Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar yapokea msaada wa vifaa vya Tiba kutoka WHO

 Mwakilishi Mkaazi wa WHO Zanzibar Dk. Andemichael Ghirmy (kushoto) akimkabidhi Mkkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Jamala Adam Taib moja ya boksi la msaada wa vifaa vya afya uliotolewa na Shirika hilo katika Ofisi ya Wizara Mnazimmoja.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Jamala Adam Taib akitoa shukrani kwa Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dk. Andemichael Ghirmy baada ya kupokea msaada wa vifaa katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.   
Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo          
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeahidi kuendeleza mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha mifumo ya afya ya wananchi.

Mwakilishi Mkaazi wa WHO Zanzibar Dk.  Andemichael Ghirmy ametoa ahadi hiyo alipokabidhi msaada wa vifaa mbali mbali kwa Wizara ya Afya vikiwemo vya kupambana na maradhi ya Corona katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Wizara, Mnazimmoja, Mjini Zanzibar.

Dk. Ghirmy alisema WHO inathamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za afya na wanashawishika kuunga mkono juhudi hizo.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanikiwa katika mapambano dhidi ya maradhi ya Corona, na hali inaendelea vizuri, lakini amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwani nchi jirani bado ugonjwa huo upo na mizunguko ya watu inaendelea.

Akipokea msaada wa vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 95,657,500.00 Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Jamala Adam Taib alitoa shukrani kwa Shirika la Afya Duniani kupitia Mwakilishi wake wa Zanzibar Dk. Ghirmy kwa misaada inayotoa katika sekta ya afya.

Alisema misaada hiyo imefanikisha mapambano ya maradhi ya mripuko yanayotokea nchini na kusaidia katika kuwahudumia wagonjwa wa kawaida katika hospitali na vituo vya afya  Zanzibar.

Dk. Jamala amewataka wananchi wasijahau na waendelee kuchukua tahadhari na kufuata miongozo ya Wizara ya Afya katika kukabiliana na maradhi ya Corona ingawa maradhi hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa Zanzibar.

Vifaa vilivyotolewa vitatumika kwenye hospitali, vituo vya afya na kwa ajili ya tahadhari katika kambi zilizokuwa zikitumika kulaza wagonjwa wa Corona ambazo hivi sasa hazina wagonjwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.