Habari za Punde

TIC na Serikali Mkoani Lindi waanzisha Dawati la Uwekezaji kushughulikia Changamoto.

Na Mwandishi Wetu, Lindi.
Serikali Mkoani Lindi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC wameanzisha Dawati maalum la uwekezaji ambapo masuala yote yanayohusu uwekezaji sasa yanashughulikiwa  kupitia katika dawati hilo ambalo lengo lake ni kuwaweka karibu na kuwahudumia kwa upekee Wawekezaji wa Mkoa huo pamoja na kutangaza fursa zilizopo.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema uamuzi wa Serikali wa kuanzisha dawati hilo Mkoani Lindi umekuja kufuatia kuwepo kwa fursa nyingi za Uwekezaji ambapo kwa kushirikiana na TIC wameweza kuzitangaza.

Mhe. Ndemanga aliyasema hayo wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi Mkoani Lindi, ambapo alisema kufuatia Kongamano la Uwekezaji lililofanyika mwaka jana waliweza kubaini masuala kadhaa ambayo yatasaidia kuongeza Wawekezaji.

“ Hapa Lindi tumeanzisha Dawati la Uwekezaji ambalo linatuweka karibu sisi na Wawekezaji wetu. Pia Ofisi ya TIC katika Kanda ya Kusini inafanya kazi nzuri ya kuhamasisha uwekezaji hivyo kwa kushirikiana nao tumepanga mambo makubwa na tutafanikiwa sana” alisema Mhe. Ndemanga.

Alisema Wawekezaji wengi wanafika Mkoani humo ambapo sasa kupitia dawati hilo wataweza kuwa karibu na kuwahudumia ipasavyo ambapo pia alizitaja baadhi ya Taasisi zilizoonesha nia ya kuwekeza ikiwepo Chuo Kikuu cha Dar es Salaama (UDSM) wanaotaka kujenga Chuo cha Utafiti wa Mazao, Chuo cha Usafirishaji na Chuo Kikuu cha Kiisilamu cha Morogoro; ambavyo vyote vimepata maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo husika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi alisema hatua ya Mkoa wa Lindi ya kutenga maeneo yenye miundombinu ya uwekezaji pamoja na kuwa na kuanzisha Dawati la Uwekezaji ni ya kupongezwa na kuiomba Mikoa mingine kuiga mfano wao.

“Mkoa wa Lindi mnafanya kazi nzuri kwa kutenga maeneo, kuweka miundombinu na kuanzisha Dawati la Uwekezaji, mmerahisisha kazi hizi kwa sababu sisi wote nia yetu ni moja katika mbinu za kuvutia uwekezaji” Alisema Dkt. Kazi.

Aidha aliuomba Mkoa huo kuwa na taarifa za maendeleo ya miradi na kufuatilia endapo Mwekezaji aliyeweka nia ya kuwekeza na hajawekeza, ili kujua ni changamoto gani alizokumbana nazo ili zisiweze kujirudia ambapo pia aliwashauri kufuatilia kwa karibu miradi iliyo mbioni kuanza ili iweze kuendelea na hivyo kukuza uchumi wa Mkoa na Nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.