Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadam Tanzania

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akikabidhiwa  Taarifa ya Mpango Kazi wa Tume ya Haki za Binaadamu kwa mika mitano na Mwenyekiti wa  Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania  Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina, hafla  hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Zanzibar Vuga Jijini Zanzibar leo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seiof Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina uliofika Ofisini kwake kujitambulisha rasmi.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina  akielezea mikakati ya Tume yake wakati alipofika na Wajumbe wake kujitambulisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi Seif Ali Iddi Kati kati akiwa katika Picha ya pamoja na Wajumbe wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania walioongozwa na Mwenyekiti wao Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mbiha Kulia ya Balozi Seif.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina Kushoto wakibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seiof Ali Iddi   mara baada ya mazungumzo yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis. OMPR.
Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania ina wajibu wa kufanya kazi kwa karibu Zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  pale inapotekeleza majukumu yake kwa lengo la kuwatumikia vyema Wananchi wa pande zote Mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufanya hivyo kutaisaidia Serikali Kuu kupata nguvu na uwezo wa ziada wa kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi hususan Wanawake, Watoto na hata Wananchi wenye mahitaji Maalum.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazugumzo yake na Uongozi wa juu wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina ulipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Balozi Seif alisema Tume ya Haki za Binaadamu ina kazi kubwa katika kutekeleza majukumu yake  kwa upande wa Zanzibar kutokana na migogoro na changamoto nyingi zinazowakabili Wananchi hali inayosababisha mitafaruki na mifarakano miongoni mwa Jamii yenyewe.
“ Tume ya Haki za Binaadamu ina jukumu kubwa la kusaidia kutatua migogoro na mifarakano inayotokea na kuwasumbua Wananchi katika maeneo tofauti Nchini”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Uongozi huo wa Tume ya Haki za Binaadamu kwamba yapo matatizo mengi yanayowakabili Wananchi hasa Wanawake ya kupewa ovyo Talaka na matokeo yake kutelekezwa kunakokwenda sambamba na kuachiliwa Watoto bila ya huduma.
Alitahadharisha kwamba tabia hii iliyoanza kuota mizizi kwa baadhi ya Wanaume wasiojali utu wa Binaadamau ni ya hatari kwa Mtoto kwa vile inawakosesha haki zao za Msingi kama Elimu na Huduma za Afya.
Balozi Seif alieleza kwamba hivi sasa udhalilishaji wa Wanawake na Watoto ni janga lilnaloikumba Dunia. Hivyo Watendaji na Viongozi wa Tume ya Haki za Binaadamu lazima wajikite Zaidi kushirikiana na Vyombo vya Dola pamoja na Wananchi katika vita vya kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kupotoshwa kwa Maadili ya Jamii.
Katika kuimarisha utendaji wa Tume ya Haki za Binaadamu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi huo kuandaa Mpango Maalum wa kujenga Majengo ya Kudumu ya Ofisi zake Visiwani Zanzibar wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa maeneo ya Ujenzi huo wakati wowote pale itapohitajika kutekelezwa Mpango huo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uwepo wa huduma za Ofisi na Majengo Visiwani Zanzibar mbali ya kuendeleza ile dhana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lakini pia mfumo huo utawarahisishia Watendaji wa Tume hiyo kufanya Kazi zao kwa ufanisi mzuri.
Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina alisema Taasisi hiyo ni Chombo cha Umma kilichoundwa kusimamia upatikanaji wa Haki za Binaadamu ili kusimamia Utawala Bora hapa Nchini.
Hata hivyo, Jaji Mathew alisema Watendaji wa Tume hiyo ni Binaadamu wanaoweza kuteleza  katika Utekelezaji wa majukumu yao . Hivyo Viongozi Wakuu wanapaswa kushauri pale Watendaji hao wanapoteleza katika maeneo yao ya Kazi.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi kubwa na ngumu inayofanya ya kuhudumia Wananchi jambo ambalo Uongozi wa Tume hiyo unaliunga mkono.
Wajumbe wa Tume ya Haki za Binaadamu Tanzania waliteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mnamo Tarehe 19 Septemba Mwaka 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.