha miaka mitano Serikali yote itakuwa hapa Dodoma.....”

38.            Mheshimiwa Spika, ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na watanzania kuwa tayari Serikali imehamia Dodoma. Hadi Machi 2020, jumla ya watumishi 15,361 wa Wizara na Taasisi za Serikali wamehamia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, ujenzi wa awali wa ofisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba umekamilika, maandalizi ya ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali awamu ya pili na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika mji huo unaendelea. Vilevile, Serikali imekamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma ambao niliuzindua tarehe 13 Februari 2020 kwa ajili ya kusimamia shughuli za upangaji wa Jiji la Dodoma. Naielekeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha Jiji la Dodoma linaendelezwa kwa kuzingatia Mpango huo.

39.            Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa katika usimamizi madhubuti wa sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma. Usimamizi huo, umewezesha viongozi na watendaji wa umma kuwajibika ipasavyo kwa wananchi ambao ndiyo waajiri wao. Sambamba na hilo, nidhamu Serikalini imeongezeka kutokana na Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wazembe, wadanganyifu na wasio waadilifu.

40.            Mheshimiwa Spika, tunapotaja mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani uongozi wake mahiri na wenye uthubutu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio yaliyopatikana. Dhana na falsafa aliyojenga ya Hapa Kazi Tu imesaidia kubadili mtazamo wa Watanzania wengi ambapo sasa tunashuhudia uwajibikaji wa kiwango cha juu wa mtu mmoja mmoja, katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni na kwingineko badala ya tabia ya awali ya baadhi ya wananchi wachache kupoteza muda mwingi katika shughuli zisizokuwa na tija kwa Taifa.

41.            Mheshimiwa Spika, mafanikio haya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za jamii yameenda sambamba na uzalishaji wa ajira zipatazo milioni 12.6 zikiwemo ajira za moja kwa moja milioni 11.7 kwenye sekta mbalimbali nchini. Kwa mfano:
·                 Sekta za Afya, Elimu na Utawala zimetoa ajira za kudumu kwa kuajiri watumishi 28,403 katika mamlaka za Serikali za Mitaa,
·                 Mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa umewezesha kuzalishwa ajira zipatazo 13,177 za kitaalam na zisizo za kitalaam. Kati ya hizo, ajira za kitaalam kwa wazawa ni asilimia 46.5. Pia kupitia mradi huu kumekuwa na utoaji wa zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 664.7 kwa wazabuni na wakandarasi wa ndani 640,
·                 Mradi wa umeme wa mwalimu Nyerere kupitia maporomoko ya mto Rufiji umezalisha jumla ya ajira 3,897 ikiwemo ajira za wazawa 3,422,
·                 Ufufuaji wa shirika la ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na kuboresha viwanja vya ndege jumla ya ajira 2,970,
·                 Ujenzi wa Viwanda nchini jumla ya ajira zilizozalishwa ni 41,900.
·                 Ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Hospitali za Wilaya, vituo vya afya, Zahanati, Madarasa, Nyumba na majengo maeneo mapya ya utawala, Miradi ya barabara chini ya TARURA kwa kutumia force Account jumla ya mafundi 845,348 walipata ajira za mikataba na muda.

42.            Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza mafanikio hayo, nyote ni mashuhuda kwamba Chama Cha Mapinduzi kiliahidi na kimetekeleza kwa vitendo na ndiyo maana kinaendelea kuwa Chama cha mfano na cha kuigwa siyo tu Nchini, bali hata katika Bara la Afrika. Hata hivyo, mafanikio mengine yataelezwa kwa kina wakati Mawaziri watakapokuwa wanawasilisha hotuba za bajeti za Wizara zao.

43.            Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/2020 na shughuli zitakazotekelezwa na Serikali katika Mwaka 2020/2021.

 

MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI YA MWAKA 2020/2021

44.            Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2020/2021 yamezingatia Sera na Miongozo ikiwa ni pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/2021. Mpango huu ni wa mwisho katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka wa kutekeleza Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) wenye dhima ya Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu.

45.            Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo na Bajeti wa Mwaka 2020/2021 umezingatia yafuatayo: Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 yenye lengo la kuiwezesha Tanzania kuwa Nchi ya hadhi ya uchumi wa kipato cha kati inayoongozwa na viwanda ifikapo Mwaka 2025; Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/2017 – 2020/2021; Sera na Mikakati mbalimbali; Malengo ya Maendeleo Endelevu na Makubaliano ya Kikanda na Kimataifa ambayo Serikali imeyaridhia. Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 - 2020 imezingatiwa pamoja na Maelekezo ya Serikali yaliyoainishwa na Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi rasmi wa Bunge la 11 mwezi Novemba 2015. Vilevile, Mpango umezingatia hali halisi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2019/2020; changamoto zilizojitokeza; hali ya uchumi kitaifa, kikanda na kidunia kwa Mwaka 2019 na maoteo ya ukuaji wa uchumi kwa Mwaka 2020.

46.            Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2020/2021 ambavyo vimejikita katika masuala makuu manne yafuatayo: Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda; Kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; Uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji na Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo. Katika kufikia malengo ya Mpango, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika kutekeleza miradi ya kielelezo ya kimkakati ikiwa ni pamoja na: Ujenzi wa Reli ya Kati ya Kiwango cha Kimataifa; Mradi wa kufua umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL); Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Uanzishwaji wa kanda maalum za Kiuchumi na Kusomesha wataalam wengi zaidi katika fani za Ujuzi Adimu na Maalum. Hatua hizo, zitasaidia kufungamanisha ujenzi wa miundombinu wezeshi na sekta nyingine za kiuchumi ili kuongeza kasi ya maendeleo, ajira na kipato na hatimaye kuliwezesha Taifa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

47.            Mheshimiwa Spika,  nitumie fursa hii kutoa rai kwa Wafanyabiashara, Wawekezaji, Wajasiriamali, Wabunge, Viongozi na Watendaji wa Serikali, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo, na Wananchi wote kwa ujumla, kushirikiana na Serikali bega kwa bega katika kutekeleza Mpango huu ili azma ya kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo Mwaka 2025 iweze kutimia.

HALI YA UCHUMI

48.            Mheshimiwa Spika, uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2019, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia asilimia 6.9. Baadhi ya shughuli zilizochangia ukuaji huo kwa viwango vikubwa ni pamoja na ujenzi asilimia 14.8; uchimbaji wa madini na mawe asilimia 12.6; habari na mawasiliano asilimia 11.0; uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 8.8 na huduma za usambazaji maji asilimia 8.5.

49.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Januari 2020, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 3.7. Kiwango hiki ni chini ya lengo la Taifa la kipindi cha muda wa kati la asilimia 5.0, na chini ya malengo ya asilimia 7.0 kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na asilimia 8.0 kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na za bajeti, uhakika wa upatikanaji wa chakula na utulivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine duniani.

50.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha sekta za uzalishaji na utoaji huduma ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa. Vilevile, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati na sera za uchumi jumla ili kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuwa na mwenendo tulivu wa uchumi. Serikali pia, itaendelea kuimarisha Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG) kwa kuharakisha ufungaji wa mfumo huo katika wizara na taasisi za Serikali.

HALI YA SIASA

51.            Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na maadili ya vyama vya siasa ili kuhakikisha demokrasia ya vyama vingi inaimarika pamoja na kudumisha amani, utulivu na mshikamano uliopo katika nchi yetu.

52.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kusimamia utekelezaji na utoaji elimu kuhusu Sheria ya Vyama vya Siasa, Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, pamoja na Sheria ya Gharama za Uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Vilevile, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kufuatilia uhai wa Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu kwa lengo la kuwawezesha wananchi kushiriki na kutoa michango yao ya mawazo na fikra kupitia vyama hivyo ili kuimarisha demokrasia na maendeleo nchini.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

53.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika tarehe 24 Novemba 2019. Uchaguzi huo ulihusisha Mitaa 4,263, Vijiji 12,319 na Vitongoji 64,384. Katika uchaguzi huo, Chama Cha Mapinduzi kilipata ushindi wa kishindo wa asilimia 99.9 kwa nafasi zote zilizogombewa. Matokeo hayo yameendelea kudhihirisha imani kubwa waliyonayo wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi. Hivyo, basi natoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ili kutimiza azma ya kuwaletea maendeleo.

Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu

54.            Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2020. Pamoja na mambo mengine, maandalizi hayo yanahusisha Zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika nchi nzima. Awamu ya kwanza ilizinduliwa tarehe 18 Julai, 2019 Mkoani Kilimanjaro na kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

55.            Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa daftari hili ulihusisha: Uandikishaji wa Wapiga Kura wapya ambao wametimiza umri wa miaka 18 au watatimiza umri huo ifikapo siku ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; urekebishaji wa taarifa za Wapiga Kura walioandikishwa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 pamoja na ufutaji wa taarifa za Wapiga Kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

56.            Mheshimiwa Spika, katika zoezi hilo, jumla ya Wapiga Kura 10,285,732 wameandikishwa na kati yao, Wapiga Kura wapya ni 7,043,247, Wapiga Kura walioboreshewa taarifa zao ni 3,225,778 na Wapiga Kura waliofutwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutokana na kupoteza sifa ni 16,707. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Awamu ya Pili linatarajiwa kuanza tarehe 5 Aprili 2020 na kukamilika tarehe 26 Juni 2020. Zoezi hili litaenda sambamba na uhakiki wa taarifa za wapiga kura katika daftari hilo. Natoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo, ili waweze kutumia haki yao ya Kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.

57.            Mheshimiwa Spika, niwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Nchi. Viongozi wa Vyama vya Siasa waoneshe mfano wa kuendesha siasa za kistaarabu zenye lengo la kuwaunganisha watanzania na siyo kuwatenganisha. Hakuna kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha mifarakano. Hivyo basi, tudumishe utulivu, amani, mshikamano pamoja na ustaarabu wetu wa kitanzania katika kipindi chote cha kampeni na Uchaguzi Mkuu ili kulifanya Taifa letu kuendelea kuwa kisiwa cha amani na mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

BUNGE

58.            Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kikanuni kwa kufanya mikutano mitatu na huu ukiwa ni wa nne kwa mwaka 2019/2020. Ofisi ya Bunge kwa sasa inatekeleza shughuli za Bunge kwa kutumia TEHAMA kupitia mfumo wa Bunge Mtandao (e-Parliament) uliotengenezwa na kusimamiwa na wataalam wa ndani wa Ofisi ya Bunge. Hivi sasa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zinawasilisha taarifa na nyaraka mbalimbali Bungeni kwa kutumia nakala tete badala ya nakala ngumu.  Hatua hii imeweza kupunguza gharama za uendeshaji hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha cha takribani Shilingi bilioni 2 kilichokuwa kinatumika kila mwaka katika uandaaji na uhifadhi wa nyaraka mbalimbali zinazoandaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Bunge. Pia, Ofisi ya Bunge imeweza kuzindua ‘Bunge Mobile Application’ ambayo imewezesha Waheshimiwa Wabunge pamoja na wadau mbalimbali kupata kwa urahisi taarifa mbalimbali kama vile orodha ya shughuli za Bunge (Order Paper), Hansard pamoja na sheria na miswada. Ni matumaini yangu kwamba Bunge lako Tukufu litaendelea kuisimamia Serikali ili itekeleze majukumu yake ipasavyo.

 

MAHAKAMA

59.            Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa gharama nafuu, Mahakama imeendelea kuimarisha huduma kwa kuweka mifumo na taratibu mbalimbali za kuwafikia wananchi katika maeneo yote nchini ili kupunguza mlundikano wa mashauri. Mojawapo ya utaratibu unaotumika ni kuwatumia Mahakimu wenye Mamlaka ya Ziada (Extended Jurisdiction) kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu ambapo Mahakimu 195 walipewa Mamlaka hiyo ya ziada. Katika kipindi cha Mwaka 2019 mashauri 1,132 yalisikilizwa na kumalizwa kwa utaratibu huo.

60.            Mheshimiwa Spika, Mahakama imeendelea kuboresha miundombinu katika ngazi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo. Katika kutekeleza hilo, ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika Mikoa ya Kigoma na Mara, Mahakama ya Hakimu Mkazi katika Mikoa ya Simiyu, Manyara, Geita, Njombe, Mahakama za Wilaya 14, pamoja na Mahakama za Mwanzo za Mlowo, Magoma, Uyole, Mtowisa, Msanzi na Mkunya umekamilika.

61.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kulinda, kuheshimu na kuzingatia haki za binadamu na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa sheria na utoaji Haki kwa kutumia TEHAMA. Vilevile, Serikali itaendelea kufanya maboresho katika mfumo wa Haki Jinai ili kuwezesha shughuli za uchunguzi, upelelezi, uendeshaji wa mashauri na usikilizaji wa mashauri kufanyika kwa ufanisi.

UWEKEZAJI

62.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu na kusimamia shughuli za kuhamasisha na kufanikisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia mitaji, teknolojia na ujuzi ambao ni chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali. Serikali imeendelea kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na biashara yanakuwa rafiki.

63.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutumia vyema uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji na kuwepo kwenye eneo la kimkakati la kijiografia kwa kuhudumia nchi zipatazo 6 ambazo hazipo kwenye mwambao wa bahari. Hali hii inaifanya nchi yetu kuwa lango la biashara ya kimataifa hususani katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati pamoja na Kusini mwa Afrika. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mazingiza ya uwekezaji na biashara ikiwemo kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 ili kubaini changamoto za kisera, kisheria na kiutendaji zitakazopelekea kuhuisha Sera ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997.

64.            Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint) ambapo kupitia Mpango huo Serikali imefuta tozo mbalimbali 54 katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 pamoja na kuondoa mwingiliano wa majukumu kati ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ili kurahisisha shughuli za uwekezaji na biashara.

65.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020 Serikali pia imeratibu mikutano ya mashauriano kati yake na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo. Katika mikutano hiyo hoja nyingi na changamoto zilipatiwa ufumbuzi na nyingine kutolewa ufafanuzi ambapo pia wafanyabiashara na wawekezaji walikumbushwa wajibu wao katika uendeshaji biashara na uwekezaji wao.

66.            Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliendesha mikutano kati ya Serikali na wawekezaji kutoka China, Uingereza na Marekani waliowekeza hapa nchini. Kwa nia ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili na kupata maoni na ushauri zaidi.

67.            Mheshimiwa Spika, katika kuongeza njia za kushughulikia malalamiko ya wawekezaji, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeandaa mfumo wa kielektroniki wa kupokea malalamiko na kupata mrejesho wa wawekezaji (Online Complaints and Feedback Platform) ambao utaanza kutumika katika Mwaka 2020/2021. Mfumo huo utapokea maoni na ushauri kwa njia ya haraka na kuleta ufanisi katika kuwahudumia.

68.            Mheshimiwa Spika, Mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini yameendelea kuimarika. Taarifa ya Benki ya Dunia ya Wepesi wa Kufanya Biashara (Ease of Doing Business Report) ya Mwaka 2020 iliyotolewa Oktoba 2019 inaonesha kuwa Tanzania imepanda kwa nafasi tatu (3) kutoka nafasi ya 144 hadi kufikia nafasi ya 141. Lengo letu ni kufikia nafasi ya juu kufikia Mwaka 2025. Naziagiza Wizara na Taasisi zote za Serikali zinazohusika na utekelezaji wa maboresho na kuweka mazingira mazuri na rafiki ya kuratibu kwa ukaribu ili kufungua fursa zaidi.

69.            Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kukuza uwekezaji, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuhamasisha Mikoa yote nchini kuandaa Makongamano ya Uwekezaji sambamba na kuzindua Miongozo ya Uwekezaji ya Mikoa inayobainisha fursa za uwekezaji za Mikoa pamoja na maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa ili kuhamasisha na kuvutia uwekezaji zaidi katika Mikoa hiyo. Hadi sasa, Mikoa 14 ya Ruvuma, Songwe, Pwani, Lindi, Kagera, Mtwara, Geita, Kilimanjaro, Simiyu, Manyara, Dodoma, Mwanza, Kigoma na Morogoro imezindua miongozo hiyo. Mikoa yote ambayo haijakamilisha kuandaa miongozo hiyo ifanye hivyo kabla ya Septemba 2020.
70.            Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu makongamano ya uwekezaji yaliyofanyika hapa nchini kama vile Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uganda,  Tanzania na Afrika Kusini; Afrika Mashariki na Sweden na Makongamano mengine yaliyofanyika nje ya Nchi kama vile Tanzania na Burundi; “Investment for Africa” lililofanyika nchini Misri; Kongamano lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) lililofanyika Afrika Kusini; na Kongamano kati ya Pakistani na Afrika lililofanyika nchini Kenya. Tumeendelea kupokea wawekezaji wanaofika nchini kwa ajili ya kutafuta fursa za uwekezaji kutoka Nchi mbalimbali.

71.            Mheshimiwa Spika, Serikali inahakikisha maeneo ya uwekezaji yanatengwa na kuendelezwa kwa kuwekewa miundombinu ya msingi ya maji, umeme, mawasiliano na barabara. Hadi Februari 2020, jumla ya hekta 854,821.61 zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri zote nchini.

72.            Mheshimiwa Spika, kupitia kitengo cha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre) kilichopo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) chenye watendaji kutoka Taasisi 10 wameendelea kutoa huduma za muda mfupi kwa wawekezaji wetu kupitia Kituo hicho hadi kufikia Februari 2020, jumla ya miradi 146 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1,514.57 inayotegemewa kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 26,384 ilisajiliwa ambapo miradi 52 sawa na asilimia 36 inamilikiwa na wageni, miradi 50 sawa na asilimia 34 inamilikiwa na Watanzania na miradi 44 sawa na asilimia 30 inamilikiwa kwa ubia kati ya wageni na Watanzania. Katika miradi iliyosajiliwa katika Mwaka huu wa Fedha miradi 95 sawa na asilimia 65 ya miradi yote inahusisha sekta ya uzalishaji viwandani.

 

SEKTA ZA UZALISHAJI

Viwanda

73.            Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa viwanda Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuwezesha sekta hii kukua kwa haraka na kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa pamoja na kupunguza umaskini. Katika kutekeleza dhana hii kwa vitendo katika mwaka 2019/2020, Serikali iliimarisha kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi cha Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani) ili kuongeza uzalishaji ikiwemo wa magari ya zimamoto. Vilevile, ada na tozo 54 zilifutwa ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta hii. Aidha, uzalishaji katika baadhi ya viwanda ulianza ikiwa ni pamoja na Pipe Industries Co. Limited (Dar es Salaam), Kiwanda cha Chai cha Kabambe (Njombe), kiwanda cha Yalin Cashewnut Co. Limited (Mtwara), kiwanda cha 21st Century Food and Packaging (Dar es Salaam), kiwanda cha kusaga mahindi (MeTL, Dar es Salaam), kiwanda cha bidhaa za plastiki cha Plasco Pipelines Co. Ltd (Dar es Salaam), kiwanda cha kupakia na kuhifadhi parachichi, Rungwe Avocado na kiwanda cha kuchakata parachichi kwa ajili ya kutengeneza mafuta (KUZA Afrika).

74.            Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali za kujenga uchumi wa viwanda, jumla ya viwanda vipya zaidi ya 4,000 vimejengwa katika mikoa mbalimbali. Viwanda vilivyojengwa vinazalisha bidhaa za ujenzi; pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo nafaka, matunda, mafuta ya kupikia na bidhaa za ngozi. Ujenzi wa viwanda vipya nchini, katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano, umechangia kupatikana kwa ajira mpya 482,601 nchi nzima.

75.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuondoa kero zinazokwamisha ufanisi na ukuaji wa sekta ya viwanda. Aidha, Serikali itaimarisha ushindani katika soko kwa kuzingatia sheria na kanuni za ushindani sawa hususan wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kama vile nondo, mabomba ya plastiki, nguo na mavazi, bidhaa za ngozi na marumaru. Lengo ni kuimarisha msingi wa ukuaji wa sekta ya viwanda nchini pamoja na kuvutia sekta binafsi kuwekeza au kushirikiana na Serikali kuwekeza kwenye viwanda.

 

Kilimo

76.            Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, kupambana na umaskini, kuongeza ajira pamoja na kuleta maendeleo ya Nchi kwa ujumla. Kwa kulitambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata pembejeo na zana za kisasa ili kuongeza tija katika kilimo na hivyo kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Hali ya Upatikanaji wa Chakula

77.            Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine hususan kuimarika kwa hali ya hewa, mageuzi yanayofanywa katika sekta ya kilimo, yamechangia kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini na upatikanaji wa malighafi za viwanda, sambamba na kuongeza tija kwa wakulima. Katika msimu wa kilimo wa Mwaka 2018/2019, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 16.3 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 13.6. Uzalishaji huo umeihakikishia Nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 118 kwa msimu wa kilimo wa Mwaka 2019/2020.

 

Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo

78.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya pembejeo na mbinu bora za kilimo na teknolojia kwa lengo la kukifanya kilimo chetu kuwa cha kisasa zaidi na chenye tija. Hadi kufikia Februari 2020, upatikanaji wa mbegu bora za mazao umefikia tani 71,207 ikilinganishwa na tani 57,023 za msimu wa Mwaka 2018/2019. Kati ya mbegu hizo, tani 66,031 zimezalishwa nchini ambayo ni sawa na asilimia 93 na tani 5,175 sawa na asilimia 7 zimeingizwa kutoka nje ya nchi.


79.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa mbolea nchini kwa kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja ambao umesaidia kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima. Kutokana na mfumo huo, upatikanaji wa mbolea hadi Februari 2020 umefikia tani 516,813 sawa na asilimia 89 ya lengo la tani 586,604. Kwa kuwa mbolea hizo hutumika kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji wa mazao, Serikali inaendelea kuhakikisha asilimia 11 iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati. Aidha, Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa viuatilifu ambapo hadi Januari 2020, jumla ya tani 8,719 za viuatilifu zimeingizwa nchini ili kudhibiti visumbufu vya mimea na mazao.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB)

80.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imetoa mikopo ya Shilingi bilioni 34 kwa miradi ya kilimo 38 na kufanya jumla ya mikopo iliyotolewa kufikia Shilingi bilioni 160.6 toka Benki ilipoanza utoaji wa mikopo. Mikopo iliyotolewa imewanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa wapatao milioni 2.1 wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na viwanda vidogo vya uchakataji wa mazao.

81.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho TADB imetoa mikopo ya ziada ya Shilingi bilioni 31.77 kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo. Mikopo hiyo imewanufaisha wakulima wapatao 5,080, biashara ndogo na za kati za kilimo zipatazo 30, Vyama vya Msingi (AMCOS) 20 katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na kufanikisha ununuzi wa matrekta 19 katika mikoa hiyo.

Uzalishaji wa Zao la Chikichi

82.            Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kuendeleza zao la chikichi sambamba na mazao mengine yanayozalisha mafuta. Uendelezaji wa zao la chikichi unahusisha kupanda kwa wingi miche mipya yenye uzalishaji wenye tija. Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) imeanza uzalishaji wa mbegu bora za chikichi aina ya TENERA inayotoa mafuta mengi. Lengo ni kuzalisha mbegu bora na za kutosha zitakazowezesha wakulima kuongeza uzalishaji na hivyo kujiongezea kipato na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

83.            Mheshimiwa Spika, hadi tarehe 15 Februari 2020, mbegu 1,525,017 zimezalishwa ambazo zitatosha kupanda eneo la ekari 30,500. Tayari mbegu 1,026,111 zimesambazwa kwa ajili ya kuziotesha ili miche bora iweze kusambazwa kwa wakulima. Usambazaji kwa ajili ya uoteshaji umefanyika katika halmashauri za mkoa wa Kigoma na taasisi nyingine ikiwemo Magereza ya Kwitanga na Ilagala na JKT Bulombora.

84.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ugani, kilimo cha umwagiliaji, ushirika na upatikanaji wa pembejeo ikiwa ni pamoja na mbegu bora za mazao. Aidha, itajenga na kukarabati miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko.

Zao la Mkonge
85.            Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi kuwa zao la Mkonge lilikatiwa tamaa na wakulima na wakulima wengi waliacha kulima zao hili. Serikali imeanza kuchukua hatua za kufufua kilimo cha Mkonge na masoko yake. Tunafufua mamlaka ya Mkonge ili itambue mashamba yake na mali zingine ili ianze kuhamasisha wakulima wadogo na wakubwa na kukaribisha uwekezaji wa sekta ya Mkonge. Tunaimarisha Taasisi ya Utafiti ya Mlingano ili izalishe miche zaidi na kuisambaza kwa wakulima. Natoa wito kwa Wizara, Wakuu wa Mikoa inakolima Mkonge kutambua wakulima wa Mkonge na wapate msaada wa kitaalam.

Mifugo

86.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya mifugo nchini ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa na kutoa fursa za ajira. Ili kufikia lengo hili, Serikali imehamasisha wafugaji kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa, kuchakata bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani, ikiwemo lishe bora na kuuza nje pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi. Aidha, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imekarabati majosho 292, inaendelea na ukarabati wa majosho 207 na kuendelea na ujenzi wa majosho mapya 84 katika halmashauri mbalimbali nchini. Hatua hii imewezesha kuongezeka kwa majosho yanayofanya kazi kutoka 1,486 Mwaka 2018/2019 hadi majosho 1,738 Mwaka 2019/2020. Aidha, Serikali imenunua lita 12,549 za dawa za kuogesha mifugo.

87.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021 Serikali itaendelea kuhimiza ufugaji wa kisasa pamoja na kuimarisha afya ya mifugo kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za chanjo na tiba kwa kuimarisha vituo vya utengenezaji wa chanjo za mifugo. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa malisho kwa kutambua, kutenga, kumilikisha, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho. Vilevile, huduma za ugani zitaboreshwa na mafunzo kwa wafugaji na maafisa ugani yatatolewa ili kuwapatia maarifa na teknolojia mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija.

Uvuvi

88.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha Sekta ndogo ya Uvuvi ili iweze kuchangia kikamilifu katika Pato la Taifa na ajira kwa ujumla. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuondolewa kwa kodi katika zana na malighafi za uvuvi, kupambana na uvuvi haramu, kuboreshwa kwa mialo ya kupokelea samaki na kuwa ya kisasa, kuhamasisha uwekezaji katika ukuzaji wa viumbe maji pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kuchakata samaki.

89.            Mheshimwia Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaimarisha sekta ya uvuvi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa na kuwaongezea wavuvi kipato. Hatua zitakazochukuliwa zitahusisha, utekelezaji wa Mkakati wa kujenga na kuboresha miundombinu ya uvuvi, mkakati wa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania, kuweka mazingira bora katika uvuvi wa bahari kuu kwa kuweka vivutio kwa wawekezaji, kuendelea kupambana na wavuvi haramu na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi, uhifadhi na uchakataji wa samaki ili kuimarisha mnyororo wa thamani.

Utalii

90.            Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii nchini imeendelea kuimarika ikichagizwa pamoja na mambo mengine na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji na utoaji huduma. Katika Mwaka 2019, idadi ya watalii walioingia nchini ilifikia 1,510,151 ikilinganishwa na 1,505,702 Mwaka 2018. Ongezeko la idadi ya watalii nchini limeongeza mapato ya Serikali yatokanayo na utalii kutoka Dola za Marekani bilioni 2.4 Mwaka 2018 hadi Dola za Marekani bilioni 2.6 Mwaka 2019.

91.            Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kuimarisha shughuli za utalii nchini, Serikali imepandisha hadhi Mapori ya Akiba 6 ambayo ni Burigi (Chato), Ibanda (Kyerwa), Rumanyika (Karagwe), Nyerere, Mto Ugalla na Kigosi kuwa Hifadhi za Taifa. Lengo ni kuimarisha Sekta ya Utalii kwa kuwa na maeneo mengi ya hifadhi na vivutio vya watalii yatakayosaidia kuongeza wigo wa utalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo.

92.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuvitangaza vituo vya utalii ndani na nje ya nchi hususan kwenye masoko ya kimkakati, kuimarisha hifadhi mpya 6 za Taifa, kukuza wigo wa mazao ya utalii na kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi ishiriki kikamilifu katika uwekezaji kwenye utalii. Kadhalika, maeneo mengine yatakayopewa kipaumbele ni utalii wa meli, mikutano, fukwe, utamaduni, malikale, ikolojia na jiolojia.

Madini

93.            Mheshimiwa Spika, usimamizi mzuri wa mikakati na sheria za ulinzi wa rasilimali na maliasili zetu umekuwa chachu ya kukua na kuimarika kwa sekta ya Madini nchini. Usimamizi huo umeifanya sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa. Mathalan, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2019/2020 mchango wa Sekta ya madini ulikuwa asilimia 13.7. Katika kipindi hicho, sekta ya madini ilishika nafasi ya pili katika kuchangia Pato la Taifa baada ya sekta ya ujenzi iliyochangia asilimia 16.5.

94.            Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Januari 2020, maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kupitia Sekta ya Madini ni Shilingi bilioni 284.4. Kiwango hicho ni sawa na asilimia 60.4 ya lengo la mwaka la kukusanya Shilingi bilioni 470.89. Mafanikio hayo, ni ishara tosha ya kuendelea kuimarika kwa sekta hii kufuatia usimamizi thabiti unaowekwa na Serikali.

95.            Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi za mauzo ya madini, kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika, kupata bei stahiki kwa bidhaa za madini na kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara haramu ya madini. Hatua hiyo imewezesha kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia tozo za mrabaha na ada ya ukaguzi wa mauzo ya madini kwenye masoko.

96.            Mheshimiwa Spika, hadi Januari 2020, jumla ya masoko ya madini 28 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 28 vimeanzishwa nchini. Kupitia masoko na vituo hivyo, katika kipindi cha Machi 2019 hadi Januari 2020, jumla ya kilogramu 9,237.34 za dhahabu; karati 12,973.14 za madini ya almasi; kilogramu 20,099.17 za madini ya bati na kilogramu 514,683.28 za madini ya vito mbalimbali ziliuzwa na kuipatia Serikali mapato ya Shilingi bilioni 66.57 ambazo zimetokana na mrabaha, ada ya ukaguzi na ushuru wa Halmashauri.

97.            Mheshimiwa Spika, masoko ya madini yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake. Masoko hayo, yana ulinzi na usalama wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha biashara ya madini. Hivyo, natoa rai kwa wadau wa ndani na nje ya nchi kutumia masoko na vituo hivyo ambavyo vinaendeshwa kwa misingi ya kisheria kwa kuzingatia ushindani na uwazi wa kibiashara.

98.            Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha uchimbaji mdogo na wa kati wa madini nchini; ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini; kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini; kuimarisha shughuli za ugani na utafiti, uongezaji thamani madini na masoko.

Nishati

99.            Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa umeme nchini imeendelea kuimarika na kuchangia katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa kwa ujumla. Uwezo wa mitambo ya kufua umeme nchini ni Megawati 1,602.32 ambapo kati ya hizo Megawati 1,565.72 zipo katika Mfumo wa Gridi ya Taifa na Megawati 36.6 zipo nje ya Mfumo wa Gridi ya Taifa. Aidha, hali ya maji katika mabwawa ya Mtera, Kidatu, Kihansi, Nyumba ya Mungu na New Pangani Falls imeendelea kuwa nzuri na hivyo kutuhakikishia kuwa na umeme wa uhakika.

100.         Mheshimiwa Spika, pamoja na kuelezea juu ya mafanikio tuliyoyapata katika utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere hapo awali, Serikali vilevile inatekeleza Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rusumo utakaozalisha Megawati 80. Kukamilika kwa miradi hii na mingine itaimarisha upatikanaji wa umeme nafuu na wa uhakika na hivyo kuchangia katika maendeleo ya ukuaji wa viwanda na uchumi.

101.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa na ya kielelezo ya uzalishaji wa umeme hususan Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115), upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi I (MW 185) pamoja na kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini ili kuhakikisha vijiji vilivyobaki vinapatiwa umeme.

HUDUMA ZA KIUCHUMI

Ardhi

102.         Mheshimiwa Spika, ardhi ni rasilimali namba moja katika kuifikia ndoto ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda. Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kusimamia upimaji wa ardhi, mipango ya matumizi ya ardhi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa na umilikishaji ardhi kwa wananchi. Sambamba na kuimarisha utoaji huduma kwa njia ya kielektroniki, Serikali inatekeleza mpango wa kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi. Hadi sasa ofisi za ardhi za mikoa 26 zimeanzishwa pamoja na kuendelea kuziimarisha ofisi zote za ardhi za Halmashauri kwa kuwapatia mafunzo wataalam wa sekta ya ardhi na kununua vifaa.

103.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya usimikaji wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi katika Ofisi za Ardhi Kanda ya Dar es Salaam na Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo. Lengo ni kuharakisha upimaji na utoaji hatimiliki za ardhi ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki ardhi kisheria na kutumia hati hizo kupata mikopo katika taasisi za fedha itakayowezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Mipango ya Matumizi ya Ardhi

104.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi ya Kanda, Wilaya na Vijiji. Lengo la Serikali ni kuharakisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara na uwekezaji. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020, mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 132 imeandaliwa katika Wilaya 27.

105.         Mheshimiwa Spika, sambamba na uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Serikali imeendelea kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali. Katika Mwaka 2019/2020 Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametoa kibali kwa vijiji 920 kati ya vijiji 975 vilivyokuwemo ndani ya hifadhi na mapori ya akiba kuhalalishwa rasmi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii. Hatua hiyo itapunguza migogoro iliyokuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwawezesha wananchi kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji.

 

Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji

106.         Mheshimiwa Spika, sekta ya miundombinu hususan ya usafiri na usafirishaji ndio kiunganishi cha sekta za uchumi wa nchi ili kuwezesha shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika jamii. Kuimarika kwa sekta hii, ni kichocheo muhimu katika kukua kwa uchumi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

107.         Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sekta hii Serikali ya Awamu ya Tano ilichukua hatua za makusudi kuanza ujenzi mkubwa wa barabara, madaraja, vivuko, ufufuaji na ujenzi wa reli mpya, uimarishaji  wa usafiri wa majini, na uboreshaji wa usafiri wa anga ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kurahisisha huduma za uchukuzi na usafirishaji wa watu na bidhaa.

Barabara na Madaraja

108.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imepata mafanikio makubwa katika kujenga mtandao wa barabara za kiwango cha lami nchini. Serikali imeendelea kuhakikisha mikoa yote inaunganishwa na mtandao wa barabara za lami ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

109.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho jumla ya kilomita 399.07 za barabara kuu na barabara za mikoa zilijengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, kilomita 56 za barabara kuu zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango cha lami na kilomita 84 za barabara za mikoa zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango cha changarawe. Hadi kufikia Februari 2020, jumla ya kilomita 6,960 zimefanyiwa matengenezo ya kawaida, kilomita 1,444 zimefanyiwa matengenezo maalum na madaraja 416 yamefanyiwa matengenezo.

110.         Mheshimiwa Spika, katika kuondoa msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya njia 8 kutoka Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa Kilomita 19 ambapo ujenzi umefikia asilimia 63. Mradi mwingine ni ujenzi wa Ubungo Interchange ambao umefikia asilimia 65.

111.         Mheshimiwa Spika, miradi mingine inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Tanzanite (Salender) lenye urefu wa Kilomita 6.2 uliofikia asilimia 25 na kuanza maandalizi ya ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45. Aidha, kati ya Julai 2019 hadi Januari 2020 Serikali imetoa Shilingi bilioni 703.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja nchini.

112.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa niliyoitaja pamoja na mingine inayoendelea. Vilevile, Serikali itaanza ujenzi wa barabara na madaraja mapya ili kuwahakikishia wananchi, wawekezaji na wafanyabiashara huduma bora na za uhakika za usafirishaji katika kipindi chote cha mwaka.

Reli  

113.         Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, moja ya mafanikio makubwa tuliyoyapata katika eneo la reli ni kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa. Nikiri pia kuwa, katika kipindi hiki, Serikali inajivunia kurejesha huduma ya reli kati ya Dar es Salaam na Moshi ambayo ilisimama kwa zaidi ya miaka 20 na kufufuliwa kwa huduma ya reli kati ya Tanga na Moshi iliyosimama kwa takribani miaka 12 ambapo hadi Machi 2020 jumla ya abiria 33,459 na mizigo tani 5,080 imesafirishwa kupitia reli hizo. Aidha, ukarabati wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka nao unaendelea kwa kuondoa reli zote nyepesi na kuweka reli mpya nzito. Ukarabati huo umewezesha kurejea kwa huduma za usafiri wa abiria na mizigo na hivyo kurahisisha usafirishaji, kupunguza kero ya usafiri na ajali za barabarani.

114.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itakamilisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro na kuendelea na ujenzi wa kipande cha Morogoro – Makutupora sambamba na kukarabati miundombinu mingine ya reli.

Bandari

115.         Mheshimiwa Spika, katika eneo la bandari, Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu ya bandari zilizopo katika mwambao wa pwani na maziwa kwa lengo la kuendeleza huduma ya usafiri wa majini ndani ya nchi na nchi jirani. Katika Mwaka 2019/2020, Serikali imekamilisha ujenzi wa gati namba 1, 2, 3 na gati la kupakia na kupakua magari (RoRo Berth) katika Bandari ya Dar es Salaam. Kazi ya ukarabati wa gati namba 5 hadi 7 inaendelea.

116.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Bandari ya Mtwara, ujenzi wa Gati lenye urefu wa mita 300 umefikia asilimia 60 wakati ukarabati wa Gati namba 2 na uongezaji wa kina cha Bandari ya Tanga unaendelea na umefikia asilimia 60. Ujenzi na ukarabati wa bandari zetu utaifanya nchi yetu kuendelea kuwa lango muhimu la uagizaji na uingizaji bidhaa kuelekea nchi jirani.

Ujenzi wa Meli

117.         Mheshimiwa Spika, Serikali inafanyia kazi changamoto ya utoaji wa huduma za usafiri katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Kwa upande wa ziwa Nyasa, tayari ujenzi wa Meli ya MV Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo umekamilika. Vilevile, tarehe 8 Desemba 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa chelezo, meli mpya ya MV Mwanza na ukarabati wa Meli za MV Victoria na MV Butiama.

118.         Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari 2020, ujenzi wa meli ya MV Mwanza itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ulikuwa umefikia asilimia 52. Aidha, ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 80, ukarabati wa meli za MV Victoria asilimia 75 na MV Butiama asilimia 70. Katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi inayoendelea, kukarabati vyombo vilivyopo na kununua vyombo vipya.

Usafiri wa Anga na Viwanja vya Ndege

119.         Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio niliyoyaeleza hapo awali kuhusu kufufua Shirika la Ndege Tanzania, katika Mwaka 2019/2020 Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa anga la Tanzania ni salama ili kuimarisha utoaji wa huduma za usafiri wa anga. Aidha, Serikali inakamilisha usimikaji wa mfumo wa rada 4 za kuongozea ndege za kiraia katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe.

120.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali vilivyopo nchini. Hadi kufikia Februari, 2020 Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. Kukamilika kwa jengo hilo kunawezesha kuwahudumia abiria milioni 6 kwa mwaka na hivyo kuongeza mapato. Serikali pia, imekamilisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza na inaendelea na ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huo. Jengo hilo ambalo litagharimu Shilingi bilioni 13.26 litahudumia abiria 400,000 kwa mwaka. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea, Geita, Nachingwea, Iringa na Musoma.

121.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuboresha usafiri wa anga nchini ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Katika kufanikisha azma hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa usalama na miundombinu ya viwanja vya ndege inaboreshwa.  

 

Mawasiliano

122.         Mheshimiwa Spika, katika eneo la mawasiliano Serikali imeendelea na zoezi la usajili wa laini za simu kwa njia ya biometria Nchi nzima. Hadi mwisho wa mwezi Februari, 2020 jumla ya laini milioni 31.4 kati ya laini milioni 43.9 zilikuwa zimesajiliwa. Idadi hii ni sawa na asilimia 71 ya zoezi zima la usajili. Nitoe wito kwa wananchi waliopata namba za vitambulisho vya Taifa kukamilisha usajili wa laini zao kwa njia ya biometria ili waendelee kupata huduma za mawasiliano. Zoezi hili lina umuhimu kwa Taifa kwani linasaidia kuimarisha usalama wa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini na Taifa kwa ujumla.

123.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia, imeendelea kusimamia mtambo wa Telecommunications Traffic Monitoring System (TTMS) ili kuhakikisha kuwa tunapata mapato stahiki kutokana na huduma za mawasiliano. Mfumo huu umeongeza ufanisi katika kusimamia huduma ya mawasiliano ya simu nchini. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Februari, 2020 jumla ya miamala bilioni 2 yenye thamani ya Shilingi trilioni 12.2 imefanyika ambapo Serikali imepata mapato ya Shilingi bilioni 7.3.

124.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kushirikiana na makampuni ya simu kuboresha huduma za mawasiliano hususan maeneo ya pembezoni ili kuongeza kasi ya mawasiliano ya kimtandao kwa wananchi wa maeneo hayo. Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufikisha huduma katika Makao Makuu ya Wilaya zote nchini pamoja na kuanza ujenzi wa Kituo cha Data Dodoma.

HUDUMA ZA JAMII

Elimu 

125.         Mheshimiwa Spika, elimu ya kisasa na hasa yenye mwelekeo wa sayansi na teknolojia ina nafasi ya pekee katika kufanikisha ujenzi wa msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Kwa kutambua umuhimu huo na kama nilivyoeleza awali Serikali ilianzisha na kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Ada ili kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anaandikishwa.

126.         Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kuboresha elimu ya sekondari ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa tarehe 31 Machi, 2020 Benki ya Dunia imeridhia kuipatia Tanzania mkopo wa Dola za Marekani Milioni 500 sawa na takriban shilingi trilioni 1.14 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa maboresho ya elimu ya sekondari nchini.

127.         Mheshimiwa Spika, Benki ya Dunia imeridhia kuipatia Tanzani mkopo huo baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada. Hivyo, mpango huu utaimarisha usalama wa watoto shuleni, kuongeza uandikishaji katika shule za sekondari na elimu mbadala, kuimarisha mafunzo kwa walimu na matumizi ya TEHAMA katika kufundisha hususan masomo ya sayansi.

128.         Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango huo utaongeza wigo wa elimu ya sekondari hususan kwa watoto wa kike na kuwawezesha wavulana na wasichana kukamilisha elimu hiyo. Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya Elimumsingi Bila Ada kwa lengo la kuwawezesha watoto wetu wa kike kupata elimu ya sekondari na stadi za kazi, kuondoa vikwazo kwa watoto wa kike kupata elimu ya sekondari, kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uratibu, usimamizi na tathmini ya ubora wa elimu ya sekondari.

129.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya juu, Serikali imeongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kutoa kipaumbele kwa watu wenye mahitaji maalum. Katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi 130,883 ikilinganishwa na wanafunzi 122,754 kwa Mwaka 2018/2019.  Aidha, Shilingi bilioni 450 zilitumika katika kipindi hicho ikilinganishwa na Shilingi bilioni 424.8 kwa Mwaka 2018/2019.

130.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Elimumsingi Bila Ada, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuhimiza uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi hususan katika kuboresha miundombinu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuendeleza rasilimali watu ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu.

Maji

Upatikanaji wa Maji Vijijini

131.         Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote hususan wale wanaoishi maeneo ya vijijini. Katika Mwaka 2019/2020, jumla ya miradi 94 ya maji yenye vituo vya kuchotea maji 2,495 katika maeneo mbalimbali vijijini imekamilika. Aidha, miradi 558 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

132.         Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi kubwa za Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo, hadi Desemba 2019, upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya vijijini umefikia asilimia 64.8. Vilevile, ili kuboresha utoaji wa huduma ya maji vijijini, Serikali imeanzisha Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wenye jukumu la kutekeleza miradi na kusimamia utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira vijijini.

Upatikanaji wa Maji Mijini

133.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maji mijini, Serikali imetekeleza miradi mipya ya maji katika Jiji la Dodoma na Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Kibaha, Bagamoyo na Kisarawe. Aidha, Serikali pia imeboresha miundombinu ya upatikanaji wa huduma ya maji katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na miradi ya maji ya kitaifa ya Chalinze, Mugango – Kiabakari, Maswa, Wanging’ombe, Masasi - Nachingwea na Kahama – Shinyanga. Utekelezaji wa miradi hiyo umewezesha upatikanaji wa maji katika miji ya mikoa kufikia asilimia 85.

134.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaifanyia mapitio Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 ili kuzingatia masuala mapya ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, kutilia mkazo suala la usafi wa mazingira na matumizi ya vyanzo vya maji chini ya ardhi. Serikali pia, itakamilisha miradi inayoendelea, kuanza miradi mipya ya maji na kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Singida hadi Dodoma.

 

Afya

Ujenzi na Ukarabati wa Hospitali  

135.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi wa hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo ujenzi wa hospitali za Mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Songwe, Katavi, Njombe (Mgondechi). Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali za Mikoa ya Mara, Singida na Shinyanga pamoja na ujenzi wa hospitali za Wilaya katika Halmashauri 70 nchini. Vilevile, Serikali inajenga Hospitali ya Uhuru wilayani Chamwino, Dodoma na hospitali za rufaa za kanda za Mtwara, Mbeya na Burigi - Chato.

Huduma za Afya za Kibingwa

136.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa bobezi (super specialist) katika Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa. Utoaji wa huduma hizo umewezesha wananchi wengi kupata huduma ambazo awali zilikuwa zinapatikana nje ya Nchi. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2020, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Benjamini Mkapa, MOI na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete zimetoa huduma mbalimbali za kibingwa kwa wagonjwa wa ndani na nje ya Nchi.

137.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, idadi ya wagonjwa waliopata huduma za kibingwa bobezi katika hospitali hizo ni 1,970. Kati yao, wagonjwa 18 walipata huduma za kupandikiza figo, 330 walipata huduma ya upasuaji wa uti wa mgongo, 730 upasuaji wa ubongo, 507 upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, 610 upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo, 101 upasuaji wa mishipa ya damu na watoto 284 walifanyiwa upasuaji wa vichwa vikubwa na mgongo wazi.

138.         Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imetoa tiba mionzi kwa wagonjwa 110,979 ikilinganishwa na wagonjwa 52,890 Mwaka 2018. Kati ya wagonjwa hao, 5,788 walipatiwa tiba ya mionzi. Ongezeko la tiba mionzi kwa wagonjwa limetokana na uwepo wa mitambo mipya miwili kwa ajili ya tiba ya saratani (LINAC) ambayo imesaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri tiba mionzi kutoka wiki nne Mwaka 2018 hadi wiki mbili Mwaka 2020.

139.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya afya ikiwemo ukarabati na ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Vilevile, itaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba pamoja na kuboresha huduma za kibingwa za afya na ubobezi katika Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalum na Hospitali za Rufaa za Kanda ili kuziwezesha kutoa huduma bora zaidi za kibingwa nchini.


Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu

140.         Mheshimiwa Spika, watu wenye ulemavu wanayo haki kwa mujibu wa Katiba ya kutambuliwa utu wao, kuendelezwa, kuheshimiwa na kulindwa dhidi ya vitendo vinavyoshusha utu wao ikiwemo ubaguzi, uonevu, ukatili na mila potofu. Katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa miongozo na mipango mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji wa haki na ustawi wa Watu Wenye Ulemavu na kuhakikisha huduma  zinazotolewa katika ngazi zote kwa ajili ya  Watu Wenye Ulemavu na wenye mahitaji maalum zinatolewa kwa haki na usawa.

141.         Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili Watu Wenye Ulemavu hususan kiuchumi, Serikali imezielekeza Halmashauri kutenga asilimia 2 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Watu Wenye Ulemavu. Kupitia mikopo hiyo jumla ya vikundi 160 vya Watu Wenye Ulemavu vimeundwa na vilipatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.87. Pamoja na hatua tuliyofikia napenda kutoa rai kwa Halmashauri zote nchini kutoa fedha hizi ili ziweze kutatua changamoto za kiuchumi zinazowakabili Watu Wenye Ulemavu kama ilivyokusudiwa na Serikali.

142.         Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imefanikiwa kuanzisha Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu na kufungua akaunti kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji. Serikali itatumia Mfuko huo kuratibu upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa wadau ili kuhakikisha Mfuko huo unakidhi malengo ya uanzishwaji wake.

143.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia, iliwezesha uendeshaji wa Baraza la Ushauri la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ambalo limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na 9. ya Mwaka 2010. Aidha, wajumbe wa Baraza hilo wamepatiwa mafunzo kuhusu Sera, Sheria, miongozo na mipango inayowahusu Watu Wenye Ulemavu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

144.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, wahitimu wa vyuo vikuu 167 wenye ulemavu, walipatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi kupitia Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi. Serikali itaendelea kuwahamasisha wahitimu wenye ulemavu kujiandikisha kwenye daftari la wanaotafuta ajira ili kupata fursa ya kuajiriwa pale nafasi zinapotangazwa. Aidha, Serikali imefanya jitihada na kufanikiwa kufufua vyuo vitatu vya mafunzo ya ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu. Vyuo hivyo ni Mirongo (Mwanza), Ruwanzari (Tabora) na Masiwani (Tanga).

145.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa. Baadhi ya shughuli zitakazopewa kipaumbele ni pamoja na kukamilisha maandalizi ya Mfuko wa Taifa wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu, kuratibu maadhimisho ya Siku za Kitaifa na Kimataifa za Watu Wenye Ulemavu na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu. Vilevile, Serikali itaendeleza vyuo vya mafunzo ya ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu.

ULINZI NA USALAMA

146.         Mheshimiwa Spika, hali ya amani na usalama ndani ya mipaka ya Tanzania ni shwari. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinatekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka ya Nchi, kudumisha amani, usalama wa raia na mali zao pamoja na kufundisha wananchi ulinzi wa umma. Serikali imeendelea kuliimarisha na kuliongezea uwezo Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia vifaa na zana bora za kisasa pamoja na kutoa mafunzo na mazoezi stahiki kwa wanajeshi ili kuliwezesha Jeshi kutekeleza majukumu yake ya msingi ya ulinzi wa mipaka ya Nchi yetu.

147.         Mheshimiwa Spika, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na majanga na matukio yenye kuleta athari kwa watu na mali zao na kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi hususan ujenzi, uendelezaji viwanda na shughuli za kilimo. Nitumie fursa hii kuvipongeza vyombo hivyo hususan Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Magereza kwa kushiriki ipasavyo katika ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

148.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao na kutokana na juhudi hizo, hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarika na uhalifu kupungua kwa asilimia 2.8 kwa makosa makubwa ya jinai ikilinganishwa na Mwaka 2018/2019. Halikadhalika, ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 25.7 ikilinganishwa na Mwaka 2018/2019.

149.         Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya uhamiaji haramu, Serikali ipo katika hatua za mwisho za uwekaji wa mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mipaka (e-Border Management System). Kukamilika kwa mfumo huo kutawezesha utoaji wa huduma bora za uhamiaji, kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka na kuongeza udhibiti katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

150.          Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kwamba msingi wa usalama wa raia na mali zao ni jukumu letu sote. Hivyo, ni muhimu wananchi wote tushirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kubaini wahalifu pamoja na vitendo vinavyohatarisha usalama wetu kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika.

151.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kulinda mipaka ya nchi yetu, kuimarisha usalama wa raia na mali zao ili kuhakikisha wananchi wanaishi na kufanya shughuli za maendeleo kwa amani. Vilevile Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na zana za kisasa zinazoendana na teknolojia ya kisasa pamoja na kuendelea kuhamasisha na kuelimisha wananchi juu ya masuala ya ulinzi, uzalendo, usalama na umuhimu wa kushiriki katika ulinzi.

USIMAMIZI WA KAZI NA WAFANYAKAZI

Kazi na Wafanyakazi

152.         Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuona wafanyakazi na wananchi kwa ujumla wanafanya kazi za staha na katika mazingira yanayokubalika. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kusimamia viwango vya kazi na wafanyakazi, afya na usalama mahali pa kazi, na kusimamia Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.

153.         Mheshimiwa Spika, katika kusimamia viwango vya kazi na wafanyakazi, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa kufanya kaguzi na kutoa elimu kwa wafanyakazi na waajiri. Aidha, mpaka kufikia mwezi Februari, 2020 kaguzi 3,663 zilifanyika katika maeneo mbalimbali ya kazi, ikiwa ni sawa na asilimia 76.3 ya lengo lililopangwa. Kupitia kaguzi hizo, waajiri 36 na raia wa kigeni 82 walifikishwa Mahakamani kwa kukiuka sheria za kazi ambapo, baada ya kupatikana na hatia walitozwa faini ya jumla ya Shilingi milioni 872.

154.         Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Nchini. Hadi kufikia mwezi Februari, 2020 jumla ya vibali vya kazi 6,625 vilitolewa kwa wageni na maombi 984 ya vibali vya kazi yalikataliwa kutokana na kutokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa Sheria. Vilevile, katika jitihada za kuongeza ufanisi, Serikali imejenga Mfumo wa Kielektroniki wa Vibali vya Kazi (On Line Work Permit Application and Information System) pamoja na kuanza kutoa mafunzo ya matumizi yake kabla ya kuzinduliwa na kuanza kutumika.

 

Afya na Usalama Mahali pa Kazi

155.         Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kudhibiti afya na usalama Mahali pa Kazi, Serikali kupitia Wakala wa Afya na Usalama mahali pa Kazi imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali katika maeneo ya kazi. Aidha, kwa Mwaka 2019/2020, jumla ya sehemu za kazi 2,270 zilisajiliwa, kaguzi 8,662 zilifanyika na wafanyakazi 93,575 walipimwa afya.

156.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kusajili vyama vya wafanyakazi, sehemu mpya za kazi, kufanya kaguzi za kawaida, kaguzi maalum, kupima afya za wafanyakazi na kutoa elimu ya Afya na Usalama kwa Wajasiriamali wadogo na wa kati.

UTUMISHI WA UMMA

157.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha utendaji kazi wenye tija kwa kuboresha vitendea kazi, kuongeza na kuwajengea uwezo watumishi. Hadi kufikia mwezi Machi 2020, Serikali imetoa ajira mpya na mbadala 6,975 na kuwapandisha vyeo Watumishi 290,625 wa Kada mbalimbali. Aidha, Serikali imelipa Shilingi bilioni 130.4 kwa Watumishi wa Umma 100,684 waliokuwa wanadai madeni mbalimbali na uhakiki wa Watumishi 36,981 wenye madeni ya Shilingi bilioni 88.389 unaendelea. Uhakiki huo ukikamilika madeni hayo yatalipwa.

158.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wafanyakazi wote kwa mchango wao mkubwa katika kujenga Taifa letu. Napenda kuwahakikishia watumishi wote kuwa, katika mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kufanya kazi ili Watumishi wa Umma wafanye kazi kwa weledi, juhudi, uadilifu na uwajibikaji.

 

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

159.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imefanikiwa kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye miradi ya kielelezo na kimkakati ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere ambapo Watanzania 250,000 wameajiriwa katika nafasi mbalimbali zenye ujuzi wa juu, kati na chini, ikilinganishwa na wageni 1,338. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 99 ya ajira zote kwenye miradi hiyo. Aidha, Shilingi bilioni 170 zililipwa kwa kampuni za kitanzania ambazo zilipata kazi katika miradi ya kielelezo na kimkakati inayotekelezwa nchini.

160.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuzitumia Taasisi zake za ndani za masuala ya ujuzi na teknolojia zikiwemo Vyuo vya VETA, Chuo cha Ufundi Dar es salaam (DIT), Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) na vyuo vya ufundi vya Don Bosco katika kuandaa na kufundisha programu zitakazowezesha Watanzania kushiriki katika miradi ya kimkakati,  kujiajiri na kuajiriwa katika maeneo mbalimbali.

161.         Mheshimiwa Spika, kufuatia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuwa kila Halmashauri itenge asilimia 10 ya makusanyo yake kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu, Halmashauri zilitenga jumla ya Shilingi bilioni 54.1 na kutoa jumla ya Shilingi bilioni 25.4 kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu. Kati ya fedha hizo; Shilingi 12.9 bilioni zilitolewa kwa wanawake, Shilingi 9.5 bilioni zilitolewa kwa vijana na Shilingi bilioni 2.9 zilitolewa kwa watu wenye ulemavu. Napenda kusisitiza Halmashauri zote nchini kuendelea kutenga na kutoa mikopo hiyo kwa walengwa ili waweze kuinua hali zao kiuchumi na kuongeza mchango wao katika kujenga uchumi wa Taifa.

162.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kusimamia uanzishwaji wa vituo maalum vya uwezeshaji katika mikoa mbalimbali nchini. Lengo ni kuwawezesha wananchi kupata taarifa mbalimbali kuhusu fursa za uwezeshaji, usajili na uendelezaji wa biashara, upatikanaji wa mitaji na mafunzo ya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali.

Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana

163.         Mheshimiwa Spika, ili kutumia kundi la vijana kama fursa muhimu kwa maendeleo ya Taifa, Serikali imeendelea na uboreshaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Katika Mwaka 2019/2020, Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.2 ambapo vikundi 586 vyenye jumla ya vijana 4,222 kutoka katika Halmashauri 155 walipata mikopo hiyo.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)

164.         Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Februari 2020, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Awamu ya Tatu ya TASAF utakaotekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. Kuzinduliwa kwa kipindi hiki cha Pili cha Mpango huo, kunadhihirisha nia ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutetea wanyonge na wasiojiweza.


165.         Mheshimiwa Spika, Mpango huu umewezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu pamoja na kujenga rasilimali watu. Mathalan, kipindi cha Kwanza cha TASAF Awamu ya Tatu kilihudumia kaya milioni 1.1 zenye watu milioni 5.2 katika Halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar.

166.         Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango huu wa TASAF kaya maskini zimemudu kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii pamoja na kujikwamua dhidi ya umaskini. Kwa mfano, asilimia 32 ya kaya zilijiunga na Bima ya Afya ya Jamii ikilinganishwa na asilimia 11 kabla ya mpango wa TASAF. Aidha, katika kipindi cha Mwaka 2011/2012 hadi 2017/2018 umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara, ulipungua kwa asilimia 1.8 na wa chakula kwa asilimia 1.7. Aidha, takwimu zinaonesha pia kuwa, umaskini uliokithiri umepungua kutoka asilimia 28.2 hadi asilimia 26.4. Kupungua huko kumechangiwa na utekelezaji wa mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini.

167.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itafanya utambuzi na uhakiki wa hali za ustawi wa maisha ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri 101. Lengo ni kubaini kaya ambazo si maskini tena sambamba na kuandikisha kaya mpya 235,647 ambazo hazikufikiwa katika kipindi cha kwanza cha Mpango. Natoa wito kwa wote waliopewa dhamana ya kutekeleza Mpango huu kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uaminifu mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 

Ukuzaji Ujuzi

168.         Mheshimiwa Spika, suala la ukuzaji ujuzi wa nguvukazi nchini ni miongoni mwa ajenda muhimu ya kisera katika kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi. Serikali imeendelea kuwezesha wananchi wake kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini kwa lengo la kuwapatia ujuzi na stadi za kazi hasa kundi la vijana, wanawake na Watu Wenye Ulemavu. Ujuzi huo, utawawezesha kumudu ushindani katika soko la ajira na hivyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

169.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, jumla ya vijana 30,099 wamewezeshwa kupata ujuzi kupitia programu hiyo. Kati yao, vijana 5,875 wamepata mafunzo ya uanagenzi katika fani za ufundi stadi katika maeneo mbalimbali. Mafunzo haya yamefanyika katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Geita, Mara, Kilimanjaro, Iringa, Morogoro, Kagera, Singida, Shinyanga na Ruvuma. Aidha, jumla ya vijana 5,395 wamepewa mafunzo na kurasimishiwa ujuzi walioupata kupitia mfumo usio rasmi wa mafunzo kupitia VETA katika fani za uashi, useremala, ushonaji, ufundi bomba, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi magari, ufundi umeme, ukarabati wa bodi za magari, upishi na uhudumu katika hoteli.


170.         Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wahitimu wa elimu ya juu wanapata uzoefu wa kazi ili kuwawezesha kupata ajira, jumla ya wahitimu 2,115 wamewezeshwa kupata mafunzo ya uzoefu kazini kupitia viwanda na kampuni mbalimbali nchini. Kati yao, wahitimu 100 wa fani ya kilimo wamewezeshwa kwenda nchini Israeli kuhudhuria mafunzo ya uzoefu kazini katika kilimo cha kisasa kwa muda wa mwaka mmoja. Aidha, vijana wengine 3,200 wataanza mafunzo mwezi huu wa Aprili 2020. Nichukue fursa hii kuzishukuru taasisi za umma na binafsi ambazo zinaendelea kutoa nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wahitimu wetu.

171.         Mheshimia Spika, kwa Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana katika fani mbalimbali. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika nyanja mbalimbali ili kukuza ujuzi wa rasilimali watu.

 

Ukuzaji wa Fursa za Ajira

172.         Mheshimiwa Spika, sambamba na ukuzaji ujuzi, Serikali pia imeendelea kuratibu juhudi za ukuzaji wa fursa za ajira. Katika kipindi cha Julai hadi Februari 2020, jumla ya ajira 1,577,622 zimezalishwa katika sekta mbalimbali ambapo ajira 579,518 zimezalishwa na sekta rasmi na ajira 998,104 zimezalishwa na sekta isiyo rasmi. Serikali pia, imeendelea na utoaji wa huduma za ajira ili kuwezesha watafutakazi kumudu ushindani wa soko la ajira. Hadi kufikia tarehe 31 Januari 2020, jumla ya watafutakazi 6,756 wamesajiliwa na Kitengo cha Huduma za Ajira ili kupatiwa huduma mbalimbali za ajira hususan, ushauri nasihi (vocational guidance and employment counselling) na mafunzo ya kumudu ushindani katika soko la ajira. Watafutakazi waliopatiwa huduma ya ushauri nasihi pamoja na mafunzo hayo walikuwa 5,266.

173.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya ukuzaji wa fursa za ajira. Mikakati hiyo ni pamoja na kuwawezesha vijana wabunifu na makundi mbalimbali ya vijana na wanawake kuanzisha shughuli za uzalishaji mali na ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine na kuimarisha mifumo ya taarifa za soko la ajira na mitaji ili kuwezesha vijana kutumia fursa hizo.

HIFADHI YA JAMII

 

Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii

 

174.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kutekeleza programu ya maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa Kinga ya Jamii inawafikia wananchi walio wengi.  Maboresho yaliyofanyika yamelenga kuongeza ufanisi katika sekta ya hifadhi ya jamii. Vilevile, Serikali imeanza kutekeleza kipindi cha Mpito cha miaka mitano (2019 – 2023) cha kuendelea kuboresha Sekta ya Hifadhi ya Jamii hususan suala la pensheni kwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mifuko ya Pensheni          

175.         Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Pensheni ya NSSF na PSSSF imekuwa ikifanya kazi muhimu ya kulipa pensheni pamoja na mafao mengine kwa wastaafu katika sekta za umma na binafsi. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, Mifuko hiyo ililipa pensheni, malipo ya mkupuo pamoja na mafao mengine yenye jumla ya Shilingi trilioni 1.4 kwa wanachama 206,897 na wastani wa Shilingi bilioni 51.7 zimelipwa kila mwezi kwa wastaafu kama pensheni.

176.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaboresha uchakataji wa mafao ili kulipa mafao stahiki na kwa wakati; na kuimarisha ukusanyaji wa michango na mapato yatokanayo na uwekezaji na Mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utendaji kazi.

MASUALA MTAMBUKA

Vita Dhidi ya Rushwa

177.         Mheshimiwa Spika, jitihada za kuinua uchumi na kuongeza huduma za jamii hazitaleta manufaa kwa wananchi na kuondoa umasikini iwapo adui rushwa ataendelea kulitafuna Taifa letu. Rushwa ni adui wa haki, maendeleo na ustawi wa wananchi, pia ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili Nchi yetu na dunia kwa ujumla.

178.         Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na rushwa ambayo imeweza kupunguza vitendo vya rushwa kwa kiasi kikubwa nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Awamu ya Tatu wa Mwaka 2017 - 2022. Hii inadhihirishwa na matokeo ya tafiti zilizofanywa Mwaka 2019 na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa na kuonesha kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kudhibiti vitendo vya rushwa na ufisadi. Aidha, kiashiria cha Corruption Perception Index (CPI) cha taasisi ya Transparency International kimeonesha Tanzania imefikia kiwango cha asilimia 37 na kushika nafasi ya 96 kati ya nchi 180 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 30 katika nafasi  ya 119 Mwaka 2015.

179.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeokoa kiasi cha Shilingi  bilioni 47.3 zikiwa ni thamani ya mali na fedha taslimu zilizotokana na operesheni  mbalimbali za kiuchunguzi zilizofanyika nchini. Serikali pia, ilifanya ufuatiliaji katika miradi 244 ya maendeleo iliyohusisha sekta za Afya, Elimu, Maji, Ujenzi na Nishati yenye thamani ya Shilingi trilioni 9.86 ili kuhakikisha inatekelezwa kulingana na thamani halisi ya fedha.

180.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo mbalimbali kwenye Sekta za Umma katika ngazi zote nchini ili kubaini na kupendekeza njia madhubuti za kuziba mianya ya rushwa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa kwa ajili hiyo.

Mapambano Dhidi ya UKIMWI

181.         Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa Mwaka 2018/2019 - 2022/2023 ambao unalenga kutekeleza malengo ya dunia yenye mwelekeo wa kupambana na UKIMWI ili kufikia TISINI TATU (90:90:90). Katika kutekeleza malengo hayo, lengo la 90 ya kwanza ni kuhakikisha asilimia 90 ya watu wanapima na kujua hali zao ambapo hadi Desemba 2019 wenye VVU na waliopima na kujua hali zao ilikuwa asilimia 80.1 ikilinganishwa na asilimia 75 kwa Mwaka 2018. Lengo la 90 ya pili ni kuhakikisha asilimia 90 ya waliokutwa na VVU wanaanzishiwa dawa za kufubaza VVU ambapo walioanza dawa za ARV na kubaki katika dawa ni asilimia 98.8 ikilinganishwa na asilimia 98 kwa Mwaka 2018. Lengo la 90 ya tatu ni kuhakikisha asilimia 90 ya wanaoanzishiwa dawa za ARV kinga zao za mwili zinaimarika ambapo lengo hili limefikiwa kwa asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 88 kwa Mwaka 2018.

182.         Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi za dhati zilizofanywa na Serikali, hali ya maambukizi ya UKIMWI inaonesha kuna Watanzania takribani milioni 1.6 wanaoishi na VVU ambapo kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 7 ya Mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 4.7 kwa Mwaka 2020.

183.         Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo yamechangiwa na jitihada mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na kupitia miongozo na Sheria mbalimbali ambapo umri wa vijana kupima VVU bila ya kuambatana na wazazi au walezi wao umeshushwa kutoka miaka 18 hadi 15. Aidha, dawa mpya ya ARV yenye ufanisi  (Dolutegravir) imeruhusiwa kuingizwa na kutumika nchini ambapo hadi Desemba 2019 asilimia 53 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) wameanza kutumia dawa hiyo. Serikali pia imeridhia mfumo wa watu kujipima wenyewe.

184.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kufanya jitihada za kupunguza kasi ya maambukizi katika jamii kwa kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali muhimu kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI; kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuimarisha huduma za elimu ya UKIMWI.

Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya

185.         Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kimataifa katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya. Nchi yetu imefanikiwa kwa ufanisi mkubwa kudhibiti uzalishaji, uuzaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya. Mafanikio hayo, yamewezesha waathirika wengi hasa vijana kubadilika na kujihusisha katika shughuli za uzalishaji mali pamoja na kuipatia sifa Tanzania kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa.

186.         Mheshimiwa Spika, katika kikao cha 63 cha Kamisheni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu kilichofanyika Machi 2020, Tanzania ilipongezwa kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza miongozo ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

187.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020 Serikali ilifanikiwa kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya 6,350. Katika kipindi hicho, kilogramu 34.986 za heroine na kilogramu 1.556 za cocaine zilikamatwa. Kadhalika, tani 10.559 za bangi, tani 6.016 za mirungi na mashamba ya bangi 9 yenye jumla ya ekari 4.25 yaliteketezwa.

188.         Mheshimiwa Spika, pamoja na kukamata watuhumiwa na madawa ya kulevya, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za matumizi ya dawa za kulevya kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Elimu kuhusu dawa za kulevya na UKIMWI pia imetolewa kwa wasanii 600 pamoja na makundi maalum ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na viongozi wa mbio za Mwenge. Elimu hiyo, imesaidia kujenga uelewa wa pamoja juu ya athari na namna ya kupambana na kudhibiti dawa za kulevya nchini.

189.         Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imefanya ukaguzi wa kampuni 58 zinazojihusisha na biashara ya kemikali bashirifu na usafirishaji wa vifurushi. Kupitia ukaguzi huo, imegundulika kuwa baadhi ya kampuni hizo hutumia majina bandia katika kuingiza kemikali bashirifu na kusafirisha vifurushi vya dawa za kulevya. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imefanikiwa kukamata watuhumiwa 7 na zaidi ya kilo 890 za dawa za kulevya aina ya mirungi katika Ofisi za Posta zilizokuwa na majina bandia kama vile mlonge na majani ya chai zikisafirishwa kwenda nchi za Ulaya, Marekani na Canada.

190.         Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeimarisha ukaguzi katika kampuni zinazosafirisha vifurushi kwenda nje ya nchi zikiwemo Ofisi za Posta. Aidha, katika kuboresha shughuli za ukaguzi wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, Serikali imeandaa miongozo ya ukaguzi na uchukuaji sampuli itakayosaidia kufanya ukaguzi wenye ufanisi kubaini usafirishaji dawa za kulevya, kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

191.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa tiba dhidi ya waathirika wa dawa za kulevya, Serikali inapanua wigo wa utoaji huduma za tiba kwa kujenga na kuanzisha vituo vya utoaji wa huduma ya methadone katika Mikoa ya Tanga na Pwani. Hadi sasa, zaidi ya watumiaji 8,200 wanapata huduma za tiba ya methadone kila siku katika vituo vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tanga na Pwani.

192.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kudhibiti uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kuongeza huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya.

Uratibu wa Maafa

193.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2019/2020, Nchi yetu imekumbwa na maafa mbalimbali ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi na majanga ya moto. Wananchi wa Bonde la Mto Rufiji wamepata athari ya mafuriko ambako serikali kupitia Mkoa na Wilaya, pia Ofisi ya Waziri Mkuu inashirikiana na Viongozi wa Wilaya kutoa huduma kadiri tathmini inavyoendelea. Maeneo mengi nchini yameendelea kupata mafuriko na kuathiri shughuli za wananchi. Kufuatia hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kukabili na kurejesha hali ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, reli na majengo ya umma yaliyoathirika na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika.

194.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote. Lengo ni kuongeza uelewa na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya majanga kwa kupunguza vihatarishi na vyanzo vinavyoweza kusababisha maafa. Aidha, kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha nchini,  naelekeza wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wananchi walioweka makazi katika maeneo hatarishi ikiwemo kandokando ya mito na mabonde wanahama mara moja katika maeneo hayo ili kupunguza madhara yanayoendelea kujitokeza katika jamii.

195.         Mheshimiwa Spika,  katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za tahadhari za awali na kuzingatia Wasifu wa Janga la Mafuriko na Ukame nchini. Wasifu huo, unajumuisha taarifa za ramani ya maeneo hatarishi, rasilimali,  miundombinu muhimu katika maeneo hayo, hatari ya kudhurika na makadirio ya hasara za kiuchumi kutokana na madhara ya mafuriko na ukame.

 

Mazingira

196.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na uharibifu wa mazingira ikiwemo kuhamasisha upandaji miti, usafi na utunzaji wa mazingira sambamba na kuanza mradi wa usambazaji gesi majumbani na kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

197.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa usambazaji wa gesi majumbani, viwandani na katika magari. Hadi kufikia Desemba 2019, Serikali imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji gesi asilia na kuunganisha nyumba 125 na Taasisi 4 mkoani Mtwara. Aidha, viwanda 48 vimeunganishwa na gesi asilia ikiwemo viwanda vya Coca Cola, Tanzania Breweries Ltd, Kiwanda cha Cement cha Wazo Hill vilivyopo Dar es Salaam na kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara. Halikadhalika, ujenzi wa miundombinu ya kuunganisha nyumba 185 na Taasisi 4 jijini Dar es Salaam nao umekamilika.

198.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia imefanikiwa kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Katika Mwaka 2019/2020, tani 259.2 za mifuko ya plastiki zilikusanywa nchi nzima. Kati ya hizo, tani 171.5 ziliteketezwa na tani 86.7 zilirejelezwa katika viwanda mbalimbali hapa nchini. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia ubora na matumizi ya mifuko mbadala.

199.         Mheshimiwa Spika, katazo la mifuko ya plastiki limetoa fursa za kuzalisha mifuko mbadala ambapo wadau wengi wamejitokeza kuwekeza katika sekta hiyo. Kwa mfano, hadi sasa idadi ya viwanda vipya vinavyozalisha mifuko mbadala vimefikia 7. Kati ya hivyo viwanda 6 vipo Dar es Salaam na kimoja kipo Arusha.

200.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuziagiza Halmashauri zote nchini kuendelea kutunza mazingira ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.

201.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, pamoja na mambo mengine, Serikali itaendelea na zoezi la kuunganisha viwanda na nyumba nyingi zaidi kwenye mtandao wa matumizi ya gesi asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara. Vilevile, Serikali itaimarisha juhudi za kuhifadhi na kulinda mazingira kwa kutekeleza miradi mbalimbali.


MUUNGANO

202.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kushirikiana vyema na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano wetu. Katika Mwaka 2019/2020, vikao mbalimbali vya Wataalam na Makatibu Wakuu vilifanyika na kujadili masuala ya uvuvi kwenye ukanda wa bahari kuu, na hoja za fedha na biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Aidha, maandalizi ya vikao vya pamoja vya Mawaziri wa SMT na SMZ yamefanyika ikiwemo na kuundwa kwa kamati ya kitaifa inayoratibu ugonjwa wa Corona.

203.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuenzi dhamira ya Waasisi wa Muungano.

204.         Mheshimiwa Spika, ndugu zetu Wachina wanao msemo maarufu usemao, “When we drink water from the well, we should not forget those who dug it.” Msemo huu humaanisha kuwa, tunapokunywa maji kutoka kwenye kisima basi tusisahau fadhila za waliochimba kisima hicho. Hivyo basi, nasi hatuna budi kuendelea kuenzi na kuheshimu juhudi za Waasisi wa Muungano wetu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume kwa kutuachia alama ya Muungano ambao umekuwa funzo kwa mataifa mengine. Kwa msingi huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria wa kuuenzi na kuulinda Muungano wetu sambamba na kudumisha amani na utulivu katika pande zote mbili za Muungano.
205.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru wananchi wote wa Unguja na Pemba ambao sio tu walinipokea vizuri, lakini pia walinipatia ushirikiano mkubwa wakati wa ziara yangu ya kikazi mwezi Januari 2020 kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa upande wa Zanzibar.

206.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimarisha ziara na ushiriki wa viongozi wakuu katika matukio muhimu ya kitaifa sambamba na kufanya mikutano ya mashauriano ya viongozi na watendaji kwa lengo la kuimarisha Muungano wetu.

 

UHUSIANO WA KIMATAIFA

207.         Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali ya kidiplomasia kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Aidha, mahusiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa yameendelea kuimarika.

208.         Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa mahusiano na ushawishi wetu kwa Jumuiya ya Kimataifa kumewezesha Tanzania kuanzisha Balozi mpya 2 katika nchi rafiki katika Mwaka 2019/2020. Balozi hizo ni Windhoek – Namibia na Havana – Cuba. Sanjari na hilo, Tanzania imeendelea kuridhia na kutekeleza Itifaki na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa.

209.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Tanzania itaendelea kuridhia na kutekeleza mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda sambamba na kuheshimu misingi ya mahusiano na mataifa mengine duniani. Aidha, kupitia ushirikiano mzuri uliopo na ushawishi wetu kwenye jumuiya za kikanda na kimataifa, Tanzania italinda uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe, na kujenga umoja na mtangamano wa kikanda wa Bara la Afrika. Halikadhalika, Tanzania itashiriki kikamilifu katika kuendeleza siasa ya kutofungamana na upande wowote kama dira na msimamo wetu katika mahusiano baina yetu na Nchi nyingine katika Jumuiya ya Kimataifa.

210.         Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kukuza ushirikiano kwenye nyanja za biashara, uwekezaji, masoko ya bidhaa zetu, utalii na lugha ya Kiswahili ili kuchochea maendeleo ya Nchi.

 

HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO

211.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2019/2020 Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha upatikanaji wa habari, kurasimisha kazi za kitamaduni, sanaa na ubunifu na kuhakikisha watendaji wa kazi hizo wanapata maslahi yanayoendana na kazi zao. Aidha, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili inaendelezwa ndani na nje ya Nchi na kutumika kama bidhaa ya soko na chanzo cha ajira kwa wataalam wa lugha yetu ya Kiswahili.
           
212.         Mheshimiwa Spika, Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Tanzania tarehe 17 na 18 Agosti, 2019 jijini Dar es Salaam ulipitisha lugha adhimu ya Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi za Jumuiya hiyo. Serikali imeandaa Miongozo ya Ufundishaji Kiswahili kwa Wageni na kubainisha mahitaji ya uandaaji wa Mitaala ya kufundishia Kiswahili katika Nchi za kigeni. Aidha, kupitia kanzidata ya usajili wa Wataalam wa Kiswahili iliyopo Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), jumla ya wataalam 1,159 wamesajiliwa  hadi mwezi Machi, 2020.

213.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kulipongeza Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kufuatia maboresho muhimu kwenye mfumo wa urushaji matangazo. Tarehe 30 Machi, 2020 TBC iliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la studio na kuzindua programu tumizi na tovuti ya Safari Channel. Maboresho hayo yataimarisha mfumo mzima wa urushaji matangazo hususan taarifa ya habari (Aridhio).

214.         Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2020/2021, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya Mwaka 2016 na kuratibu na kusimamia maendeleo ya michezo nchini ikiwemo ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

HITIMISHO

215.         Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, katika kipindi cha takriban miaka mitano tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie madarakani tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii.

216.         Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo ni ishara tosha kwa Watanzania kwamba ahadi za Chama Cha Mapinduzi ndani ya kipindi cha miaka mitano (2015 hadi 2020) zinatekelezwa vyema na kwa mafanikio makubwa. Hivyo basi, katika Mwaka 2020/2021, Serikali pamoja na mambo mengine, itaweka mkazo katika masuala yafuatayo:
Mosi:              Kuimarisha na kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo ili kuleta maendeleo endelevu hususan tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020;

Pili:                Kulinda uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe bila kuingiliwa; mipaka ya Nchi; haki; kuimarisha ujirani mwema na kuunga mkono Sera ya Kutofungamana na Upande wowote kama dira na msimamo wetu katika mahusiano na Nchi nyingine katika Jumuiya ya Kimataifa;

Tatu:               Kudhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na utoaji huduma hususan kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuondoa urasimu usio wa lazima pamoja na kuwahudumia wananchi wote kwa tija tena bila ubaguzi wa aina yoyote;

Nne:               Kuendelea kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji;

Tano:              Kuhimiza uwajibikaji wa watendaji wa Serikali katika ufuatiliaji wa miradi ya kielelezo hususan ujenzi wa miundombinu muhimu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo reli, bandari, ujenzi wa meli, vivuko, viwanja vya ndege, barabara na madaraja;

Sita:                Kuwatumikia Watanzania wote kwa kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa kukamilisha na kuendelea na ujenzi wa miradi ya miundombinu ya maji, afya na elimu;

Saba:              Kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa nishati ya uhakika kwa kukamilisha Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa MW 2,115 la Julius Nyerere na kuhakikisha vijiji vilivyobaki katika utekelezaji wa mradi wa REA III vinapatiwa umeme;

Nane:             Kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi, mashamba na maeneo ya makazi, uwekezaji na ujenzi wa viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira zaidi kwa watanzania;

Tisa:               Kusimamia kikamilifu matumizi sahihi na yenye tija ya rasilimali zilizopo ili zitumike kwenye maeneo yanayochochea ukuaji uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi; na

Kumi:            Kuhimiza Watanzania kufuata maelekezo ya Serikali kuhusu kujikinga, kudhibiti na kutosambaza virusi vya Corona ili kupunguza athari za kijamii na kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na maambukizi hayo. Serikali kwa upande wake inashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na kutokomeza maambukizi ya virusi hivyo vya Corona.

217.         Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa kila mwananchi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi mahiri na thabiti wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa.

 

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2020/2021


218.         Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2020/2021, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni mia tatu kumi na mbili, milioni mia nane na mbili na mia tano ishirini elfu (312,802,520,000); kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni themanini na nane, milioni mia nne ishirini na tisa na mia moja hamsini na sita elfu (88,429,156,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni mia mbili ishirini na nne, milioni mia tatu sabini na tatu na mia tatu sitini na nne elfu (224,373,364,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

219.         Mheshimiwa Spika, Vilevile naliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni mia moja ishirini na moja, milioni mia saba themanini na sita na mia mbili hamsini na saba elfu (121,786,257,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni mia moja kumi na tatu, milioni mia tano sitini na saba na mia sita arobaini na saba elfu (113,567,647,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni nane, milioni mia mbili kumi na nane na mia sita na kumi elfu (8,218,610,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

220.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.