HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA SHERIA,
UTAWALA BORA NA IDARA MAALUM KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA
RAIS, UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA
KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021
Mheshimiwa Spika, kila sifa njema anastahiki Mwenyezi
Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia Uzima na Afya njema ambavyo
vimetuwezesha kukutana tena katika Baraza hili kwa lengo la kujadili na kuidhinisha
Mapato na Matumizi ya Fedha za Serikali yetu Tukufu. Vile vile, nachukua fursa
hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote
wa Baraza kwa kuliongoza Baraza hili kwa umahiri mkubwa na ninaamini kwamba
mtaendelea kuliongoza Baraza hili kwa uadilifu wa hali ya juu.
Mheshimiwa
Spika, aidha,
napenda kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein
kwa kuiongoza nchi yetu kwa uadilifu, hali inayopelekea kupatikana kwa
maendeleo pamoja na kuendelea kudumu kwa amani na utulivu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pia, sina budi kumshukuru Waziri wa
Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Mwalimu Haroun Ali
Suleiman kwa umahiri wake uliomfanya aweze kuteuliwa tena kuwa Waziri katika
Wizara hii mpya pamoja na kuwapongeza watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu,
Naibu Katibu Mkuu na bila ya kuwasahau watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango
kwa mashirikiano waliyotupatia wakati wa kupitia makadirio ya Bajeti ya Wizara
hii.
Mheshimiwa Spika, vile vile, nachukua fursa hii
kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu kwa umoja wao na kazi nzuri
waliyoifanya kiasi cha kunirahisishia kazi yangu ya kuongoza kikao kuwa nyepesi
zaidi, kwa hakika ni Wajumbe mahiri, wameweza kuijadili ipasavyo na kuhoji
mambo mbali mbali kwa lengo la kuhakikisha kwamba fedha wanazoidhinisha kwa
Wizara hii zinatumiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima ya hali ya juu kabisa
napenda kuwatambua Wajumbe hao kwa majina kama ifuatavyo:
1.
|
Mhe. Machano Othman Said
|
Mwenyekiti
|
2.
|
Mhe. Zulfa Mmaka Omara
|
Makamu Mwenyekiti
|
3.
|
Mhe. Ali Khamis Bakar
|
Mjumbe
|
4.
|
Mhe. Salma Mussa Bilal
|
Mjumbe
|
5.
|
Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed
|
Mjumbe
|
6.
|
Mhe. Suleiman Makame Ali
|
Mjumbe
|
7.
|
Mhe. Maryam Thani Juma
|
Mjumbe
|
8.
|
Ndg. Ali Alawy Ali
|
Katibu
|
9.
|
Ndg. Haji Jecha Salim
|
Katibu
|
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora katika kusimamia na kutekeleza Bajeti yake,inatekeleza jumla ya Mafungu
matano (5) ambayo ni Fungu E 06 – Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Fungu E 02 –
Kamisheni ya Utumishi wa Umma, Fungu E 03
– Tume ya Utumishi wa Umma, Fungu E 04
– Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na Fungu E 05 – Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na
Uhujumu wa Uchumi Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ina jumla ya Programu kuu nne (4) ambazo ni:
(i)
Usimamizi na Uendelezaji wa Utumishi wa Umma;
(ii)
Huduma za Serikali Mtandao;
(iii) Usimamizi wa Utawala Bora; na
(iv)
Uendeshaji na Uratibu wa Ofisi ya Rais Uumishi wa Umma na
Utawala Bora.
Hata
hivyo, Kamati yetu haikujadili fungu nambari4 la Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti
wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa vile
fungu hilo lilipitiwa na Kamati ya PAC.
FUNGU E 06: OFISI YA RAIS – UTUMISHI WA UMMA NA
UTAWALA BORA
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza na kusimamia dhana
ya Utawala Bora nchini, Kamati yetu imeridhishwa sana na utekelezaji wa
programu mbali mbali ambazo zimepangwa kwa lengo la kuendeleza Utawala Bora
baada ya kuona taasisi zinazohusika na usimamizi wa masuala haya zimepiga hatua
kubwa za kuitetea Nchi yetu na kusimamia Haki katika jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa elimu bora ndio msingi wa
maendeleo na utendaji bora ambayo pia hujengwa kwa misingi imara ya elimu.
Kamati yetu imeridhishwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa programu za masomo
na maendeleo ya Chuo cha Utumishi wa Umma (IPA)
kwa jinsi walivyojipanga katika kuhakikisha kuwa maendeleo endelevu yanafikiwa
kwa kutumia dira na malengo ya elimu wanayotoa. Aidha, Kamati inazishauri
Taasisi zote za Serikali na zile zisizo za Serikali kukitumia Chuo hiki kwa
kuwapatia watendaji wao mafunzo ya muda mfupi kwa mwaka huu ambao nchi nyingi
duniani zimezuia kutoa mafunzo ya aina hii kutokana na athari za corona.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia makadirio ya Bajeti ya
mwaka2020/2021, Kamati inaishauri
Serikali kukiwezeshana kukijengea uwezo wa kufanya tafiti Chuo hiki ili kiweze
kufanya tafiti mbali mbali za kitaalamu ambazo ni dhahiri zina mchango mkubwa
kwa Serikali na maendeleo ya nchi yetu. Aidha, Kamati inaishauri Serikali kukipatia
Chuo hiki walimu wenye uzoefu katika kada mbali mbali ambao watakiwezesha Chuo
hiki kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
FUNGU E 02: KAMISHENI YA UTUMISHI WA UMMA
Mheshimiwa Spika, Kamisheni ya Utumishi wa Umma, miongoni
mwa programu zake ni Usimamizi wa Utumishi wa Umma na Usimamizi wa Nidhamu na
Maadili ya Utumishi wa Umma. Kamati imebaini kuwepo kwa changamoto kubwa kwa baadhi
ya watumishi wa Umma kushindwa kuzifahamu kikamilifu Sheria ya utumishi wa Umma
na Kanuni zake ambapo kupelekea kutoweka kwa nidhamu za kiutumishi katika
maeneo yao ya kazi, hali ambayo inaathiri kwa kiasi kikubwa uwajibikaji wao
kazini.
Aidha, Kamati inashauri utaratibu maalum uandaliwe wa
kutolewa mafunzo kwa watumishi licha ya mafunzo ya awali yanayotolewa kwa
waajiriwa wapya lakini ipo haja kwa watumishi wakongwe ambao wana uzoefu wa
kutosha katika utekelezaji wa majukumu yao, kupatiwa elimu juu ya sheria na
miongozo ya kazi. Mafunzo haya yatapunguzakwa kiasi
kikubwa tabia mbaya kwa waajiriwa.
FUNGU E 03: TUME YA UTUMISHI SERIKALINI
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Tume ya Utumishi Serikalini
ina wajibu na jukumu la kusimamia watumishi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kushirikiana na tume nyenginezo za kiutumishi, Kamati inashauri
kuzidi kusimamia watumishi wa Serikali katika kuhakikisha wanapata haki zao
zote za msingi sambamba na kuimarika kwa maslahi yao ya msingi.
Vile
vile, Kamati inashauri Tume hii kusimamia kikamilifu na kuona kwamba watumishi
wa Serikali wanapatiwa fursa zaidi za kujiendeleza kielimu kwa misingi kwamba
elimu bora ndio msingi wa maendeleo katika Taasisi yoyote katika Nchi yetu.
Aidha, Kamati inaishauri Tume kufuatilia kwa karibu hali za watumishi wa Umma
na kuona namna wanavyojikinga na maambukizi ya virusi vya corona na kupelekea
kupotea kwa rasilimali watu katika nchi.
FUNGU E 05: MAMLAKA YA
KUZUIA RUSHWA NA UHUJUMU WA UCHUMI
Mheshimiwa
Spika,
wajibu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ni Taasisi yenye jukumu
la kuhakikisha makosa yanayohusiana na rushwa na uhujumu wa uchumi yanapungua
nchini. Mamlaka hii inatarajia kuhakikisha kwamba Mfumo wa Utawala Bora na
Muundo wa Serikali unakuwa wa wazi na wenye uwajibikaji wa kupingana na vitendo
vya rushwa.
Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhishwa na kipaumbele cha Ofisi
hii katika ujenzi wa jengo la kudumu la Ofisi ya ZAECA huko Tunguu na hivyo,
Kamati inaiomba Serikali pia,kuliingiza katika vipaumbele vyake suala hili ili
ujenzi huu ufanyike kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kuwepo kwa baadhi ya
changamoto ambazo zinarudisha nyuma juhudi za watumishi wa Ofisi hii Unguja na
Pemba. Katika kutekeleza majukumu hayo, Kamati imebaini wapo baadhi ya
watendaji wa Ofisi za Serikali na zile za binafsi kutotekeleza majukumu yao
ipasavyo jambo ambalo linawanyima haki raia wasiokuwa na uwezo kiuchumi na
kusimamia haki zao kisheria. Licha ya hayo, kwa kuwa maadili ya viongozi ni
jambo lenye nafasi kubwa katika uimarishaji wa utawala Bora nchini, taasisi hii
kwa kushirikiana na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma inashauriwa kuwachukulia
hatua viongozi wote wenye kuvunja maadili na desturi za uongozi ambao wanaonesha
taswira mbaya katika ujenzi wa utawala bora.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kuchukuwa fursa hii
kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha maoni machache sana ya Kamati
yangu, kwa niaba ya Kamati pamoja na kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza
lako kwa kunisikiliza kwa umakini mkubwa wakati wote wa uwasilishaji wa maoni
yetu.
Kamati
pia, inatoa shukrani zake za dhati kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi ndugu
Raya Issa Mselem, Mratibu wa Shughuli za Kamati ndugu, Khamis Hamad Haji pamoja
na watendaji wote kwa ujumla wa Afisi ya Baraza la Wawakilishi ambao wameisaidia
sana Kamati hii kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, nachukuwa nafasi hii ya pekee
kuwashukuru kwa dhati kabisa Makatibu wetu wa Kamati kwa namna walivyoweza
kutekeleza vyema majukumu yao katika kipindi chote cha uhai wa Kamati hii na
wakati wa kujadili makadirio ya Bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, mwisho
kabisa, Kamati inawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako waichangie Bajeti
hii na hatimae waiidhinishie Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
makadirio ya fedha zilizopangwa kutumiwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 ili wapate kutekeleza majukumu
yao ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kamati yangu Naomba Kuunga Mkono Hoja.
Ahsante,
(Mhe. Salma Mussa Bilal)
Mjumbe,
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar
No comments:
Post a Comment