Habari za Punde

Lina Medina msichana aliyezaa akiwa na miaka mitano

Na Ali Shaaban \Juma


Muuguzi akiwa  mtoto wa Lina Medina aliyelala kitandani baada ya kujifungua akiwa na umri wa miaka mitano hapo mwaka tarehe 14 Mei, 1939.



Katika hali isiyo  ya kawaida, msichana aitwae Lina Medina ameweka kumbukumbu duniani kwa kuwa mwanamke mwenye umri mdogo kabisa kubeba mimba na  kujifungua.
Lina Medina alizaliwa  tarehe 13 Septemba, 1933 katika mji wa Ticrapo huko nchini Peru. Baba yake mzazi ni muhunzi aliyeitwa Tiburelo Medina na mama yake ni Victoria Losea.

Akiwa na umri wa miaka mitano, binti huyo aliumwa na ndipo wazazi wake walipoamua kumpeleka hospitali wakilalamika kuwa mtoto wao huyo amekuwa akisumbuliwa na tumbo kwa muda mrefu. Kama ilivyo kawaida, baada ya kufikishwa katika hospitali ya mji wa Pisco na kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu, madaktari wa hospitali hiyo walipigwa na mshangano pale walipogundua kuwa msichana huyo wa miaka mitano alikuwa na mimba ya miezi saba.

Daktari aitwae Geraldo Lozada wa hospitali hiyo ndiye aliyepewa jukumu la kumsimamia binti huyo. Kutokana na kuwa binti huyo alikuwa na mimba akiwa na umri mdogo, Dakatari Lozada alishauri msichana huyo apelekwe katika hospitali kuu ya nchini Peru iliyoko katika mji mkuu wa nchi hiyo Lima. Baada ya kufikishwa katika hospitali kuu ya mjini  Lima na kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kitaalamu, madaktari waligundua kuwa binti huyo alizaliwa na hali isiyo ya kawaida ya kukuwa kwa viungo vya uzazi katika umri mdogo ambayo kitaalamu inajulikana kama “precocious puberty”.

Kwa ufupi hali ya “precocious puberty” humfanya msichana kuvunja ungo mapema na kupata mzunguko wa damu ya hedhi katika umri mdogo kulika hali ya kawaida. Kitaalamu katika hali ya kawaida msichana, huvunja ungo akiwa na wastani wa kati ya  miaka 10 hadi 11.

Uchunguzi ulofanywa na madaktari kwa binti huyo ulibaini kuwa alivunja ungo na kupata mzunguko wa damu ya hedhi akiwa na umri wa miaka miwili na nusu au mitatu na alichuchua maziwa akiwa na miaka minne.

Akiwa na miaka mitano, tayari viungo vya uzazi vya binti huyo vilikuwa tayari  kupokea na kulea  mimba.
Lina Medina na mwanawe wa kiume aitwae Gerardo ambae alipokuwa  mdogo alidhani kuwa mama huyo  ni dada yake.



Lina Medina alijifungua tarehe 14 Mei, 1939  akiwa na umri wa miaka mitano, miezi saba na siku 21 akiwa ndiye mwanamke aliyeweka historia duniani kuzaa akiwa na umri mdogo. Alijifungua kwa operesheni maalum iliyofanywa na madaktari watatu ambao ni  Dakatari Lozada akishirikiana na Busalleu na Daktari Colareta. Mtoto huyo wa kiume alikuwa na uzito wa ratili 6 (Gramu 2,700) na alipewa jina la Geraldo la mkunga aliyemzalisha mama yake.  Binti huyo alitoka hospitali na mwanawe wakiwa na afya nzuri baada ya  siku chache.

Kwa vile tukio hilo  si la  kawaida, kulijengeka dhana katika jamii ya taifa la Peru kuwa binti huyo alibakwa na kupata mimba hiyo. Awali, polisi walimkamata baba mzazi wa mtoto huyo kwa tuhuma za kumbaka binti yake, lakini baadae aliachiwa kwa kukosekana ushahidi.

Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na watu kadhaa kutaka binti huyo amtaje aliyempachika mimba hiyo, Lina Medina hakumtaja aliyempa uja uzito huo. Hata hivyo kwa mujibu wa mapitio ya kesi hiyo yalofanywa mwaka 1955, ilionekana kuwa makabila mengi ya wahindi wekundu wanaoishi sehemu za vijijini huko nchini Peru na Marekani ya kusini kwa ujumla yana sherehe nyingi za jadi ambazo hatimae  hutoa fursa ya ubakaji wa wasichana na wanawake na hatimae kusababisha uja uzito usiotarajiwa.

Geraldo alikuwa akiamini kuwa Lina Medina ni dada yake na alijua kuwa huyo ni mama yake alipofika umri wa miaka kumi ambapo katika mwaka 1979, kijana huyo alijihusisha na harakati za afya ya uzazi katika jamii hadi alipofariki dunia kutokana na maradhi ya mifupa akiwa na miaka 40.

Lina Medina aliajiriwa kama katibu muhutasi katika hospitali binafsi ya Dokta Lozada huko mjini Lima, ambapo pia Daktari huyo alimsaidia binti huyo kujiendeleza kielimu pamoja na mtoto wake. Baadae katika mwaka 1972, Lina Media aliolewa na Raul Jurado ambapo walikuwa wakiishi  katika mtaa uitwao Chicago Chico mjini Lima.  Alijifungua mtoto wake wa pili  miaka 33 baada ya kuzaa mtoto wake wa kwanza alipokuwa na miaka mitano.

Mara kadhaa binti huyo alifuatwa na vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo magazeti, Televisheni na Redio maarufu za Marekani na Canada kwa ajili ya kufanywiwa mahojiano ambapo alikataa.

Kwa mara ya mwisho, Lina Medina alifuatwa na wandishi wa habari wa Shirika la Habari la Uingereza “Reuters” hapo mwaka 2002 kwa ajili ya mahojiano ambapo pia alikataa.

Katika miaka  ya hivi karibuni, nyumba anayoishi na mumewe imevunjwa kwa ajili ya utanuzi wa barabara ambapo amelalamikia kulipwa fidia  ndogo ya nyumba yao  ambapo pia fidia iliyoahidiwa na serikali kutokana na kujifungua akiwa  na umri mdogo hakupewa hadi leo.

Soma makala hii na nyenginezo katika Blog ya Rafikifumba.com 

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.