Habari za Punde

Tamko la Serikali kuhusu kufunguliwa kwa skuli tarehe 29/06/2020

SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI

TAARIFA KWA UMMA

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU KUFUNGULIWA KWA SKULI LILILOTOLEWA NA MHE. RIZIKI PEMBE JUMA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR

Ndugu wananchi,
Ndugu walimu,
Ndugu wazazi /walezi na
Wanafunzi wote kwa jumla.

Assalaam alaykum,

Siku ya Jumamosi ya tarehe 20 Juni 2020, Rais wetu Mpendwa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein alitangaza kufunguliwa kwa skuli zote za Msingi na Sekondari ifikapo tarehe 29 Juni 2020. Hii imefuatia baada ya Serikali kuzifunga skuli zote tarehe 18 Machi 2020 kwa kuingianchini maradhi yanayosababishwa na virusi vya Korona (COVID-9). 

Kwa sasa, Serikali imejiridhisha na hatua zilizochukuliwa katika kupambana na maradhi hayo. Hali halisi inaonesha kuwa janga hilo la COVID-19 limepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hivyo, Serikali imeamua kuzifungua skuli ili watoto wetu waendelee na masomo yao wakiwa katika mazingira ya skuli zao. Mheshimiwa Rais, hata hivyo alisisitiza mashirikiano kwa jamii nzima yaendelee katika kuchukuwa tahadhari za kujikinga na maradhi hayo ili kuepusha maambukizi mapya.  

Ndugu Wananchi, Mheshimiwa Rais, pamoja na kuzifungua skuli, aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuandaa utaratibu utakaotumika baada ya kufunguliwa skuli hizo ili wanafunzi, walimu na jamii nzima waufuate kuhakikisha wanafunzi wetu wanasoma kwa salama na kuepusha maambukizi ya maradhi haya kwani yapo Duniani.

Ndugu Wananchi, napenda sasa kutoa utaratibu wa Utekelezaji kufuatia Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, kuzifungua skuli kwa ajili ya kuendelea na masomo.

Utaratibu

1. Skuli zote za Maandalizi, Msingi na Sekondari zitafunguliwa siku ya Jumatatu tarehe 29 Juni 2020.

2. Shughuli za masomo zitafanyika kwa siku zote za wiki kwa utaratibu wa shifti.

3. Uongozi wa skuli zote za Maandalizi, Msingi na Sekondari uhakikishe kuwa idadi ya wanafunzi kwa darasa wasizidi 40. Kwa skuli ambazo zina wanafunzi wengi, watafuata utaratibu maalum wa shift utaoelekezwa na Wizara. 

4. Kila skuli iimarishe mazingira ya usafi yanayohusiana na mapambano dhidi ya COVID-19 ikiwemo walimu, wanafunzi na wageni kunawa mikono kwa maji na sabuni, kuacha kusalimiana kwa kupeana mikono na kuvaa barakoa katika mazingira ya Skuli.

5. Katika kipindi hiki, masomo yataendelea bila ya skuli kufungwa mpaka wiki ya tatu ya mwezi Disemba 2020. Mapumziko yatakuwa kwa siku za Sikukuu za kitaifa tu. 

6. Uongozi wa skuli unatakiwa kusimamia utekelezaji wa miongozo itakayoandaliwa na Wizara katika kuhakikisha wanafunzi wanafuata maelekezo ya viongozi wao katika kujiepusha na maambukizi na hivyo kusoma kwa salama.

7. Wanafunzi wajiepushe na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima wanapokuwa katika maeneo ya skuli na nyumbani na kila mmoja awe mlinzi kwa mwenziwe.

8. Wafanyabiashara ndogondogo katika maeneo ya skuli wazingatie kanuni zote za Afya ili kuhakikisha kuwa huduma wanazozitoa kwa wanafunzi zipo salama.

9. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ na Wizara ya Afya zitafuatiliakwa karibu skuli zote ili kuhakikisha maagizo yote yaliyotolewa na Serikali yanatekelezwa kikamilifu.  

Hitimisho

Wizara inapenda kusisitiza kwa uongozi wa skuli zote, skuli zinapofunguliwa zihakikishe wanazingatia maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa na Wizara ya Afya katika kujikinga na virusi vya Korona. 

Vile vile, walimu wanatakiwa kuongeza bidii katika ufundishaji na kukamilisha mihutasari ndani ya mwaka huu kufidia muda uliopotea kwa kufungwa skuli. 

Aidha, Wizara inatoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatoa mashirikiano ya karibu ili kuwawezesha watoto wetu kusoma kwa usalama na kwa ufanisi mkubwa. 

Asanteni kwa kunisikiliza.

Tarehe: 25 Juni, 2020

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.