Habari za Punde

MAJALIWA AREJESHA FOMU ZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya  Ruangwa, Frank Chonya ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, fomu za kuwania Ubunge wa Jimbo la Ruangwa kupitia CCM,,wakati aliporejesha fomu hizo kwenye Ofisi ya Mukurugenzi huyo, 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhiwa barua na kupita bila kupingwa katika jimbo la Ruangwa kwa nafasi ya Ubunge na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya  Ruangwa, Frank Chonya ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ruangwa, Agosti 25,2020.Kulia ni Mkewe Mary Majaliwa. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha  barua ya kupita bila kupingwa katika jimbo la Ruangwa kwa nafasi ya Ubunge baada ya kukabidhiwa barua  hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya  Ruangwa, Frank Chonya ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ruangwa, Agosti 25,2020.Kulia ni Mkewe Mary Majaliwa.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Agosti 25, 2020 ametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) KUPITIA msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kupita bila kupingwa katika nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Ruangwa.

Akitangaza matokeo hayo kwenye viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Frank Chonya amesema Mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Majaliwa ndiye pekee aliyekidhi vigezo vilivyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kumfanya kupita bila kupingwa.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa amepita bila kupingwa, Mheshimiwa Majaliwa amesema anawashukuru  wanaCCM, Viongozi na  wanachama wa vyama rafiki  na wana Ruangwa kwa ujumla  kwa heshima waliyompatia na kumwezesha kupita bila kupingwa.

“Sisi wanaRuangwa  wote bila kujali siasa zetu tunajua tulikotoka na wilaya hiitunajua changamoto tulizonazo kwenye wilaya hii lakini tunajua hatua tuliyoifikia sasa hivi  na kauli zenu zilikuwa zinaangalia tunakokwenda na uwezekano wa kutatua changamoto huko mbele na ndiyo kwa sababu basi mwakilishi huyu tumpe nafasi nyingine tena aendelee”.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameahidi kuwa ataendelea kuwa mtumishi wa wanaRuangwa, kuendelea kuwa mhudumu wao, kuwa mwakilishi wao katika maeneo mbalimbali na ataendelea kuwasemea.

“Ahadi yangu ni kuwatumikia wote bila kujali vyama vyenu vya siasa, makabila yenu, maeneo mnayotoka wala uwezo wenu.  Ninyi wote nawaona kuwa ni wazazi wangu, mama zangu, baba zangu, kaka zangu, dada zangu lakini pia wadogo zangu”.


Pia Waziri Mkuu amesema kuwa Ruangwa imepata heshima kubwa kutoka kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumsaidia kazi  ambayo pia iliwezesha kutatua matatizo mbalimbali katika wilaya ya Ruangwa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.