
Na Ali Shaaban Juma
Chai ni kinywaji maarufu duniani ambapo katika baadhi
ya mataifa zao hilo ni moja kati ya mazao ya biashara yanayoingiza fedha za
kigeni kwa mataifa hayo.
Kihistoria, Chai ni moja kati ya vinjwaji
vikongwe kabisa duniani. Wanahistoria wengi wankubaliana kuwa kinywaji hicho
asili yake ni China ambako inasadikiwa kuwa kinywaji hicho kilianza kunywewa
kiasi miaka 5,000 iliyopita.
Kumbukumbu hizo za kihistoria zinaeleza kuwa
miaka Elfu tano iliyopita, mtawala mmoja wa China aliona majani yaliyodondoka
katika chungu cha maji ya moto aliyoteleka. Mtawala huyo alionja maji hayo na
ladha yake aliipenda na pia alipata uchangamfu fulani kutokana na kinywaji
hicho. Hali hiyo ilitokea kwa bahati tu ambapo mtawala huyo aliendelea kunywa
kinywaji hicho kwa kuchemsha majani ya mmea huo katika maji. Kuanzia hapo chai
ikaanza kupata umaarufu huko China na kuwa ni kinywaji cha kawaida miongoni mwa
watu wa enzi hizo.
Nadharia nyengine inaeleza kuwa kabla ya hapo, miaka 800 baada ya kuzaliwa Nabii
Issa tayari mtawala mmoja wa Kibuda aliandika historia ya matumizi ya chai.
Mtawala huyo alieleza kuwa kinywaji hicho kinasaidia utulivu na usikivu katika
mahubiri ya dini ya Kibuda.
Kwa upande mwengine, Wamishonari wa Kibuda huko
nchini Japan enzi hizo walitumia chai kuwa ni kinywaji cha lazima katika
mahubiri na ibada zao. Baadae Chai ilifika nchini India ambako pia waumini wa
Kibuda walitumia kinywaji hicho wakati wa usiku wanaposimulia hadithi za Buda.
Baada ya chai kupata umaarufu huko nchini
Japan, Wajapani wa enzi hizo walianzisha utamaduni wa karamu maalum ya chai
iliyoitwa “Cha-no-yu” maneno ambayo tafsiri yake ni “maji ya moto kwa chai”.
Utamaduni huo ulizoeleka haraka miongoni mwa
Wajapani ambapo kulitengenezwa vibaku maalum vya kutilia chai hiyo ambapo ili
kuonesha heshima anayekunywa chai hiyo hutakiwa kukaa kitako na mtindo maalum.
Mwandishi wa habari na mwanahistoria mwenye
asili ya Ugiriki na Ireland aitwae Lafcadio Hearn ambae ni mmoja kati ya watu
wachache kutoka nje ya Japan kupata uraia wa taifa hilo enzi hizo aliandika kwa
urefu kuhusiana na utamaduni huo wa Wajapan wa kunywa chai.
Biashara kati ya bara Ulaya na China na Japan
ilianza katika karne ya 13 ambapo Wazungu kutoka Ulaya waliokwenda huko China
na Japan kufanyabiashara walianza kupata taarifa ya kuwepo kinywaji hicho. Pole
pole wafanyabiashara hao kutoka Ulaya walianza kunywa chai na kuzoea kinywaji
hicho. Ingawa katika hatua hiyo chai ilikuwa bado kujulikana barani Ulaya,
lakini tayari taarifa ya kuwepo mmea huo unaochemshwa na kunywea na watu
ilianza kufika barani Ulaya.
Katika kipindi hicho, hakuna mfanyabiashara
aliyebainisha ni vipi chai inalimwa au inapikwa huku kukiwa na maelezo tofauti
kuhusu jinsi chai inavyopikwa. Kuna wale walodhani kuwa Chai ilipikwa kwa
kuchemsha maji yaliyotiwa chumvi ambapo wengine walidhani kuwa kinywaji hicho
kilipikwa kwa kuchemshwa maji yanayochanganywa na asali au mimea mengineyo.
Dhana hiyo ya upishi
wa chai iliondoka barani Ulaya hapo mwaka 1560 pale Wamishonari wa Ureno
walipoanzisha njia ya biashara kati ya China na bara Ulaya kwa kupitia Ureno na
Uholanzi. Wamishonari hao walikuwa ndio watu wa mwanzo kuingiza chai barani
Ulaya. Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha chai kutoka China hadi Uholanzi
enzi hizo, Chai ilikuwa ni kinywaji cha matajiri na hivyo moja kwa moja
kuongeza umaarufu wa kinywaji hicho barani Ulaya hasa miongoni mwa matajiri wa
Uholanzi.
Kutokana na kwamba
bado chai ilikuwa ni kinywaji kipya barani Ulaya, kulikuwa na mabishano
miongoni mwa madaktari, wasomi na hata waliouza dawa za kienyeji kuhusu usalama
wa kinywaji hicho kwa binaadamu. Baadhi ya watu hao walitilia shaka usalama wa
kinywaji hicho cheusi na kichungu. Marumbano hayo yalidumu kwa miaka kadhaa
Kutokana na
kuongezeka kwa vyombo vya usafiri kiwango cha chai iliyoingizwa barani Ulaya
kutoka China kiliongezeka katika miaka 1600 na hivyo kufanya kinywaji hicho
kupungua bei na kuongezeka wanywaji. Baadhi ya wanyaji chai wakati huo walianza
kugundua kuwa kinywaji hicho kilikuwa kikichangamsha kinyume na dhana potofu
iliyokuwepo kuwa kinywaji hicho si kizuri kiafya.
Baada
ya chai kuanza kupata umaarufu huko Ureno na Uholanzi, katika mwaka 1652 kinywaji
hicho kilianza kuuzwa sokoni mjini London nchini Uingereza pamoja na kahawa na
Kakao. Hadi kufikia mwaka 1700, Uingereza ilikuwa ikiingiza nchini humo wastani
wa Ratili 240,000 za chai kutoka China. Chai ilizidi kupata umaarufu nchini
Uingereza ambapo watu wa taifa hilo walikifanya kinywaji hicho kuwa rasmi
wakati wa asubuhi na usiku. Ni katika kipindi hicho ambapo utamaduni wa kualika
watu katika chai rasmi ya usiku ulipoanza nchini Uingereza.
Kampuni
kubwa ya biashara ya Uingereza enzi hizo iitwayo “East India Trading Company”
ilikuwa ndio muingizaji mkuu wa Chai nchini Uingereza kwa vile kampuni hiyo
ilikuwa ikifanya misafara ya baharini kati ya Uingereza na India. Kuongezeka
kwa mahitaji ya chai barani ulaya kusababisha kuwepo kwa ushirika wa kibiashara
wa zao hilo kati ya Ureno, Uingereza, India na China. Kwa wakati huo, China na
India walikuwa ni wazalishaji wa chai na Uingereza na Ureno walikuwa ni
wanunuzi na wasafirishaji wa zao hilo kwenda barani Ulaya.
Hata hivyo
kutokana na tama ya kipato kati ya washirika hao wa biashara, kulizuka
sitofahamu na ndipo kampuni ya Uingereza ya East India Trading Company
ilipohodhi njia ya biashara ya mwambao wa pwani ya India na kuwafukuza Wadachi
na Wafaransa.
Waingereza hao
badala ya kununua na kusafirisha chai, waliwalazimisha wakulima wa India kulima
Mirungi waliyopeleka huko China ambako walibadilisha majani hayo kwa chai.
Biashara hiyo ya
mirungi ndiyo iliyosababisha kuzuka kwa vita vya mirungi, “Opium War” katika
miaka ya 1800 na kusababisha kuporomoka kwa himaya ya biashara ya chai ya Waingereza katika bara la Asia.
Mwanzo mwa karne
ya 19, chai ilisababisha mabadiliko makubwa ya kijamii barani Ulaya na
Marekani. Katika mwaka 1864, mwanamke mmoja aliyemiliki duka la mikate aliweka
meza za kunyea chai mbele ya duka lake na kuwabembeleza wale walonunua mikate
kukaa katika viti hivyo na kunywa chai
pamoja na mikate walonunua.
Duka hilo lilipata
umaarufu mkubwa ambapo pia baadhi ya watu walikutana hapo na kubadilishana
mawazo. Kwa vile chai sio kilevi, mwanamke huyo hakupata kikwazo cha kuendesha
biashara hiyo ambapo si muda mrefu baadae katika maeneo mengine huko nchini
Uingereza mikahawa kadhaa ya chai ilianzishwa na kupata umaarufu.
Biashara ya
watumwa ilifanyika kati ya bara la Amerika na Afrika ilichangia kuenea kwa zao
hilo hasa katika visiwa vya Caribbean, Afrika na Marekani ambako mashamba
makubwa yalianzishwa kwa kutumia vibarua watumwa. Kutokana na kuongezeka kwa
mahitaji ya chai duniani, makampuni kadhaa makubwa yaliyouza bidhaa hiyo
duniani yalianzishwa barani ulaya mwanzoni mwa karne ya 19.
Viwanda vya
kusafiru na kushindika chai vilijengwa barani Ulaya ambapo zao hilo lililimwa
kama mali ghafi barani Afrika na Asia na kusafirishwa nje na makampuni makubwa
ya Ulaya. Baadhi ya makampuni makubwa ya Ulaya yanayouza chai duniani ni pamoja
na Brooke Bond, PG Tips, Lipton na Limtex.
No comments:
Post a Comment