Habari za Punde

Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ Yakabidhi Msaada wa Shs Milioni Mia Moja Kuchangia Kupambana na Maradhi ya Corona Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akipokea mfano wa Hundi ya Shilingi Milioni 100,000,000/- kutoka kwa Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Corona hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Wa kwanza Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Nd. Iddi Haji Makame na wa kati kati ni Naibu Mkurugenzi wa Benki hiyo Bibi Khadija Shamte Mzee.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Nd. Iddi Haji Makame akifafanua mchango uliotolewa na Benki yake kuwahusisha wale waliowakusudia kuhudumiwa kutokana na athari ya Corona.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiushukuru Uongozi pamoja na Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar {PBZ} kwa uamuzi wake wa kuchangia mapambano dhidi ya kuangamiza Virusi vya Corona Nchini.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Uongozi mzima wa Benki ya Watu wa Zanzibar {PBZ} umeamua kujitolea kuungana na Serikali Kuu kwa kutoa mchango wa Shilingi Milioni Mia Moja Taslim {100,000,000/-} katika kusaidia mapambano dhidi ya kukabiliana na Virusi vya Corona Nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Nd. Iddi Haji Makame akiuongoza Uongozi wa Taasisi hiyo ya Fedha alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi sampuli ya Hundi ya Fedha hizo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanziba ambazo tayari zimeshaingizwa kwenye Akaunti ya Mfuko wa Corona.
Nd. Iddi Haji Makame alisema Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar umezingatia kazi kubwa na ya Kizalendo inayofanywa na Madaktari pamoja na Watendaji wa Sekta ya Afya na kupendelea Shilingi Milioni 40,000,000/-  za mchango huo wapatiwe wahudumu hao wa Sekta ya Afya.
Alisema Shilingi Milioni 60,000,000/- wamefikiria kuhudumia Wananchi wa Kaya  zilizoathirika na Virusi vya Corona ambao walilazimika kukaa katika Kambi Maalum muda ambao umeviza harakati zao za Kimaisha za kujitafutia riziki za kila siku.
Akipokea Mchango huo wa PBZ Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema inatia moyo kuona kwamba kasi ya kuenea kwa Virusi vya Corona imepungua sana ndani ya Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Balozi Seif  alisema mchango wa Benki ya Watu wa Zanzibar umeonyesha Watendaji hao kuguswa na janga hilo ambapo pia aliwashauri Wananchi waendelee kushirikiana na Viongozi, Taasisi pamoja na Wataalamu wa Afya katika kuhakikisha Corona ndani ya Visiwa vya Zanzibar inabakia kuwa Historia katika muda mchache ujao.
Aliwashukuru Wananchi wa Zanzibar kwa ukubali wao wa kuitikia pamoja na kupokea maagizo yote yaliyokuwa yakitolewa  na Viongozi wao pamoja na ushauri wa Wataalamu wa Afya katika kuepuka vishawishi vinavyosababisha kuambukizwa na Virusi hivyo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi pamoja na Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar {PBZ} kwamba mchango huo utatumika na kuelekezwa kwa walengwa wote kama ilivyokusudiwa.
Corona (Covid - 19) ni familia ya virusi vinavyosababisha ugonjwa kuanzia mafua ya kawaida hadi magonjwa makali zaidi kama vile matatizo ya kupumua ikiwa ni mripuko mpya uliogunduliwa mwaka 2019 na havikuwahi kubainika hapo kabla miongoni mwa bindamu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.