Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar yapokea msaada kutoka shirika la Afya ya duniani WHO

 Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirmay Andemichael (kushoto) akikabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 110 kwa ajili ya kituo cha kuratibu maradhi ya mripuko ikiwemo (COVID -19) kwa Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Jamala Adam Taib, hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
 Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Jamala Adam Taib (alievaa shati jeupe) akitoa shukrani kwa Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Ghirmay Andemichael msaada walioutoa.
Gari lililobeba vifaa mbalimbali kwa ajili ya kituo cha kuratibu maradhi ya mripuko ikiwemo (COVID -19) vilivyotolewa msaada na Shirika la Afya Duniani.
Picha na Makame Mshenga.
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar  28/04/2020.
Wizara ya  Afya Zanzibar imepokea msaada wa vifaa mbali mbali vya kuthibiti maambukizi ya Corona kutoka Shirika la Afya Duniani  (WHO)  vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 110.
Akipokea msaada huo, huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Jamala Adam Taib amelishukuru  shirika hilo  kwa kutoa msaada ambao utawasaidia wafanyakazi  kutekeleza kazi zao kwa ufanisi pamoja na kujikinga na maambukizi ya Corona
Alifahamisha kuwa Shirika la Afya Duniani linaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuonyesha mashirikiano  ya pamoja katika udhibiti na  ufuatiliaji wa mwenendo mzima tokea mwanzoni mwa Mripuko wa maradhi hayo kuanza .
Nae  Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani  Ghirmay Ande Michel wakati akikabidhi vifaa hivyo amesema vifaa hivyo vimekusudiwa kutumika katika kitengo cha mwenendo wa  Kuratibu Maradhi ya Mripuko yakiwemo (COVID -19).
Amesema vifaa hivyo ni vitendea kazi ikiwemo komputa za kisasa vifaa vya thamani,Barakoa,vipima joto ,cloves,nguo maalumu za kujikinga na maambukizi ya maradhi ya Corona na vyenginevyo .
Alifahamisha kuwa Shirika la Afya Duniani litaendelea kutoa misaada mbali mbali ya kujikinga na maambukizi ya Corona na (COVID-19) Kwa lengo la kupambana na mripuko huo ambao umeikumba Dunia .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.