Katika salamu hizo za Rambirambi, Rais Dk. Shein
alisema kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha mpendwa
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin
William Mkapa, kilichotokea mapema usiku wa kuamkia leo Ijumaa, tarehe 24,
Julai, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Salamu hizo zilieleza kuwa Rais Dk. Shein yeye binafsi
na kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, anatoa salamu za
rambirambi kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa msiba huo mzito.
“Tutamkumbuka Mheshimiwa Benjamin William Mkapa
kwa uongozi wake wa busara, uzalendo, ukweli na uwazi, sifa ambazo zimeweza
kuendeleza umoja na mshikamano wa Watanzania wote hasa katika ule wakati mgumu
wa mabadiliko ya kisiasa, ambapo Taifa letu liliingia katika mfumo wa vyama
vingi”, ilieleza sehemu ya salamu hizo za rambirambi alizotuma Rais Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein katika salamu hizo za rambirambi
alieleza kwamba kwa hakika kifo hicho kinaacha pengo kubwa kwa Watanzania, na
Afrika kwa jumla na wananchi wote wa Zanzibar wanaungana na Watanzania na
Waafrika wote kuomboleza msiba huo.
‘Kupitia kwako Mheshimiwa Rais, tunatoa salamu
zetu za pole kwa familia, ndugu, marafiki na jamaa wote wa marehemu”,ilieelza
sehemu ya salamu hizo.
Sambamba na hayo, salamu hizo za rambirambi
zilieleza kwamba kutokana na thamani kubwa aliyo nayo Rais mstaafu Benjamin
Mkapa kwa Watanzania, wanamuomba MwenyeziMungu amuweke mahala pema na awape
subira na ustahamilivu wafiwa na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha
msiba.
Kifo cha Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Benjamin Willium Mkapa kimetokea usiku wa kuamkia leo
ambapo kiongozi huyo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa kwa taifa usiku
wa kuamkia leo kupitia televisheni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dk. John Pombe Joseph Magufuli kutoka Jijini Dodoma.
Kufuatia
kifo hicho, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza siku saba za
maombolezo ambapo bendera itapepea nusu mlingoti. Rais mstaafu Mkapa ambaye alizaliwa tarehe 12
Novemba mwaka 1938 alishika nyadhifa hiyo kubwa zaidi Tanzania kuanzia mwaka
1995 hadi mwaka 2005 baada ya kumaliza awamu zake mbili za uongozi wake.
Rais Mstaafu
Benjamin Willium Mkapa atakubukwa kwa uongozi wake mkubwa uliotukuka ndani na
nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kwa upande wa Umoja wa Mataifa (UN),
hayati Mkapa atakumbukwa kwa mchango wake katika diplomasia ya kuleta amani,
hususan baada ya kustaafu.
Tarehe 21
mwezi Septemba mwaka 2010, aliteuliwa na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Ban Ki-Moon kuongoza jopo
la kusimamia kura ya maoni ya kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka Sudan.
Mkapa akiongozana na wajumbe ambao ni Antonio Monteiro,
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ureno na Bhoiraj Pokharel, Mwenyekiti wa
zamani wa Tume ya Uchaguzi nchini Nepal, walitembelea mara kadhaa Sudan
kuhakikisha ufanikishaji wa kura hiyo ya maoni.
Kura ya maoni
ya Sudan Kusini kujitenga kutoka Sudan ilifanyika kuanzia tarehe 9 hadi 15
Januari mwaka 2011 na matokeo ya kura hiyo yalidhihirisha nia ya Sudan Kusini
kujitenga na hatimaye ikapata uhuru tarehe 9 Julai mwaka 2011.
Aidha, kutokana
na uwezo wake wa diplomasia ya usuluhishi, Mkapa ambaye pia, aliwahi kuwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania aliteuliwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, EAC, kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi ambapo ilikuwa
inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment